IQNA

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu aainisha Kigezo cha Maendeleo cha Kiislamu - Kiirani

13:43 - December 04, 2010
Habari ID: 2041659
Mkutano wa kwanza wa "Fikra za Kiistratijia" katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ulifanyika mjini Tehran Jumatano usiku, Novemba 11, 2010, na kuhudhuriwa na Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na makumi ya wasomi, wahadhiri wa Vyuo Vikuu pamoja wanafikra wa Vyuo Vikuu na Hawza (Vyuo Vikuu vya Kidini).
Mkutano huo umezungumzia fikra za pamoja na kujadili misingi, sifa za kipekee na vipengee mbalimbali vya Kigezo cha Maendeleo cha Kiislamu - Kiirani.
Mwanzoni mwa mkutano huo uliodumu kwa muda wa masaa manne, wasomi na wanafikra 14 wametumia karibu masaa matatu na nusu kutoa mitazamo yao mbalimbali katika suala zima la Kigezo cha Maendeleo cha Kiislamu - Kiirani.
Ayatullah Udhma Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amehutubia mkutano huo akitilia mkazo suala la udharura wa kutumiwa suhula na uwezo wote walio nao watu wenye vipaji nchini katika kuandaa, kubuni na kutunga kigezo hicho cha kiistratijia akisisitiza kuwa mambo manne yaani "fikra, elimu, maisha na umaanawi" ni muhimu sana katika suala la kuandaa Kigezo cha Maendeleo cha Kiislamu - Kiirani. Amesisitiza kuwa, kigezo hicho kitakuwa ni hati na sanadi muhimu kwa ajili ya marejeo ya kuandalia mipango na malengo ya muda mrefu ya nchi.
Ayatullah Udhma Khamenei vilevile ameelezea kufurahishwa kwake na makala ya kielimu na hotuba zilizotolewa na wanafikra na wahadhiri wa Vyuo Vikuu katika mkutano huo wa kwanza wa fikra za kiistratijia na kuongeza kuwa, suala hilo linaonyesha uwezo mkubwa wa kielimu na kifikra walio nao wasomi na wanafikra nchini. Ameongeza kuwa, haijawahi kutokea kufanyika mkutano wenye kiwango na upeo kama huo katika katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Amesisitiza pia juu ya haja ya kuendelea kufanyika vikao na mikutano kama hiyo ya fikra za kiistratijia akisema kuwa, moja ya malengo makuu ya kufanyika silisila ya mikutano kama hiyo ni kuwafanya wasomi na wanafikra wahusike moja kwa moja katika masuala ya kimsingi na makuu ya nchi. Ameongeza kuwa, nchini Iran kuna malengo na kazi kubwa ambazo zinahitajia msaada wa wasomi, watu wenye vipaji na wanafikra kuweza kufanikishwa na kwamba ili suala hilo liweze kutimia, inabidi fikra za wasomi na wananadharia zipewe kipaumbele na kuhusishwa moja kwa moja.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema malengo mengine ya kuitishwa vikao kama hivyo vya kiistratijia ni kueneza utamaduni wa majadiliano kuhusu masuala makuu na muhimu ya nchi kati ya wasomi na wanafikra wenyewe kwa wenyewe na baadaye kati ya wananchi wa kawaida katika jamii na kusisitiza kuwa, lengo la tatu la kuitishwa vikao hivyo ni kuainisha njia na namna ya kuweka gurudumu kwa ajili ya mustakbali bora wa nchi.
Ayatullah Udhma Khamenei aidha amesisitiza juu ya haja ya kujiepusha na maamuzi ya pupa katika juhudi za kuyafikia malengo ya mwisho na kuongeza kuwa, kubuniwa na kuandaliwa Kigezo cha Maendeleo cha Kiislamu - Kiirani ni suala lenye malengo ya muda mrefu na ukweli wa mambo ni kuwa matunda ya hatua hiyo hayawezi kuonekana katika kipindi cha muda mfupi hivyo inabidi kuongezwe kasi inayokubalika katika suala hilo.
Amekumbusha kuwa, ndani ya Kigezo cha Maendeleo cha Kiislamu - Kiirani, huainishwa malengo maalumu lakini mikakati inaweza kubadilika kulingana na mazingira na hali ilivyo na kwamba jambo hilo linaonesha jinsi kigezo kinavyopaswa kunyumbulika.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinhduzi ya Kiislamu ametoa ufafanuzi kuhusu istilahi ya "Kigezo cha Maendeleo cha Kiislamu - Kiirani" akisema kuwa neno "Kigezo" katika istilahi hiyo lina maa ya ramani kuu na kuongeza kuwa, bila ya kuwa na ramani kuu kunaweza kupelekea kushuhudiwa migongano katika baadhi ya masuala kama ilivyoshuhudiwa katika baadhi ya kadhia za kiutamaduni na kiuchumi kwenye kipindi cha miaka 30 iliyopita.
