IQNA

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu atoa nasaha kwa Wanachuo

15:18 - August 23, 2010
Habari ID: 1979591
Husainia ya Imam Khomeini mjini Tehran, Jumapili, Agosti 22, 2010, imekuwa mwenyeji wa mkutano wa kidugu, kirafiki na kimapenzi kabisa kati ya maelfu ya wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya Iran na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei.
Katika mkutano huo wa masaa matatu, wawakilishi 12 wa jumuiya na makundi mbali mbali ya wanachuo nchini wamepata nafasi ya kutoa hotuba, mitazamo na mapendekezo mbali mbali kuhusu masuala muhimu sana ya kielimu na Vyuo Vikuu na masuala ya kiutamaduni, kijamiii, kisiasa na kiuchumi.

Baada ya hapo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amehutubia umati huo mkubwa akijibu na kutoa ufafanuzi wa baadhi ya masuala tata yaliyoulizwa na kuzungumziwa na wanachuo hao.

Ayatullah Udhma Khamenei amesema kwamba mkutano huo wa leo ulikuwa ni mojawapo ya mikutano mizuri kabisa na huku akigusia ulazima wa kufuatiliwa masuala yaliyozungumzwa na wanachuo kwenye mkutano huo amesema, mitazamo tofauti na ya aina kwa aina iliyotolewa na wanachuo katika mkutano huo ni mazuri na ni jambo la kuvutia na kufurahisha sana kuona wamejitahidi kubainisha fikra zilizodurusiwa vyema na zenye ushahidi makini.

Amesema, hotuba makini sana zilizotolewa na wawakilishi wa jumuiya na vyama vya wanachuo zinaonyesha kuwa kuna nafasi kubwa ya kuwa na fikra zinazofanana kati ya jumuiya na vyama hivyo na kwamba hotuba zilizotolewa kwenye mkutano huo zinaonyesha upana wa mawazo, kuangalia mbali kwa mtazamo wa kina na kufikia kwenye uhakika.

Ayatullah Udhma Khamenei vile vile ametoa majibu chanya na ameunga mkono maneno ya mmoja wa wanachuo waliotoa hotuba zao kwenye mkutano huo kuhusu udharura wa kuulizwa maswali na kutolewa mitazamo na ukosoaji kutoka kwa wanachuo na kuongeza kuwa, tabaka la wanachuo ni tabaka bora kabisa nchini na viongozi mbali mbali wanapaswa wakae pamoja na wanachuo na kujibu maswali ya tabaka hilo la wasomi ambalo lina mitazamo ya mbali mbali ya kujenga na welewa mpana.

Amesema kuna tofauti kati ya upinzani na kuuliza maswali na kukosoa mambo na amekumbusha kuwa, harakati ya wanachuo haipaswi kudhani kuwa iko hapo kwa ajili ya kupinga tu vyombo mbali mbali nchini na wala isifikiri kuwa kupinga ni sehemu ya majukumu yake bali lililo muhimu kwa harakati hiyo ni kuuliza maswali na kuhakikisha inapatiwa majibu yanayotakiwa na viongozi husika.

Mmoja wa wanachuo alisema katika hotuba yake kuwa, hivi sasa baadhi ya watu wanaamini kwamba inabidi suala la umoja na mshikamano lifanywe kuwa ndiyo asili ya mambo yote, lakini wengine wanaamini kuwa inabidi watu wasio wasafi watolewe katika Mapinduzi kwa kuzingatia mazingira yanavyoruhusu.

Akijibu matamshi hayo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameunga mkono masuala yote mawili ya umuhimu wa kuweko umoja na ikhlasi hata hivyo ameongeza kuwa, kuitakasa jamii hakupatikani kwa mashinikizo na kwa harakati kali na kwamba dini tukufu ya Kiislamu nayo haikumwamrisha mtu yeyote kuwafukuza na kuwatenga watu walio dhaifu kiimani kwa kisingizio cha kuitakasa jamii.

Amesema, kutia nguvu ikhlasi katika nyoyo za watu binafsi, katika familia, makundi na jamii ndiyo njia sahihi ya kuitakasa jamii na kuongeza kuwa, inabidi wigo wa watu wenye ikhlasi upanuliwe kadiri inavyowezekana. Amesema lengo hilo litaweza kupatikana pale tu kila mtu atakapozidi kujipamba kwa sifa ya ikhlasi kuanzia yeye mwenyewe, familia yake, marafiki na wenzake katika masuala ya kisiasa na kijamii.

Ayatullah Udhma Khamenei vile vile amezungumzia lengo na makusudio yake kuhusu umoja ni kushikamana ndani ya misingi na mambo ya asili na kukumbusha kuwa, ni kwa msingi wa kiwango cha kushikamana na kukubaliana kwake mtu na misingi na mambo ya asili ndivyo tunavyoweza kuungana na kushikamana naye na kwamba kila mtu ambaye haikubali misingi iliyopo, bila ya shaka yoyote atatoka kwenye wigo huo wa umoja.

