IQNA

UN: China iwaachilie huru Waislamu Milioni 1 walio katika kambi za Ukomunisti

14:32 - September 02, 2018
Habari ID: 3471657
TEHRAN (IQNA)- Wataalamu wa haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa wametoa wito kwa China kuwaachilia huru mara moja Waislamu wanaoshikiliwa katika kambi za kuwafunza Ukomunisti na kwa kisingizio cha kukabiliana na ugaidi.

Taarifa zinasema wakuu wa utawala wa China wanawashikilia kwa nguvu Waislamu karibu milioni 1 wa jamii ya Uighur katika kambi zenye msongamano mkubwa ambapo wanafunzwa kwa lazima itikadi za Kikomunisti mkoani Xinjiang.

Waliowahi kuwa katika kambi hizo wanaema wanaoshikiliwa wanalazimishwa kula nyama ya nguruwe na kunywa pombe kinyume cha mafundisho ya Kiislamu.

Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Kuangamiza Ubaguzi wa Rangi imesema imeandika ripoti kuhusu masaibu ambayo Waislamu wanakumbana nayo katika kambi hizo. Wizara ya mambo ya Nje ya China imepinga ripoti hiyo kuhusu kukandamizwa Waislamu katika jimbo la Xinjiang. Ripoti hiyo inasema China inatumia kisingizio cha kukabiliana na ugaidi na misimamo mikali ya kidini kuwakandamiza Waislamu na kuwaweka katika kambi hizo.

Kamati hiyo ya Umoja wa Mataifa inasema, kwa mfano Waislamu wanakandamizwa hata kwa ajili tu ya kutoa salamu za Kiislamu za Assalam Aleikum. Aidha kamati hiyo imesema uchunguzi umebaini kuwa karibu Waislamu milioni moja wa jamii ya Uighur wanashikiliwa katika kambi hiyo.

Mkoa wa Xinjiang una wakazi Waisalmu zaidi ya milioni 10 kutoka kabila la Uighur na katika miaka ya hivi karibuni eneo hilo limeshuhudia makabiliano makali baina ya wanajeshi na Waislamu.

Serikali ya China imechukua hatua kadhaa kuwadhibiti Waislamu katika eneo hilo ikiwa ni pamoja na kumteuwa Mkomunisti mwenye misimamo mikali Chen Quanguo kuwa katibu wa chama tawi la Xinjiang tokea mwaka 2016.

3466665/

captcha