IQNA

Ban Ki-moon

Waislamu ni waathirika wakuu wa ugaidi duniani

18:38 - April 09, 2016
Habari ID: 3470236
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, amesema Waislamu ni waathirika wakuu wa ugaidi duniani.

Ban ameyasema hayo Ijumaa katika kongamano kuhusu kuzuia itikadi kali katili linaloendelea mjini Geneva Uswisi ambapo ameiomba nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuunga mkono mpango wake wa kupambana na ugaidi. Ban amesisisitza kwamba ugaidi hauhusiani na dini, kabila au taifa moja tu, bali unaathiri dunia nzima. Hata hivyo ameongeza kwamba wengi wa waathirika wa ugaidi ni Waislamu.
Katibu Mkuu amezingatia hatari ya tishio la ugaidi kwa mshikamano wa jamii, usalama wa kimataifa, na maadili ya Umoja wa mataifa. Amefafanua zaidi mpango wa Umoja wa Mataifa dhidi ya ugaidi, akieelezea kwamba cha msingi ni kuzuia vitendo hivyo visitokee kwa kukabiliana kwa pamoja na mizizi yake vikiwa ni pamoja na umaskini, ukosefu wa ajira na mivutano ya kisiasa.
Ameongeza kuwa, "Kuzuia itikadi kali katili kunapitia njia mbalimbali, lakini dharura zaidi ni kutunza na kuwezesha wavulana na wasichana. Wao ni wahanga mara mbili: Wanashawishiwa kujiunga na vikundi kali katili na pia wanashambuliwa kwenye sehemu za burudani, shule na vyuo.”

Kikao cha kimataifa cha kuzuia kuenea vitendo vya uchupaji mipaka mjini Gemeva Uswisi kimehudhuriwa na Mawaziri na Manaibu Mawaziri kutoka nchi 30 duniani. Kikao hicho kimefanyika katika hali ambayo kundi la magaidi wakufurishaji wa ISIS au Daesh katika miezi ya hivi karibuni limetenda jinai chungu nzima katika nchi za eneo hili khususan huko Iraq na Syria kwa kuungwa mkono kifedha na kijeshi na Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi na Kiarabu.

/3486831

captcha