Ayatullah Udhma Khamenei aidha amesema katika kujibu swali la mwanachuo mmoja katika upande wa misimamo rasmi na isiyo rasmi ya Kiongozi Muadhamu kuwa, Mwenyezi Mungu apishie mbali mtu kudhani kuwa Kiongozi Muadhamu anaamini na ana misimamo tofauti na ile ambayo anaitoa rasmi na ambayo hawaelezi watu wote isipokuwa watu maalumu tu kwani mtazamo huo ni ghalati na ni makosa kikamilifu na kama mtu atakuwa na fikra hiyo basi atakuwa anafanya madhambi makubwa.

Ameongeza kuwa, mitazamo na misimamo yake yote anaitoa hadharani kwani anaamini kidhati kwamba si sawa na si busara kwa Kiongozi kuwa na misimamo tofauti na ile anayoitangaza hadharani.

Akijibu swali la mwanachuo mwengine, Ayatullah Udhma Khamenei amewataka walichukulie suala la kuulinda Mfumo wa Kiislamu kuwa ni mambo ya wajibu kabisa. Ameongeza kuwa, maana ya kuulinda mfumo ni kulinda mipaka yake tofauti ikiwemo mipaka ya kiutamaduni na kimaadili.

Vile vile amesema kuhusu ukosoaji wa mmoja wa wanachuo kuwa hadi sasa hakuna uzalishaji wa bidhaa za kiutamaduni zinazokubaliana na uadilifu na matukufu mengine ya Kiislamu kwamba, ukosoaji huo ni wa mahala pake na amewataka wahusika wa masuala ya kiutamaduni likiwemo Shirika la Utangazaji la Sauti na Televisheni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB, Shirika la Tablighi ya Kiislamu na kitengo cha sanaa nchini kufanya kazi zaidi katika upande huo.

Ayatullah Udhma Khamenei aidha amesema kuhusu suala hilo la uzalishaji wa bidhaa za kiutamaduni kuwa, kazi hiyo inachukua muda na inahitajia miundombinu tofauti na kuongeza kwamba, inasikitisha kuona kuwa katika kipindi chote hiki miundombinu hiyo haijaandaliwa bali hata wakati wa baadhi ya serikali nchini, miundombinu ya kazi hizo za kiitikadi na kiutamaduni zilidhoofishwa na kuharibiwa.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha ameunga mkono matamshi ya mwanachuo mwingine kuhusu kutengana nyanja za kiutamaduni na kiafya katika kifungu cha 44 cha Katiba na kuingizwa katika masuala ya ubinafsishaji na kuongeza kuwa, tatizo hilo inabidi lizingatiwe na kufuatiliwa.

Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria juu ya matamshi ya viongozi mbali mbali kuhusu utekelezaji mzuri wa kifungu cha 44 cha Katiba na baadhi ya mitazamo mingine inayotofautiana na kuwausia wanachuo kwamba wafuatilie maswali na mambo wanayoyaona tata kupitia kwenye vyama na jumuiya zao za wanachuo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, uwepo wa wanachuo katika jumuiya za wananchi na za wanachuo wa nchi nyinginezo kwa ajili ya kufikisha fikra na ujumbe safi na sahihi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni jambo zuri na kusisitiza kuwa, ni jambo lililo wazi kwamba kazi nyingi zinafanyika katika uwanja wa kuimarisha mawasiliano na mataifa mengine lakini pamoja na hayo ni jambo zuri kushiriki wanachuo wa Iran katika nyanja hizo wakiwa na mipango iliyodurusiwa na kufikiriwa vyema.

Hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mkutano huo uliojaa mapenzi, urafiki na udugu imegusia pia suala la kutoka watu wenye vipawa nchini.

Amesema kuhusu suala hilo kwamba, inawezekana kuna baadhi ya mambo ya ndani ya nchi yanapelekea kushuhudiwa hali hiyo lakini jambo kubwa linapelekea watu hao wenye vipaji kutoka nchini na kwenda kwenye nchi nyingine ni ahadi wanazopata kutoka nje ya nchi ambapo baadhi ya ahadi hizo hata zinatokana na upinzani wa mikono hiyo ya nje dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amesema, masuala ya kidini na kiimani nayo kwa upande wake yanapelekea watu wenye vipaji kurejea nchini Iran na ameongeza kuwa, baadhi ya watu wenye vipawa, watu wakubwa na muhimu katika jamii wanarejea nchini kutokana na masuala hayo ya kidini na kiimani.

Ayatullah Udhma Khamenei amegusia pia matamshi ya mwanachuo mwingine kuhusu udharura wa kufuatiliwa sisitizo la Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusiana na uvamizi wa mabweni ya Chuo Kikuu mjini Tehran na kuongeza kuwa ufuatiliaji huo ulikuwa wa kusuasua na haukufanyika kwa namna iliyotakiwa lakini suala hilo halijasahaulika na Inshaallah litazidi kufuatiliwa.

Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia juu ya maneno yaliyokuwemo kwenye hotuba ya mwanachuo mwingine aliyekosoa utendaji wa baadhi ya watu serikalini na baadhi ya watu wanaomzunguka Rais na kusema, hawezi kutoa uamuzi wala kumhukumu mtu katika suala hilo. Amesema inawezekana kuna tatizo na yumkini ukosoaji uliotolewa ni wa mahala pake, lakini inabidi mambo kuyagawanya kati ya yale ya asili na makuu na yale madogo madogo. Amesema inabidi kuwa macho na kutofanya masuala madogo madogo ambayo ni ya daraja la pili, yachukue nafasi ya masuala muhimu na ya asili.

Ayatullah Udhma Khamenei amewalaumu baadhi ya viongozi wanaotangaza hitilafu hadharani na kuongeza kuwa, kumetolewa onyo kali kuhusu suala hilo.

Vile vile amezungumzia matamshi ya mmoja wa wanafunzi kuhusiana na mkusanyiko wa wanachuo hivi karibuni mbele ya Bunge kupinga muswada uliohusiana na Chuo Kikuu cha Azadi na amesema hawezi kulitolea msimamo suala hilo isipokuwa anapenda kusema tu kuwa baadhi ya nara na kaulimbiu zilizotolewa katika mkusanyiko huo hazikuwa mbaya lakini zilikuweko nyingine kali ambazo inabidi wanachuo hao wakubali kukosolewa.

Mwishoni mwa hotuba yake kuhusu hotuba za wanachuo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezitaka jumuiya za wanachuo kuhakikisha haziathiriwi na hitilafu za mitazamo ya wanasiasa na ameongeza kuwa, kila mwanachuo na kila jumuiya ina mitazamo yake, lakini tofauti za mitazamo hazipaswi kuachiliwa kuzusha mifarakano na mizozo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, ni jambo la wajibu kwa jumuiya za wanachuo kuwa na uchanganuzi makini na wa hali ya juu kuhusu masuala muhimu ya nchi. Ameongeza kuwa, wanachuo wanapaswa kutangaza misimamo yao katika masuala muhimu yanayohusu nchi kama vile Taarifa ya Tehran (kuhusiana na kubadilishana fueli nyuklia), azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuhusu vikwazo vya upande mmoja vya Marekani na Ulaya.

Vile vile amesema miundombinu inayohitajika iko katika maandalizi kwa ajili ya kuleta mapinduzi makubwa ya kimaendeleo nchini na kwamba katika upande wa kimaanawi pia kuongezeka fikra za kupigania uadilifu na kutotosheka na maendeleo ya kimaada kunaongeza matumaini kati ya wananchi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema, harakati za kambi ya maadui wa taifa la Iran inazidi kuporomoka na katika upande mwingine harakati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inazidi kupanda na kunawiri. Amesisitiza kuwa, licha ya kuweko njama nyingi za maadui lakini taifa la Iran linaendelea kupiga hatua kwa miaka 32 sasa na Inshaallah kwa kutegemea imani, azma na nia ya kweli, taifa hili litazidi kupiga hatua katika njia yake iliyojaa fakhari.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei amewausia vijana kujua thamani ya kipindi cha ujana na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu kadiri inavyowezekana Ambaye ni chimbuko la uhakika na ujamali. Ameongeza kuwa, kuilea nafsi na kulinda usafi wa roho wakati wa ujana ni jambo rahisi zaidi kuliko katika kipindi cha uzeeni na cha kukaribia kuzeeka.

Amesema, hatua muhimu zaidi katika kuilea nafsi ni kuacha maasi na amekumbusha kuwa, baada ya kuacha maasi, sala ni ibada nyingine muhimu katika uwanja wa kuilea nafsi hususan ile sala inayosaliwa mwanzoni mwa wakati na kuhudhurishwa moyo kikamilifu katika ibada hiyo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, kuwa na mapenzi makubwa na Qur'ani na dua hususan zilizomo ndani ya kitabu cha dua cha Sahifatus Sajjadiyyah na kutilia umuhimu ibada za suna kama njia nyingine bora za kuilea nafsi.

Ameongeza kuwa, jambo kubwa linalopelekea kutetereka nafsi za baadhi ya watu katika nyuga mbali mbali za maisha ya mtu binafsi na ya kijamii ni madhambi yanayotendwa na watu hao, hivyo kufanya mazoezi na kuwa na istikama katika kuacha maasi wakati wa ujana, ni jambo muhimu mno katika kujilinda mtu asipotoke katika misukosuko mingi ya maisha.

Mwishoni mwa mkutano huo hadhirina wamesali sala za Magharibi na Isha zilizosalishwa na Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei na baada ya hapo wamekula futari waliyoandaliwa na mwenyeji wao, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
639774
captcha