IQNA

Waislamu 8 Wauawa katika hujuma ya magaidi wa Boko Haram Msikitini Nigeria

11:44 - July 24, 2018
Habari ID: 3471605
TEHRAN (IQNA) - Waislamu 8 wameuawa baada ya magaidi wakufurishaji wa kundi la Boko Haram kuushambulia msikiti na kuua watu wanane mashariki mwa Nigeria wakati wa Sala ya Alfajiri.

Taarifa zinasema mlipuko ulitokea Jumatatu asubuhi saa kumi na moja na robo  katika wilaya ya Mainari Konduga katika jimbo la Borno.

Walioshuhudia wanasema mshambuliaji aliingia msikitini wakati wa sala ya Alfajiri na kujjilipua katika umati wa waumini Waislamu waliokua katika sala. Katika shambulio hilo la kinyama Waislamu  wanane walipoteza maisha papo hapo na watano wakajeruhiwa.

Waislamu wa kaskazini mashariki mwa Nigeria wamekuwa wakilengwa kwa muda mrefu na magaidi wa Kiwahhabi wa Boko Haram ambao huwakufurisha Waislamu wote wasiokubaliana  itikadi zao potovu. Misikiti na shule za Waislamu wasioafikiana na Boko Haran hulengwa mara kwa mara na kundi hilo la kigaidi.

Neno Boko Haram kwa ya lugha ya Kihausa, ambayo inatumiwa na aghalabu ya Waislamu wa Nigeria, lina maana ya 'elimu kutoka nchi za Magharibi ni haramu'.

Zaidi ya watu elfu 20 wamepoteza maisha nchini Nigeria tokea kundi la Boko Haram lianzishe uasi mwaka 2009 huku wengine zaidi ya milioni mbili wakilazimika kukimbia makazi yao kutokana na ugaidi wa Boko Haram ambao sasa umeenea katika nchi jirani kama vile Cameroon, Niger na Chad. Halikadhalika ugaidi huo wa Boko Haram umepelekea Waislamu wa kaskazini mwa Nigeria kubakia nyuma kimaendeleo na hivyo kuathiri vibaya mustakabali wao. Serikali ya Nigeria pia inalaumiwa kwa kuzembea katika kukabiliana namagaidi hao huku kukiwa na ripoti kuwa baadhi ya majenerali jeshini na maafisa wa serikali wanaofaidika na ugaidi huo wa Boko Haram.

3466391

captcha