IQNA

Ayatullah Khamenei:

Vyuo vya kidini vinapaswa kuwa macho ili visipige hata hatua moja katika njia ya adui

17:16 - October 25, 2010
Habari ID: 2019578
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei Jumapili usiku alikutana na wahadhiri na wanafunzi hodari wa vyuo vya kidini vya Qum (hauza) akiitaja elimu kuwa ndio utambulisho halisi wa vyuo hivyo.
Amebainisha nukta muhimu kuhusu udharura wa hauza kuwa tayari kupokea maswali na tashwishi zinazowakabili watu, kuwa huru katika kutafakari, kutodumaa kifikra, kujiamini kielimu, kutegemea mbinu za kimantiki na kiakili katika kukabiliana na mitazamo ya upande mwingine, haja ya hauza kwa nyanja mbalimbali za elimu, mfumo wa kimaadili na kimalezi wa hauza na udharura wa kumtambua adui.
Katika mkutano huo ambao uliendelea kwa kipindi cha masaa manne, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliitaja elimu kuwa ndio msingi mkuu wa vyuo vya kidini. Amesema kuwa msingi wa hauza umesimama juu ya nguzo za elimu na kwa msingi huo hauza inapaswa kufungamana na athari za elimu.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa kukaribisha maswali na shaka za kielimu ni katika maswala ya kielimu na kuongeza kuwa elimu inazusha maswali na vituo vya elimu ikiwemo hauza, vinapaswa kufungua milango ya kupokea maswali na shaka za watu.
Ameashiria ushindani mkali wa kielimu uliokuwepo katika kipindi chote cha historia ya vyuo vya kidini na akasema kuwa ada hiyo yenye thamani kubwa inapaswa kuimarishwa katika nyanja mbalimbali za taaluma za vyuo vya kidini.
Amesema kuwa kukata na kuzuia maswali kutapelekea kukatika na kusimama elimu na maarifa. Amesisitiza kuwa kutoa maswali na kueleza majibu kwa kutumia mbinu za kisasa hakuna mushkeli wowote na hata kama yanayoulizwa si sahihi lakini yanapaswa kujibiwa kwa kutumia mbinu za kielimu na kisayansi.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa uhuru wa kutafakati ni miongoni mwa ada zilizoenea katika vyuo vya kidini na amesisitiza juu ya kuimarishwa zaidi ada hiyo njema. Amesema uhuru wa kutafakari ni miongoni mwa sifa za elimu, na kudumaa na ukosefu wa harakati za kutafakari hakuna maana katika medani ya elimu.
Ayatullah Khamenei ameashiria baadhi ya mitazamo inayotoa madai ya kutokuwepo anga huru na ukosoaji katika vyuo vya kidini na akasema, hiyo ni tuhuma kubwa. Ameongeza kuwa uhuru wa kutafakari katika hauza na vyuo vya kidini ni mkubwa zaidi kwa sasa kuliko hata ilivyokuwa huko nyuma lakini uhuru huo unapaswa kupanuliwa na kuimarishwa katika nyanja mbalimbali na wanafikra wanapaswa kutoa maoni na fikra zao kwa uhuru katika nyanja zote za elimu.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa hali ya kujiamini kielimu ni miongoni mwa sifa za kubakisha hai utambulisho wa elimu katika vyuo vya kidini. Amesema kuwa katika kipindi hiki cha mgongano wa fikra na mitazamo mbalimbali, elimu inapaswa kuwa na thamani kubwa zaidi katika hauza na vyuo vya kidini. Ameongeza kuwa japokuwa takwa, kuipa mgongo dunia na unyenyekevu (khushui) vina thamani ya juu zaidi lakini elimu inaweza kupimwa na kwa msingi huo mtu mwenye elimu kubwa zaidi anapaswa kuwa na thamani kubwa zaidi katika vyuo vikuu.
Kuhusu maadili na akhlaki ya kivitendo katika hauza na vyuo vya kidini, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza juu ya udharura wa kuwepo insafu katika medani ya elimu na bidii katika kazi za kielimu. Amesema kuwa wahadhiri wa hauza wanapaswa kuzalisha fikra mpya kwa kufanya utafiti na kutaamali ili hauza isikumbwe na matatizo ya mfumo mpya wa elimu.
Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa kudumisha mawasiliano makubwa na jamii ya elimu kitaifa na kimataifa ni miongoni mwa mambo mengine ya dharura kwa ajili ya kulinda muundo wa kielimu wa vyuo vya kidini. Amesema hauza ya Qum inapaswa kuwa na uhusiano madhubuti wa kielimu na vyuo vikuu na vyuo vingine vya kidini hapa nchini na katika ulimwengu wa Kiislamu. Amesisitiza kuwa utumiaji wa vyombo vya kisasa vya mawasiliano ya umma unaweza kusahilisha na kuharakisha mawasiliano hayo.
Ameutaja upinzani dhidi ya ukandamizaji wa fikra na mitazamo tofauti kuwa ni miongoni mwa ada nzuri za hauza na vyuo vya kidini. Amesisitiza juu ya kujiepusha na mbinu zisizokuwa za kielimu katika kujibu mitazamo ya upande mwingine. Amesema kuwa hoja za kiakili ndio msingi wa mbinu za kielimu za hauza, na kuwakufurisha watu wengine ni mbinu isiyokuwa ya kielimu. Amewashauri wanazuoni na wanafunzi wa vyuo vya kidini kukabiliana na fikra zisizokuwa sahihi kwa kutumia hoja madhubuti.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa elimu sambamba na kutafakari na kufanya uhakiki ni mingoni mwa sifa za kielimu za hauza na vyuo vikuu vya kidini. Ameongeza kuwa wahadhiri wa vyuo vya kidini wanapaswa kuwalea wanafunzi kwa kuwafundisha mbinu za kutafakari, kufanya utafiti na uchunguzi.
