Abdul Nabii al Attar amechapisha kwanza fatuwa ya Ayatullah Khamenei na kuandika kuwa misimamo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran daima imekuwa ikibatilisha njama za maadui wa umma wa Kiislamu wanaofanya jitihada za kuzusha hitilafu na mifarakano katika safu za Waislamu.
Makala ya mhariri wa gazeti la al Qabas la Kuwait imepongeza misimamo ya Ayatulla Ali khamenei ya kusisitiza daima juu ya umoja na mshikamano wa Kiislamu na kusema: “Si ajabu kwa maulama wakubwa wa Kishia kama Ayatullahil Udhmaa Ali Khamenei kuwa na misimamo kama hiyo kwani mwenendo huo ndio sira ya Ahlul Bait (as).
Wakati huo huo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maulama wa Kisuni mwa Iraq Sheikh Khalid al Mulla amepongeza fatuwa ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na ametoa wito wa kuitishwa mkutano wa maulama na wanafikra wa Kiislamu kwa ajili ya kukabiliana na fitina na njama zinazokusudia kuzusha fitina na hitilafu kati ya Waislamu.
Siku chache zilizopita Ayatullahil Udhmaa Ali Khamenei alitoa fatuwa inayoharamisha kumkosea heshima Bibi Aisha, mke wa Mtume wetu Mtukufu Muhammad (saw) na shakhsia wengine wa Kiislamu wanaoheshimiwa na Waislamu wa madhehebu ya Suni. Fatuwa hiyo imetolewa baada ya msoni wa Kishia wa Kuwait Yasir al Habib kumkosea adabu Bibi Aisha. 669736