IQNA

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Jihadi kwa maana yake pana hulipa taifa maendeleo na matumaini

12:48 - November 18, 2010
Habari ID: 2033612
Ayatullah Khamenei amesema kuwa jihadi kwa maana yake pana hulipa taifa maendeleo na matumaini. Ameongeza kuwa jihadi ina maana ya kuwepo katika medani, harakati sambamba na kutambua wadhifa na mapambano ya kudumu dhidi ya vizuizi vya mandeleo na ustawi; mahudhurio haya mara nyingine huambatana na kusabilia roho na mali, wakati mwingine kushiriki katika medani mbalimbali za kijamii na kisiasa na hata kuwa na mahudhurio katika medani za kifikra.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei leo amehutubia umati mkubwa wa wananchi wa mkoa wa Isfahan waliokwenda kuonana naye akisisitiza kuwa imani na kushikamana na thamani za Mwenyezi Mungu ndiyo siri ya mafanikio ya taifa la Iran. Ayatullah Khamenei amesema taifa la Iran litaendelea kupata ushindi na kuwa mstari wa mbele katika nyanja zote kwa kuimarisha mfungamano huo wenye baraka, na adui ataendelea kushindwa na kupoteza matumaini.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa mkono na baraka na heri kwa taifa lenye imani na lenye kujitolea la Iran na Waislamu wote ulimwenguni kwa mnasaba wa sikukuu ya Idul Haji na kusema kuwa kuelewa vyema hikima na falsafa ya Idul Adh’ha ni ufunguo wa nyanja mbalimbali za maisha ya mtu binafsi na taifa. Ameongeza kuwa kujitolea vilivyo kwa Nabii Ibrahim (as) na malipo makubwa ya Mwenyezi Mungu kwa Mtume huyo adhimu ni nembo ya hakika yenye hikima kubwa kwamba ni muhali kuweza kukata masafa katika njia ya ufanisi, maendeleo na daraja za juu bila ya kujitolea.
Amesema kuwa falsafa ya mitihani ya mara kwa mara ya Mwenyezi Mungu ni kutaka kuwawezesha watu na mataifa kuingia katika awamu mpya ya maendeleo na ustawi. Amesisitiza kuwa kila mtu anayevuka bonde la mitihani, mashaka na matatizo huwa amepiga hatua mbele kuelekea kwenye malengo aali kwa baraka zake Mola.
Kuhusu suala hilo la falsafa ya mitihani ya Mwenyezi Mungu, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria fitina za mwaka jana na jinsi taifa la Iran lilivyofanikiwa kuvuka mtihani huo.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa maana ya taufiki ya taifa la Iran ya kuvuka fitina hiyo si kudhihiri nguvu na uwezo wa taifa hili pekee bali maana halisi ya mafanikio ya taifa ya kuvuka kwa mishindo mtihani na mashaka ya mwaka jana ni kwamba taifa hili limeingia katika awamu na kipindi kipya cha uhai wake na kupata nishati mpya kwa ajili ya kufikia kwenye lengo lake la juu kabisa kwa kutegmea imani, uwezo wa kumaizi, kutambua hali ya mambo na kuelewa vyema mahitaji ya zama.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa hamasa ya wananchi wa mkoa wa Isfahan hapo tarehe 25 Aban 1361 (16 novemba 1982) ni kielelezo kingine cha mafanikio ya Iran katika mitihani ya Mwenyezi Mungu. Ameongeza kuwa katika siku hiyo adhimu sambamba na kusindikiza mashahidi 370, wananchi wa Isfahan walipeleka maelfu ya vijana wao shupavu katika medani za vita na kuonesha mfano wa juu kabisa wa kujitolea.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa mahudhurio ya wananchi wenye imani, utamaduni na wanamapinduzi wa mkoa wa Isfahan katika masuala mbalimbali ya kabla na wakati wa Mapinduzi ya Kiislamu, katika vita vya kulazimishwa na vilevile katika nyanja mbalimbali za maendeleo na ustawi wa taifa ni dhihirisho la roho ya imani, kujitolea na jihadi ya wananchi wa mkoa huo. Amesema kuwa kutafakari na kutaamali katika fahari hizo kunatupa fursa ya kutambua utambulisho na vipawa vya watu wa Isfahan na kuweka wazi njia ya maendeleo na ustawi wa wananchi hao.