IQNA

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Mapambano yameuzuia utawala ghasibu wa Israel

7:23 - November 30, 2010
Habari ID: 2039887
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhma Ali Khamenei amekutana na Waziri Mkuu wa Lebanon Saad Hariri mjini Tehran Novemba 29 na kusema kwamba jambo pekee linalouzuia utawala huo ghasibu kuvamia Lebanon ni kuweko harakati ya mapambano.
Kiongozi Muadhamu amesema katika mazungumzo hayo kuwa, Lebanon ni nchi muhimu iliyoko mstari wa mbele katika kupambana na utawala ghasibu wa Israel na kuongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka kuona Lebanon iliyostawi, yenye ufanisi na maendeleo ya hali ya juu.
Amesisitiza kuwa Iran haitosita kutoa msaada wowote ule utakaopelekea kupatikana ustawi Lebanon na kuongeza kuwa, kupata mafanikio wananchi wa Lebanon ni furaha kwa Iran kama ambavyo matatizo na mitihani inayopata nchi hiyo inaiumiza na kuisikitisha Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia mazungumzo yaliyofanyika baina ya nchi mbili mjini Tehran na kukumbusha kuwa, kuna nyanja nyingi za kuweza kuimarisha zaidi uhusianio wa Iran na Lebanon katika sekta tofauti na kwamba inabidi uhusiano huo uimarishwe zaidi hususan katika sekta za biashara na ujenzi.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia juu ya uchokozi wa mara kwa mara wa utawala wa Kizayuni dhidi ya Lebanon na kuendelea kuwepo uwezekano wa kuzidi kushuhudiwa uchokozi wa utawala huo ghasibu na kusisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni kama ungeliweza kuiteka Beirut ingeliuteka pia mji wa Tripoli (wa kaskazini mwa Lebanon) na kufikia hadi ya kuizingira Syria, na kwamba jambo pekee linalouzuia utawala huo ghasibu kufanya hivyo ni kuweko harakati ya mapambano au muqawamah.
Amesisitiza kuwa, Lebanon ndiyo nchi pekee ya Kiarabu iliyoweza kuushinda utawala wa Kizayuni katika vita na kukumbusha kuwa, muqawamah ndicho kitu pekee kilichowafanya maadui wa Lebanon washindwe kukabiliana na nchi hiyo, hivyo inabidi muqawamah utunzwe na uhifadhiwe kikamilifu.
Ayatullah Udhma Khamenei aidha ameelezea kufurahishwa kwake na uhusiano mzuri uliopo baina ya Saad Hariri, Waziri Mkuu wa Lebanon na Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah pamoja na viongozi wengine wa muqawamah na kusisitiza kwamba, inabidi uhusiano huo uimarishwe kadiri inavyowezekana.
Vile vile amekumbusha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono kikamilifu umoja, mshikamano na uhuru wa Lebanon na kuongeza kuwa, Lebanon ni nchi yenye wafuasi wa dini na madhehebu mengi tofauti, lakini wafuasi wa dini na makundi hayo yoe wamekuwa wakiishi pamoja kwa salama na amani, lakini pamoja na hayo kuna baadhi ya watu wanafanya njama za kuzusha migogoro na mizozo ya kidini na kimadhehebu nchini humo na inabidi kupambana vikali na watu wenye fikra za namna hiyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia mazungumzo yake yaliyofanyika miaka kadhaa iliyopita kati yake na marhum Rafiq al Hariri Waziri Mkuu wa zamani wa Lebanon (ambaye pia ni baba yake Saad Hariri, Waziri Mkuu wa hivi sasa wa nchi hiyo) na amemsifu Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Lebanon kutokana na juhudi nyingi alizokuwa akizifanya kwa ajili kuiletea maendeleo nchi yake.
Katika mazungumzo hayo yaliyohudhuriwa pia na Bw. Rahimi, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Bw. Saad Hariri, Waziri Mkuu wa Lebanon amesema amefurahishwa na mazungumzo aliyofanya na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa, Lebanon inaihesabu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ni nchi rafiki na ndugu ambayo imekuwa pamoja na wananchi wa Lebanon katika vipindi vyote vigumu.
Ameongeza kuwa, serikali ya Lebanon inapenda kuona uhusiano wa nchi hiyo na Iran unazidi kuimarishwa hususan katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni.
Waziri Mkuu wa Lebanon aidha amesema serikali ya nchi hiyo ni serikali ya umoja wa kitaifa iliyoundwa na mirengo na makundi yote muhimu ya nchi hiyo na kuongeza kuwa, lengo kuu la serikali ya Lebanon ni kulinda na kutia nguvu umoja wa kitaifa, kufanyia kazi masuala yenye kuleta mshikamano na kusimama kidete mbele ya maadui.
Bw. Saad Hariri ameongeza kuwa, utawala pekee unaonufaika na mivutano na hitilafu zozote zile za ndani ya Lebanon, ni utawala wa Kizayuni wa Israel.
703742



captcha