IQNA

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu aonana na mamia ya wahadhiri wa vyuo vikuu

11:47 - September 07, 2010
Habari ID: 1989144
Chuo Kikuu ni injini ya maendeleo ya nchi na kama taifa linataka kuwa na heshima, istiklali, uhuru, nguvu na utajiri, basi halina budi kuimarisha vyuo vikuu vyake.
Hayo ndiyo mambo makuu yaliyokuwemo kwenye hotuba ya Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran aliyoitoa Jumapili, Septemba 5, 2010, mbele ya mamia ya wahadhiri wa vyuo vikuu na vituo vya elimu ya juu nchini.
Mwanzoni mwa mkutano huo uliochukua masaa matatu, wahadhiri 14 wametumia masaa mawili kutoa mapendekezo na mitazamo yao kuhusu masuala tofauti ya kielimu, kiutamaduni, kijamii, kiuchumi na kisiasa.
Miongoni mwa nukta zilizozungumziwa na wasomi hao ni pamoja na:
- Umuhimu wa kuzingatiwa kikamilifu jamii ya watu wanaojishughulisha na masuala ya elimu nchini ikiwa ni kama ramani ya njia ya kuibadilisha Iran kuwa marejeo ya kielimu duniani.
- Kuimarishwa mashirika yanayojishughulisha na masuala ya kielimu ili kujitoa katika uchumi unaotegemea mafuta.
- Kuwa tayari wahadhiri na watafiti kushiriki vilivyo katika kutatua tatizo lolote lile na upungufu wowote unaoweza kujitokeza kutokana na vikwazo.
- Kufufuliwa tiba ya jadi ikiwa ni sehemu ya njia za kimantiki za kuvirithisha vizazi vichanga utajiri wa kihistoria wa Iran.
- Kutiliwa mkazo zaidi elimu ya humaniora yaani Sayansi ya Jamii (humanities) ukiwa ni kama msingi wa maendeleo na ustawi wa kweli wa nchi.
- Udharura wa kuanzishwa harakati mpya ya kiakili na kifikra katika Vyuo Vikuu na Vituo vya Elimu ya Juu.
- Kustawi na kupiga hatua kubwa Iran katika masuala mbalimbali ya afya na matibabu kwa mujibu wa viwango vya kimataifa.
- Umuhimu wa kufanyika juhudi kubwa zaidi katika suala zima la kulea nguvu kazi ya wataalamu katika uga wa sayansi ya uchumi wa Kiislamu.
- Umuhimu wa kuanzishwa muundo mpya na usimamiaji wenye mlingano unaotakiwa katika upande wa sayansi na teknolojia.
- Suala la mashirika ya kibepari ya nchi za Magharibi yanayodhibiti kazi na maendeleo ya tiba duniani, n.k.
Baada ya wahadhiri hao 14 wa vyuo vikuu na vituo vya elimu ya juu kutoa hotuba zao, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameanza kuhutubia hadhirina akiashiria umuhimu mkubwa wa vyuo vikuu katika suala zima la kuiletea Iran heshima na kuipa nguvu. Amesisitiza kuwa, Iran inahitajia jihadi ya kielimu katika nyanja na nyuga zote na kwamba yeye analifuatilia kwa kina, kwa wasiwasi, kwa hamu na kwa matumaini suala hilo lenye muhimu mkubwa.
Vilevile ameashiria vizuizi na vizingiti vilivyopo katika njia ya maendeleo ya kielimu ya Iran na kuongeza kuwa, katika utamaduni wa Kiislamu, neno jihadi linapata maana yake halisi katika uga wa kufanya juhudi za kupambana na vizuizi na vizingiti vilivyopo na kwamba kwa kuzingatia mtazamo huo wa Kiislamu, Iran hivi sasa inahitajia kikweli kweli kuwa na jihadi ya kielimu.
