IQNA

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu akutana na Uongozi wa Hawza ya Qum

22:26 - October 27, 2010
Habari ID: 2021110
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Jumanne usiku, Oktoba 26, 2010, ameonana na wajumbe wa Baraza Kuu la Chuo Kikuu cha Kidini na huku akisisitizia udharura wa kuandaliwa mfumo mkuu wa elimu, utafiti na tablighi katika Hawza ameongeza kuwa, moja ya mambo muhimu sana ya Chuo Kikuu cha kidini ni kutunga na kuandaa mpango wa stratijia za muda mrefu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema, kuweko mpango wa muda mrefu wa kiistratijia ndiko kunakoweza kufungua uwanja kuweko mipango na kuainisha vipaumbele vya kielimu na kuongeza kuwa, uongozi na uendeshaji wa taasisi za Hawza nao inabidi urahisishie watu mambo na kuwasahilishia huduma.

Amesema ni jambo la dharura kuweko mawasiliano ya kuendelea na ya kudumu kati ya Baraza Kuu la Hawza ya Qum na marajii na wanavyuoni wakubwa na kuongeza kuwa, kuna haja pia ya kustafidi na mitazamo na fikra za fudhalaa vijana katika Hawza.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, yeye haingilii kabisa misimamo na maamuzi ya Baraza Kuu la Chuo Kikuu cha kidini cha Qum.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza juu ya haja ya kutowekewa mipaka namna na mbinu za usomeshaji wa vijana katika Chuo Kikuu cha kidini na kuongeza kuwa, irfani ya kivitendo ni moja ya masuala ya dharura yanayopaswa kutiliwa maanani na wanafunzi na watu wa dini.

Aidha amekumbushia mjadala unaohusiana na kuweko mageuzi na mabadiliko katika Hawza mjadala ambao umepata nguvu katika miaka ya hivi karibuni na ameongeza kuwa, suala la kuweko mabadiliko katika Chuo Kikuu cha kidini inabidi lifuatiliwe kwa uzito wa hali ya juu na lipewe umuhimu mkubwa.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amelishukuru Baraza Kuu la Uongozi wa Chuo Kikuu cha Kidini cha Qum kutokana na kazi zake kubwa linazofanya.

Mwanzoni mwa mkutano huo, Ayatullah Yazdi, Mkuu wa Baraza Kuu la Chuo Kikuu cha Kidini cha Qum ametoa ripoti kuhusiana na muundo mpya wa baraza na kamati za wataalamu za baraza hilo na vile vile masuala yaliyopitishwa na baraza lake na kuongeza kuwa, kuchunguza kiwango cha kielimu cha Vyuo Vikuu vya kidini kote nchini Iran sambamba na kuviainishia daraja zake, kuanzishwa ofisi ya shakhsia wenye vipaji na kuasisi mfumo wa uratibu wa pamoja wa kiidara na kifedha katika majimui ya Hawza pamoja na kuwa na ajenda ya mfuko wa kuwaunga mkono watafiti katika Chuo Kikuu cha kidini ni miongoni mwa mambo yaliyopasishwa na Baraza Kuu la Hawza ya Qum.

Kwa upande wake, Ayatullah Muqtadai, mkuu wa Vyuo Vikuu vya kidini amesema katika ripoti yake kwamba kuleta mabadiliko na mageuzi katika muundo wa Hawza kunakokwenda sambamba na risala na ujumbe wake, kuandaa mpango wa wamaendeleo wa miaka 20, kuasisi Baraza la Sera za Tablighi na kamati ya kusimamia baraza hilo, kurahisisha masuala ya elimu kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya mawasiliano na vile vile kuanzisha mfumo madhubuti wa kutoa taarifa za elimu ni sehemu ya hatua zilizochukuliwa hadi hivi sasa nchini.

Aidha katika mkutano huo, baadhi ya wajumbe wa baraza hilo wamezungumzia mambo mbali mbali kuhusiana na udharura wa kuweko mipango mizuri ya kulinda na kulea vipaji vya watu katika Vyuo Vikuu vya kidini nchini, kutumia vizuri mitazamo ya marajii muhtaramu, ulazima wa kuweko kwa vipindi vya muda maalumu baadhi ya wahadhiri bingwa katika Hawza za miji mbali mbali nchini na kuandaliwa mipango ya muda mfupi na ya muda mrefu kwa ajili ya kuleta mageuzi na mabadiliko katika Hawza.
683885
captcha