IQNA

Rais wa Iran alaani hujuma ya Marekani Syria, asema imeimarisha magaidi

10:59 - April 08, 2017
Habari ID: 3470922
TEHRAN (IQNA)-Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani hujuma ya Marekani nchini Syria na kutoa wito kwa walimwengu kupinga sera kama hizo.

Katika ujumbe aliotuma kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter Ijumaa usiku, Rais Hassan Rouhani wa Iran ameongeza kuwa, sera za kivita za Marekani zitakuwa na matokeo mabaya na haraibifu kwa eneo na dunia nzima.

Ameongeza kuwa hujuma hiyo ya makombora ya Marekani nchini Syria ina maana ya kuyapa nguvu na kuyaimarisha makundi ya ugaidi na misimamo mikali katika eneo.

Rais Rouhani katika ujumbe wake huo amesema kutozingatia sheria na nidhamu duniani ni jambo linalolaaniwa kikamilifu.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia ameashiria tukio la mji wa Khan Sheikhun mkoani Idlib nchini Syria Jumanne iliyopita ambapo silaha za kemilkali zilitumiwa katika eneo hilo na kusema: "Tukio la Khan Sheikhoun nchini Syria ni la kushtua na linalaaniwa hasa na watu watu Iran ambao kwa muda wa miaka mingi walikuwa waathirika wa silaha za kemikali katika maafa ya Sardasht kaskazini magharibi mwa Iran."

Itakumbukwa kuwa Ijumaa Alfajiri, kwa kisingizio cha hujuma ya kemikali huko Khan Sheikhun, Marekani kwa kutumia manoari zake za kivita zilizo katika Bahari ya Mediterenea ilivurumisha makombora 59 ya Tomahawk katika uwanja wa jeshi la anga wa Shayrat katika mkoa wa Homs nchini Syria. Katika hujuma hiyo raia 9 waliuawa wakiwemo watoto wanne na watu wengine saba kujeruhiwa. Hii ni katika hali ambayo serikali ya Syria imekanusha madai kuwa ilitumia silaha za kemikali dhidi ya raia.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran Muhammad Javad Zarif jana Ijumaa aliandika katika ukurasa wake wa Twitter amelaani hujuma hiyo ya Marekani nchini Syria na kuongeza kuwa: "Marekani ilimsaidia Saddam Hussein dikteta wa zamani wa Iraq kutumia silaha za kemikali dhidi ya Iran katika muongo wa 80 na kisha nchi hiyo ikaishambulia Iraq kwa kisingizio kuwa ilikuwa na silaha za kemikali; na hivi sasa pia wanajeshi wa Marekani wanapigana vita pamoja na magaidi wa al Qaida na ISIS huko Yemen na Syria."

3462518


captcha