Ayatullah Ali Khamenei amebainisha kuwa, kupenda kuhodhi kila kitu na uchoyo wa nchi zilizoendelea kisayansi katika suala zima la elimu na suhula za kielimu ni miongoni mwa vizuizi vilivyopo katika njia ya ustawi wa kielimu nchini na kusisitiza kuwa, inabidi taifa la Iran lipambane vilivyo na kuvishinda vizuizi hivyo vyote kwa kutumia vipaji vyake vya ndani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbusha kuwa sifa ya taifa la Iran ya kuwa na historia ndefu ya fakhari za kielimu na kiutamaduni pamoja na vipaji na akili ya aina yake waliyo nayo Wairani katika nyanja mbali mbali ni fursa nzuri ya kuliwezesha taifa hili kufikia vilele vya juu vya elimu. Ameongeza kuwa, Mapinduzi ya Kiislamu nayo yameliongezea taifa hili sifa muhimu sana ya kuweza kupiga hatua kubwa za maendeleo ya kielimu kutokana na mapinduzi hayo kulizawadia taifa hili mwamko na kulipa nguvu za kujiamini na kujifanyia lenyewe mambo yake.
Amesema maendeleo ya kupigiwa mfano ya Iran katika nyuga tofauti za sayansi na teknolojia ni ushahidi wa uwezo walio nao wananchi wa Iran katika kupiga hatua kubwa za kimaendeleo na ameongeza kuwa, maendeleo yote yaliyopatikana nchini Iran katika kipindi cha miaka 30 iliyopita inabidi yahesabiwe kuwa ni hatua za awali tu za kunawiri kielimu Iran na inabidi wananchi wa Iran wawe na fikra za kiistratijia za kuwawezesha kupiga hatua kubwa zaidi za kimaendeleo.
Ayatullah Udhma Khamenei pia amesema hotuba zilizotolewa na wahadhiri wa Vyuo Vikuu katika mkutano huo zinafurahisha sana, zilikuwa na mada aina kwa aina, zilisheheni nukta muhimu na zilijaa mapendekezo yanayotekelezeka. Ameongeza kuwa, fikra mpya iliyotolewa kwenye mkutano huo kuhusiana na Chuo Kikuu cha "Misingi ya Hekima," pendekezo la kuundwa kituo cha kisasa cha uchunguzi wa ramani kuu ya kielimu nchini na sisitizo juu ya umuhimu wa somo ya humaniora (Sayansi ya Jamii) katika pande zake tofauti ni miongoni mwa nukta nyingine muhimu zilizotiliwa mkazo na wasomi hao wapendwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema, mapungufu yaliyozungumziwa na mmoja wa wahadhiri kuhusiana na kuzeeka na kutobadilishwa mtaala wa somo la Sayansi ya Jamii yapo na ni sahihi na amesisitizaa kuwa, nuksani hiyo inaonyesha kuwa hakuna uthubutu unaotakiwa wa kuingia kwenye mijadala ya kifikra na demokrasia ya kiliberali ya Magharibi.
Amesema, kutolewa majibu ya kukinaisha na yenye ushahidi wa Kiislamu kuhusu masuala yanayohusiana na somo la humaniora ni njia sahihi ya kujadiliana na Sayansi ya Kijamii ya Magharibi na ameongeza kuwa, wahadhiri wa Hawza na Vyuo Vikuu wanapaswa kujitokeza kishujaa katika medani hiyo na watekeleze majukumu yao ya kutunga na kutoa majibu ya kweli na ya kukinaisha kuhusiana na masuala hayo kama yanayofundishwa na dini tukufu ya Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amegusia pendekezo lililotolewa na mwalimu mmoja wa kike wa Chuo Kikuu kwenye mkutano huo kuhusiana na udharura wa kuweko mawasiliano makubwa zaidi kati ya Kiongozi Muadhamu na jamii ya akinamama nchini na kuongeza kuwa, wanawake wa Iran wanaunda nusu ya watu wote nchini na ni wazi kwamba hawawezi kufananishwa na taasisi au majimui moja tu kama ilivyokuja kwenye pendekezo hilo lakini pamoja na hayo asili ya pendekezo hilo ni sahihi na inabidi kupendekezwe njia na mikakati bora zaidi ya kuweza kumfikia vizuri zaidi taarifa na fikra za wanawake wasomi nchini.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia pia matamshi ya mhadhiri mwingine wa Chuo Kikuu kuhusiana na maendeleo makubwa na ya kujivunia ya Iran katika uwanja wa afya na tiba na kusisitiza kuwa, maendeleo yaliyopatikana nchini katika nyanja nyinginezo nayo pia ni makubwa sana lakini pamoja na hayo kuna baadhi ya watu hawachoki kuimba wimbo wa kukatisha tamaa katika pembe hii na ile na daima utawaona wanajaribu kuwavunja moyo wananchi, wanachuo na watu wa Vyuo Vikuu nchini.
