IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Kura ya maoni ifanyike kuainisha hatima ya Palestina

17:49 - June 05, 2019
Habari ID: 3471988
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbusha kuhusu pendekezo la Jamhuri ya Kiislamu la kufanyika kura ya maoni ya kuainisha hatima ya taifa la Palestina.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo Jumatano mjini Tehran katika Baraza la Idi wakati alipoonana na maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu, mabalozi wa nchi za Kiislamu na matabaka mbalimbali ya wananchi hapa mjini Tehran. 

Kiongozi Muadhamu ametoa mkono wa baraka na fanaka kwa Waislamu wote ulimwenguni kwa mnasaba wa sikukuu ya Idul Fitr na kusisitiza kuwa kadhia ya Palestina ni suala kuu zaidi la ulimwengu wa Kiislamu hivi sasa na amezilaumu zile nchi za Kiislamu ambazo zinashiriki katika ufanikishaji wa malengo haramu ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Katika kikao hicho, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu  ameashiria pendekezo hilo la Jamhuri ya Kiislamu la kufanyika kura ya maoni itakayowashirikisha wakazi wote wa Palestina; Waislamu, Wakristo na Mayahudi pamoja na wakimbizi wa Kipalestina ili wenyewe waamue ni mfumo wa aina gani wanataka utawale huko Palestina.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, nchi za Kiislamu zina wajibu wa kukabiliana na adui ghasibu anayetenda jinai huko Palestina na sio kuzozana zenyewe kwa zenyewe.

Ayatullah Khamenei amesema: Mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ni tofauti na mtazamo wa baadhi ya viongozi wa zamani wa Kiarabu ambao walikuwa wakiamini kuwa lazima Mayahudi watupwe baharini, bali Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tangu mwanzo kabisa ilikuwa inasisitiza kulindwa taifa la Paletsina na itaendelea kusimama imara kukabiliana na ulimwengu wa kiistikbari. (Ikumbukwe kuwa kuna tofauti baina ya Mayahudi na Wazayuni kwani Mayahudi na Wakristo ni sehemu ya wakazi wa Palestina kama walivyo Waislamu tofauti na Wazayuni).

Aidha amesema, mapambano ya kijeshi, kisiasa na kiutamaduni ya Wapaletina lazima yaendelee hadi pale wavamizi na maghasibu wa Kizayuni watakapoheshimu maamuzi ya taifa la Palestina. Kiongozi Muadhamu amesema kuwa vijana wa leo watapata taufiki ya kuishi na kuona siku ambayo taifa la Palestina litakombolewa na kurejea kwa Wapalestina.

3817284

captcha