Ameashiria pia udharura wa kupewa umuhimu suala la utafiti katika vyuo vya kidini na kukumbusha haja ya hauza kwa nyanja mbalimbali za taaluma ikiwa ni pamoja na falsafa. Amesema kuwa elimu ya fiqhi ndio uti wa mgongo wa hauza lakini vyuo vikuu vya kidini vinapaswa kulea na kutayarisha wataalamu katika nyanja nyingine za elimu kama tafsiri ya Qur'ani, mbinu za ulinganiaji na sayansi za jamii.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza juu ya udharura wa kutumiwa mbinu za kisasa katika kufunza na kuzalisha elimu. Vilevile ameashiria umuhimu wa mfumo wa akhlaki na malezi na akasema kuwa hauza na vyuo vya kidini vinapaswa kuwa na harakati na mahudhurio makubwa nje ya vyuo vya kidini hususan katika taasisi kubwa na yenye taathira ya elimu na malezi.
Amesema kuwa ili kufikia lengo hilo kunahitajika wataalamu wa masuala ya elimu, malezi na maadili na amewausia viongozi wa vyuo vya kidini kutilia maanani suala hilo.
Ayatullah Khamenei amezungumzia pia suala la kujitokeza nyanja na zana mpya na zenye taathira kubwa katika fikra za watu ndani na nje ya nchi na akasema kuwa uwezekano wa kujitokeza fikra na tashwishi za aina mbalimbali unaifanya kazi ya hauza na vyuo vya kidini kuwa nzito zaidi na kuzidisha udharura wa hauza kutilia maanani nyanja mpya na mbalimbali za taaluma.
Amehimiza pia ulazima wa kuvutia watu wenye vipawa na hamu kubwa ya kusoma katika vyuo vya kidini. Ayatullah Khamenei ameashiria hatua nzuri na muhimu zilizochukuliwa katika hauza na akasema kuwa uongozi imara, unaokubalika na kuungwa mkono na marja na viongozi wa ngazi za juu wa dini umekuwa na taathira katika kufanikisha hatua hizo.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza juu ya udharura wa kujiepusha na hatua yoyote ya kudhoofisha uongozi wa hauza na akasema watu wote wanapaswa kuwa na tahadhari ili wasidhoofishe taasisi kubwa na zenye historia ya muda mrefu kama Jumuiya ya Wahadhiri wa Vyuo vya Kidini.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia pia uadui wa ubeberu hususan Marekani na Wazayuni dhidi ya kazi ya kulingania na kuimarisha hisia za kufuata mafundisho ya dini na akasema kuwa njama na hatua mbalimbali kama uchoraji vibonzo na katuni zinazovunjia heshima matukufu ya Kiislamu, kuchomwa moto Qur'ani na hatua nyingine za kanali ya kimataifa ya Uzayuni, zinadhihirisha uhabithi na uovu wa maadui wa Uislamu na hatutupaswi kupuuza mambo hayo.
Ayatullah Khamenei amesisitiza juu ya udharura wa kumtambua adui na kujiepusha kikamilifu kupita katika njia yake. Amesema kuwa wananchi wote wakiwemo watu wa vyuo vya kidini, wanapaswa kuwa macho daima na wasisema hata neno moja au kupiga hatua ndogo katika njia ya adui.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa masuala ya kiroho, kutawasali, kuomba, takwa na ucha-Mungu na kutojishughulisha na masuala ya dunia ndio msingi wa kazi za hauza. Amesema kuwa iwapo mambo yote ya kielimu na kifikra yatafanyika bila ya kutawaliwa na masuala ya kiroho na akhlaki, kazi haziwezi kwenda mbele kwa njia sahihi.
Ayatullah Khamenei amekumbusha sira na mwenendo wa walimu na maulama wakubwa wa hauza akiwemo Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu katika kuwanasihi wanafunzi na kuwalingania kivitendo maadili mema na masuala ya kiroho. Amesema kuwa moyo wa vijana ni uwanja mzuri wa kukubali nasaha na kupiga hatua katika upande wa daraja za juu za kiroho na uwanja huo mzuri unapaswa kutumiwa vyema. Amesema wanafunzi wanapaswa kulinganiwa kwa maneno na vitendo jinsi ya kutaamali na kutafakari masuala ya akhera na kutafuta elimu kwa nia safi na kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.
Amesema kuwa kukutana kwake na maulama, wahadhiri na wafafunzi wa Qum ni jambo lenye faida kubwa na litakalokumbukwa siku zote. Amepongeza pia matamshi yaliyotolewa na wahadhiri na maulama katika mkutano huo na akasema kuwa mipango yote inapaswa kutekelezwa kwa kutilia maanani hali ya mambo ili kuweza kufanikisha utekelezaji wake.
Ameunga mkono matamshi yaliyotolewa na baadhi ya wahadhiri kuhusu sayansi za jamii na akasisitiza kuwa taaluma hizo ni muhimu na za dharura kwa sharti kwamba zibuniwe kwa mujibu wa aidiolojia ya Kiislamu.
Ameitaka hauza na vyuo vya kidini kubuni sayansi za jamii kwa mujibu wa aidiolojia na teolojia ya Kiislamu.
Mwanzoni mwa mkutano huo wahadhiri 12 wa hauza na vyuo vya kidini, maulama na wanafunzi wa hauza ya Qum walitoa maoni yao kuhusu masuala mbalimbali yanayohusiana na vyuo vya kidini, taaluma za fiqhi, sayansi, falsafa na masuala ya kijamii na kiutamaduni.
682103
captcha