Amesema, watu wa namna hiyo ni sawa na mchwa waharibifu na waangamizaji. Ameongeza kuwa, ni jambo lililo wazi kwamba harakati adhimu ya taifa la Iran kama zilivyo harakati zote za kijamii na kihistoria inakabiliwa na changamoto mbali mbali lakini mmea wa Mapinduzi ya Kiislamu leo umekuwa ni mti mwema na kwamba Iran hivi sasa inazidi kustawi na kunawiri kwa namna ya kipekee.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile amesema kuwa, suala la kuzalisha fikra ni jambo muhimu sana na amesisitiza kuwa, Iran ni kitovu cha falsafa na walimu wa Hawza na Vyuo Vikuu wanapaswa kufanya juhudi za kuzalisha fikra ambazo chimbuko lake litakuwa ni mitazamo ya kifalsafa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia juu ya hatua za mwisho ilizofikia ramani kuu ya elimu nchini na kusisitiza kwamba, ramani hiyo inahitaji kuwa na ratiba za utekelezaji na amewataka wahusika wa vyombo vinavyoshughulikia suala hilo watunge ratiba makini na za kina za kuweza kutekeleza ipasavyo ramani hiyo.
Aidha amesema ni jambo la dharura kwa vituo vyote vya kielimu na utafiti kuheshimu ramani hiyo kuu ya elimu nchini na kuongeza kuwa, wakati ramani kuu ya elimu inapokuwa hai, safi na ya kisasa, inahitajia kuwa na mipango makini ya kuitekeleza.
Vile vile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbusha kuwa, kama hakutakuwa na malengo maalumu katika ukuzaji wa elimu ya juu basi bila ya shaka jambo hilo litapelekea kufuja mali tu na nguvukazi na halitaleta matunda yaliyokusudiwa. Ameongeza kuwa, inabidi yachunguzwe na yawekwe wazi mahitaji makuu ya nchi katika nyanja mbali mbali za elimu na teknolojia ili kwa njia hiyo viweze vyuo vikuu na waweze wanachuo kuchagua masomo yanayohitajiwa na nchi. Amesema Wizara ya Sayansi na Elimu ya Juu nchini nayo inapaswa kuzingatia misingi hiyo katika kustawisha na kuendeleza elimu ya juu nchini.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei amegusia siku za mwisho za mwezi huu mtukufu wa Ramadhani na kusisitizia umuhimu wa kutumia vizuri zaidi anga iliyopo ya upole, huruma, rehema, nyofu na iliyojaa nuru kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ameongeza kuwa, kuitoharisha na kuisafisha nafsi kuna faida kwa watu wote lakini kwa upande wa wasomi na wahadhiri jambo hilo linakuwa na faidi na manufaa makubwa zaidi kwani mwenendo na huluka ya mwalimu wa chuo kikuu ina athari kubwa za moja kwa moja katika uundikaji wa shakhsia ya wanachuo vijana.
Amesema faida nyingine ya kujitoharisha kinafsi mhadhiri na mwalimu wa chuo kikuu ni kupata uwezo wa kuainisha harakati ya kielimu kwa njia iliyo sahihi.
Mwishoni mwa mkutano huo, hadhirina wamesali sala za Magharibi na Isha zilizosalishwa na Kiongozi Muadhamu na baadaye wamekula futari pamoja na mwenyeji wao Ayatullah Ali Khamenei.
649601
captcha