IQNA

Kwa munasaba wa kuanza Wiki ya Umoja wa Kiislamu

Rais Rouhani akutana na Maulamaa wa Kisunni Iran na kusisitiza umoja wa Waislamu

11:18 - December 12, 2016
Habari ID: 3470737
IQNA-Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema uwepo wa dini na madhehebu mbali mbali hapa nchini umesaidia kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, Rais Rouhani aLIyasema hayo Jumapili mjini Tehran kwa mnasaba wa kuanza Wiki ya Umoja wa Kiislamu, alipokutana na maulamaa wa Kisunni hapa Tehran na kufafanua kuwa, uwepo wa dini na madhehebu tofauti haufai kutazamwa kama tishio, bali unafaa kuwa fursa ya kipekee ya kuimarisha umoja wa kitaifa, mshikamano na maendeleo.

Kiongozi wa taifa wa Iran amesema serikali inapania kutumia suala la dini na madhehebu tofauti hapa nchini kuelekea kwenye shina la umoja wa kitaifa na utamaduni. Rais Hassan Rouhani amesema tangu huko nyuma Jamhuri ya Kiislamu imekuwa ikisisitizia suala la kuimarishwa umoja na mshikamano pasina na kuruhusu kugawanywa kwa misingi ya dini na madhehebu.

Kwa upande wao, wanazuoni wa Kisunni hapa nchini wamesema kuna haja ya kuimarishwa umoja kati ya Waislamu wa madhehebu za Shia na Sunni sambamba na kueleza utayarifu wao wa kusaidia kulifikia lengo hilo.

Kadhalika wamelaani jinai za kutisha zinazofanywa na genge la kigaidi na kitakfiri la Daesh katika nchi za Iraq na Syria, nyuma ya pazia la dini.

Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu Hayati Imam Ruhullah Khomeini alitangaza tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal hadi tarehe 17 ya mwezi huu kuwa Wiki ya Umoja wa Kiislamu, kwa ajili ya kuimarisha umoja kati ya Waislamu wa madhehebu za Shia na Sunni.

Wiki ya Umoja wa Kiislamu

Inafaa kuashiria hapa kuwa Siku kama ya leo miaka 1490 inayosadifiana na tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal miaka 53 kabla ya Hijria, kwa kauli ya baadhi ya wanazuoni wa Kiislamu akiwemo Masoudi, alizaliwa Mtume Muhammad SAW. Wanachuoni wengine wa Kiislamu wanaamini kwamba, Mtume Muhammad SAW alizaliwa tarehe 17 Rabiul Awwal mwaka huohuo. Kwa msingi huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitangaza kipindi cha kuanzia tarehe 12 hadi 17 Rabiul Awwal kila mwaka kuwa ni Wiki ya Umoja kati ya Waislamu kote duniani. Wiki ya umoja ni fursa nzuri ya kuzikurubisha nyoyo za Waislamu na kuimarisha umoja na mshikamano wao katika kukabiliana na maadui wa ulimwengu wa Kiislamu.

3552936


captcha