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa jihadi kwa maana yake pana hulipa taifa maendeleo na matumaini. Ameongeza kuwa jihadi ina maana ya kuwepo katika medani, harakati sambamba na kutambua wadhifa na mapambano ya kudumu dhidi ya vizuizi vya mandeleo na ustawi; mahudhurio haya mara nyingine huambatana na kusabilia roho na mali, wakati mwingine kushiriki katika medani mbalimbali za kijamii na kisiasa na hata kuwa na mahudhurio katika medani za kifikra.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu pia ameashiria kushindwa mara kwa mara njama za maadui akisisitiza kuwa ni muhali kuweza kupambana na taifa linalojitolea na kupigana jihadi la Iran. Amesema kambi ya maadui wa Uislamu, Mapinduzi ya Kiislamu na Iran haikuweza kusimama kidete mbele ya wananchi wa Iran hata kwa kutumia vita na vitisho vya kijeshi na wale wanaofikiria kulipigisha magoti taifa la Iran kwa kutumia vikwazo, wanatwanga maji kwenye kinu.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa matarajio ya maadui wa Iran ni kuzusha migawanyiko katika taifa, kuanzisha ufa kati ya wananchi na viongozi wao na kuzusha hali ya ukosefu wa maelewano na mabishano juu ya masuala yasiyokuwa na maana; kwa msingi huo wananchi wote wanapaswa kuwa macho mbele ya harakati hizo za maadui.
Amewakosoa vikali wale wanaoneza hali ya ukosefu wa matumaini, kukata tamaa na hitilafu kwa kuuzulia tuhuma mfumo wa Kiislamu hapa nchini katika masuala yanayowafurahisha wageni na akaongeza kuwa watu hawa wanafanya kazi kwa niaba ya maadui wa taifa la Iran na wanataka kufidia kushindwa kwa propaganda za Wazayuni na Wamarekani; hata hivyo taifa linatambua kwamba harakati kama hizo ni usaliti wa wazi.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa maadui wanatumia mbinu za kueneza ufuska, utovu wa maadili na dawa za kulevya kama nyenzo za kufikia malengo yao na amelitaka taifa na viongozi hususan tabaka la vijana kuwa macho.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja mkoa wa Isfahan kuwa ni kituo cha elimu ya dini na sayansi za aina mbalimbali. Ameashiria chuo kikuu cha kidini chenye mafanikio na vyuo vikuu vyenye hadhi vya Isfahan na akasema kuwa mkoa huo uliwahi kuwa kituo cha tochi ya elimu katika ulimwengu wa Kiislamu. Amewataka maulamaa, wasomi na wasanii wa mkoa huo kulitia maanani suala hilo katika shughuli na kazi zao.
Mwanzoni mwa mkutano huo Ayatullah Tabatabai Nejad, mwakilishi wa Faqihi Mtawala na Imam wa Ijumaa wa Isfahan ametoa hotuba fupi akiashiria mchango mkubwa wa wakazi wa mkoa huo katika kipindi chote cha vita vya kujitetea kutakatifu (vita vilivyoanzishwa na Saddam Hussein dhidi ya Iran) na baada yake na akasema kuwa tarehe 25 Aban mwaka 1361 (16 Novemba 1982) inakumbusha siku ya kihistoria ya kuwa mstari wa mbele wananchi wa Isfahan katika medani ya jihadi na kujitolea, kwa sababu hiyo siku hiyo katika historia ya Isfahan imepewa jina la “Siku ya Hamasa ya Kujitolea ya Isfahan”.
Ayatullah Tabatabai Nejad ameongeza kuwa wananchi wa Isfahan wataendelea kuwepo katika medani mbalimbali za kutetea na kulinda Uislamu na Mapinduzi ya Kiislamu kama chaguzi na maendeleo ya kisayansi na ujenzi wa taifa. 697303

captcha