IQNA

Kauli ya Kiongozi Muadhamu kuhusu jinai za hivi karibuni za utawala wa Bahrain

10:45 - August 01, 2019
Habari ID: 3472067
TEHRAN (IQNA) - Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha msimamo wake kuhusu jinai za hivi karibuni za utawala wa kiimla wa Bahrain ambao umewanyonga kidhalimu vijana wawili wapinzani katika nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi.

Ofisi ya Kulinda na Kusambaza Athari za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu imetangaza msimamo wa Ayatullah Ali Khamenei kuhusu jinai zinazofanywa na utawala wa Aal Khalifa huko Bahrain baada ya utawala huo kuwaua shahidi vijana wawili wa nchi hiyo kwa tuhuma bandia.
Ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu uliochapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kuhusu jinai ya hivi karibuni ya utawala wa Bahrain umesema: "Dhulma na ukandamiaji haviwezi kudumu na hatimaye azma na irada madhubuti ya mataifa yanayopigania uadilifu itashinda na kuibuka kidedea."
Ayatullah Ali Khamenei amekuwa akikemea na kulaani jinai na mauaji yanayoendelea kufanywa na utawala wa kiimla wa ukoo wa Aal Khalifa nchini Bahrain ukisaidiwa na Saudi Arabia dhidi ya wananchi wanaotaka mageuzi na utawala utakaochaguliwa na wananchi wenyewe.
Vijana Ali al-Arab, 25, na Ahmad al-Malali, 24, wa Bahrain walinyongwa siku kadhaa zilizopita kwa tuhuma bandia za eti kumuua afisa wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo.
Utawala wa kiimla wa Aal-Khalifa umewanyonga vijana hao licha ya mashirika ya kutetea haki za binadamu yakiwemo ya Amnesty International na Human Rights Watch pamoja na Umoja wa Mataifa kutoa miito ya kutaka kusimamishwa utekelezaji wa adhabu hiyo ya kifo.
Tangu Februari mwaka 2011, wakati ulipoanza mwamko wa Kiisamu Asia Magharibi, Bahrain imekuwa uwanja wa maandamano ya amani ya wananchi wanaopinga utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal Khalifa.
Wananchi hao wanataka kuwepo uhuru, utekelezwe uadilifu, ukomeshwe ubaguzi na kuundwa serikali itakayochaguliwa na wananchi wenyewe.
Hata hivyo kwa msaada wa wanajeshi wa Saudi Arabia na askari usalama wa Imarati waliotumwa nchini Bahrain kupitia mpango wa ulinzi wa Ngao ya Kisiwa, utawala wa Aal Khalifa unatumia mkono wa chuma kukabiliana na matakwa ya wananchi hao.
Kwa mujibu wa duru za haki za binadamu, Bahrain ina idadi kubwa zaidi ya wafungwa wa kisiasa kulinganisha na idadi ya watu katika nchi hiyo ndogo zaidi katika Ghuba ya Uajemi.

http://iqna.ir/fa/news/3831574

captcha