IQNA

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu: Makundi ya Kizayuni ndiyo yaliyopanga jinai ya kuvunjiwa heshima Qur’ani nchini Marekani

7:54 - September 14, 2010
Habari ID: 1993211
Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, jana Jumatatu, alitoa ujumbe muhimu sana kwa taifa la Iran na kwa umma mkubwa wa Kiislamu duniani kufuatia kuvunjiwa heshima Kitabu Kitakatifu cha Qur'ani nchini Marekani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, makundi ya Kizayuni ndani ya serikali ya Marekani ndio wapangaji wakuu wa njama hiyo inayochefua moyo. Vile vile amesema, kama madai ya viongozi wa Marekani kuhusiana na kutohusika kwao na jinai hiyo yana ukweli, basi wawachukulie hatua kali waliofanya jinai hiyo. Vile vile amesema, kitendo cha kipunguwani na cha kuchefua moyo cha kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika nchi ya Marekani tena chini ya ulinzi wa polisi wa nchi hiyo, ni tukio chungu na kubwa ambalo si sahihi kudhania kuwa linahusiana tu na harakati ya kijinga ya mamluki na vitimbakwiri visivyo na thamani yoyote, bali hilo ni jambo lililopangiliwa vyema na vituo maalumu ambavyo kwa miaka mingi sasa ajenda yao kuu ni kueneza chuki dhidi ya Uislamu. Amesema mnyororo mchafu wa jinai za vyombo hivyo ulianza kwa usaliti wa murtadi Salman Rushdi ukaendelezwa na mchora vikatuni khabithi wa Denmark na makumi ya filamu zilizo dhidi ya Uislamu za Hollywood na hadi kufikia sasa ambapo tumeshuhudia tamthilia mbaya na ya kukasirisha mno huko Marekani. Ayatullahil Udhma Khamenei amesema pia kuwa, wapangaji na waendeshaji wakuu wa jinai hizo dhidi ya Uislamu ni viongozi wa mfumo wa kibeberu na wale wanaobuni siasa za Kizayuni ambao wana ushawishi mkubwa ndani ya serikali ya Marekani na katika mashirika ya usalama na kijeshi ya Marekani na vile vile katika ya serikali ya Uingereza na kwene baadhi ya serikali za nchi za Ulaya. Amesema, hao ndio wale watu ambao kila kukicha wananyooshewa kidole cha tuhuma na makundi huru yanayotafuta ukweli kuhusiana na matukio ya Septemba 11 ya nchini Marekani. Amesema, silisila hii ya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu inatokana na uhakika kwamba tangu miongo ya huko nyuma hadi hivi sasa, nuru ya Uislamu imekuwa iking'ara zaidi na imezidi kupenya katika nyoyo za watu kwenye ulimwengu wa Kiislamu na hata katika nchi za Magharibi. Aidha amesema, inabidi watu wazingatie kwamba tukio la hivi karibu la kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini Marekani halina mfungamano na Kanisa na wala na Wakristo bali ni kitendo kilichofanywa na baadhi chache na makasisi wajinga, wanasesere na mamluki hivyo haipasi kuwahusisha Wakristo wote na tukio hilo. Amesisitiza pia kuwa sisi Waislamu kamwe hatuwezi kulipiza kisasi kwa kuvunjia heshima matukufu ya dini nyinginezo. Ametahadharisha kuwa, maadui ndio wanaotaka kuzuke ugomvi kati ya jamii za Waislamu na Wakristo na hilo ndilo lengo lao katika kupanga na kuendesha tamthilia hiyo ya kiwendawazimu na kipunguwani huko Marekani. Vile vile amewataka Waislamu wawe waangalafu sana mbele ya uchokozi na jinai kama hizi za mabeberu na wasiruhusu ziwafanye wasahau masuala yao ya ulimwengu wa Kiislamu na hasa ya Mashariki ya Kati.
654197
captcha