IQNA

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu: "Msitosheke na mpaka maalumu katika harakati ya maendeleo"

13:02 - November 11, 2010
Habari ID: 2029942
Sherehe za nne za wanachuo na kuhitimu wanafunzi wa vyuo vikuu vya maafisa wa jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimefanyika Jumatano Novemba 10 katika Chuo Kikuu cha Jeshi la Anga cha Shahid Sattari mjini Tehran zikihudhuriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei.
Mwanzoni mwa sherehe hizo Amiri jeshi wa majeshi ya Iran alikwenda kwenye kumbukumbu ya mashahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa ajili ya kuwasomea al Fatiha na kuwaombea dua na daraja za juu peponi. Baada ya hapo Ayatullah Khamenei alikagua gwaride la vikosi vya jeshi la Jamhuri ya Kiislamu.

Baadaye Ayatullah Khamenei amehutubia vikosi vya jeshi akisema kuwa kigezo cha nguvu katika mfumo wa Kiislamu kinategemea imani, kumtegemea Mwenyezi Mungu na juhudi zilizojaa ikhlasi katika njia ya malengo aali. Amesisitiza kuwa vikosi vya jeshi la Iran vimeweza kupata maendeleo makubwa katika kuzalisha zana za kijeshi kutokana na imani na kumtegemea Mwenyezi Mungu na kwamba jeshi la anga limekuwa mstari wa mbele katika medani hiyo.

Amiri jeshi wa majeshi ya Iran amesema, kufuata mafundisho ya Mwenyezi Mungu na kuwa na malengo ya kibinadamu na mfungamano wa kiroho na wananchi ni sifa kuu mbili za jeshi la Jamhuri ya Kiislamu. Amesema kuwa nidhamu, zana za kijeshi na mafunzo vina nafasi muhimu katika vigezo vya nguvu vya mfumo wa Kiislamu lakini roho ya yote hayo ni kuhisi kuwa na wajibu mbele ya Mwenyezi Mungu na kumtegemea Yeye.

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa madola ya kimaada ambazo kigezo na nguzo ya nguvu na uwezo wao ni zana za kijeshi na mahesabu ya kimaada pekee, hayawezi kulishinda taifa linalofuata kigezo cha uwezo na nguvu cha Kiislamu. Amesema kuwa mfano hai wa nguvu za kiroho kushinda nguvu za kimaada ni ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ambapo taifa la Iran liliweza kuushinda utawala wa kidhalimu wa Shah kwa kutegemea nguvu ya imani licha ya kuwa mikono mitupu.

Amesema mfano mwingine wa ushindi wa nguvu ya imani dhidi ya nguvu za kimaada ni ushindi wa taifa la Iran katika vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran. Ayatullah Khamenei amesema taifa la Iran ambalo katika kipindi cha kujitetea kutakatifu lilikuwa chini ya vikwazo vya pande zote, liliweza kuushindwa utawala wa Kibaathi wa Iraq uliokuwa ukisaidiwa kikamilifu na madola ya Mashariki na Magharibi kwa kutegemea imani na ushujaa wa vijana na majeshi ya Iran.

Amiri jeshi wa majeshi ya Iran amesema kuwa moja ya sifa makhsusi za nguvu na uwezo wa Kiislamu ni kuimarisha hali ya kujitegemea na kuchanua vipawa vyake bila ya kutegemea wageni. Ameongeza kuwa katika kigezo cha nguvu za Kiislamu, inawezekana kujitenga na kutowategemea mabeberu wa dunia na kutengeneza jeshi lililojizatiti kwa zana na fikra za Kiirani.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa maendeleo ya vikosi vya majeshi ya Iran katika kutengeneza zana tata na za kisasa za kijeshi ni matokeo ya fikra hiyo. Ameongeza kuwa taasisi ya kwanza ya jihadi ya kujitosheleza iliibuka katika jeshi la anga na kwamba mashahidi kama Sattari, Babai, Hadhrai na Dourani walikuwa mstari wa mbele wa harakati hiyo.

Ayatullah Khamenei amewahimiza wanachuo wa vyuo vikuu vya maafisa wa jeshi la Iran kudumisha njia hiyo ya mashahidi azizi na kufanya harakati kwa kufuata kigezo cha nguvu na uwezo cha Kiislamu. Amesema: “Masomo, uhakiki na utafiti unapaswa kufanyika katika fremu ya kujitegemea na kwa kutumia uzoefu wa wataalamu wakongwe na wala msitosheke na mpaka maalumu katika harakati ya maendeleo.”

Ayatullah Khamenei amesema kuwa njia ya kuelekea kwenye ukamilifu na ufanisi haina mwisho. Amesisitiza kuwa vyuo vikuu vya vikosi vya majeshi ya Iran ni miongoni mwa vituo vya kielimu vinavyotia matumaini makubwa hapa nchini na vinapaswa kuzidisha kazi katika harakati hiyo ya kusonga mbele kwa kutazama mustakbali na kuweka dira ya wazi.

Baadhi ya familia za mashahidi, wahadhiri, makamanda wa jeshi na wanafunzi bora walienziwa katika sherehe hiyo ya kuapishwa wanachuo waliohitimu katika vyuo vikuu vya maafisa wa jeshi la Iran.

Mwanzoni mwa sherehe hiyo Brigedia Jenerali Shah Saffi, kamanda wa kikosi cha jeshi la Anga la Iran alitoa hotuba akisisitiza kuwa wanafunzi wa vyuo vikuu vya maafisa wa jeshi la Jamhuri ya Kiislamu wameingia katika medani ya jihadi na vita laini kwa kutegemea imani, nidhamu na elimu ya kisasa na daima wako tayari kukabiliana na lolote.

Vilevile Brigedia Jenerali Sheikh Hasani, mkuu wa Chuo Kikuu cha Jeshi la Anga cha Sattari ametoa ripoti kuhusu hali ya masomo katika chuo hicho.
693205
captcha