Amma kuhusiana na neno "Kiislamu" lililomo kwenye istilahi hiyo, Ayatullah Udhma Khamenei amesema, inabidi malengo, matukufu na mbinu zote za kigezo hicho zisimame juu ya maarifa, mafundisho na misingi ya Uislamu. Ameongeza kuwa, jamii na utawala wa Iran ni wa Kiislamu na kwamba Wairani wanajivunia kuona kuwa wanaweza kutegemea misingi ya Kiislamu kwa ajili ya kubuni, kutunga na kuandaa kigezo chao cha maendeleo.
Vile vile ametoa ufafanuzi kuhusu kutumika neno "Kiirani" katika istilahi hiyo akisema kuwa ni kutiliwa mkazo masuala kama ya udharura wa kuzingatia mazingira ya kihistoria, kijiografia, kiutamaduni, kiuchumi na kijamii ya Iran ndani ya kigezo hicho na kuongeza kuwa, fauka ya masuala hayo yote, watungaji na waandaaji wa kigezo hicho nao ni wanafikra wa Kiirani na kwamba Kigezo hicho cha Maendeleo ya Kiislamu - Kiirani ni dhihirisho la juhudi za wasomi wa nchi hii kwa ajili ya kuiandalia nchi yao mustakbali mwema.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema kuhusu neno "Maendeleo" lililomo kwenye istilahi ya "Kigezo cha Maendeleo cha Kiislamu - Kiirani" kwamba, limetumika neno hilo la "maendeleo" badala ya "ustawi" kwa sababu neno "ustawi" hivi sasa limekuwa ni istilahi maarufu ya kimataifa duniani yenye vigezo na mambo yake maalumu ya lazima ambayo Iran haikubaliani nayo hivyo kumetumika neno "maendeleo" ili sambamba na kujiepusha kukopa istilahi ya wengine, (tuweze kuonesha kuwa, istilahi hii ni kitu kingine kabisa tofauti na hicho kilichozoeleka duniani) jambo ambalo limekuwepo katika kipindi chote cha historia ya Mapinduzi ya Kiislamu.
Amesema suala la kuchorwa hali inayotakiwa na jinsi ya kutoka katika hali ya hivi sasa na kufikia kwenye hali inayotakiwa, ni miongoni mwa masuala ya lazima ya kubuniwa, kuchorwa na kutungwa Kigezo cha Maendeleo cha Kiislamu - Kiirani. Ameongeza kuwa, kutumiwa maneno mawili ya "Kiislamu - Kiirani" katika istilahi hiyo kamwe hakuna maana ya kuwa Iran haitotumia mafanikio na uzoefu sahihi wa wengine. Amesisitiza kuwa, Wairani wanaangalia kwa macho mawili maendeleo sahihi ya kisayansi na kiteknolojia duniani na kuchagua bora yanayowafaa.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia juu ya ulazima wa kuulizwa maswali na kutolewa majibu juu ya maswali yote yanayohusiana na Kigezo cha Maendeleo cha Kiislamu - Kiirani na kuongeza kuwa, moja ya maswali hayo ni hili kwamba kwa nini hivi sasa ndipo ilipoamuliwa kubuniwa, kutungwa na kuchorwa kigezo hicho?
Akijbu swali hilo amesema, uzoefu mwingi sana na maarifa chekwa na pomoni yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 30 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran ni mambo yanayoonesha kuwa hivi sasa ndio wakati bora kabisa wa kuanza njia na harakati hiyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, kuna baadhi ya watu wanadai kuwa hivi sasa nchini Iran hakuna uwezo wa kifikra wa kuweza kupata kigezo hicho, lakini ukweli wa mambo ni kuwa, uwezo mkubwa wa wanafikra tulio nao hivi sasa na suhula bora zilizopo nchini ni uthibitisho kuwa wasomi na wanafikra wa Kiirani wanao uwezo wa kuchora na kuandaa kigezo hicho na bila ya shaka yoyote harakati hii itafanikiwa tu.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa ufafanuzi zaidi kuhusu kigezo hicho kwa kuashiria masuala manne yaani "fikra, elimu, maisha na umaanawi" na kuongeza kuwa, Kigezo cha Maendeleo cha Kiislamu - Kiirani inabidi kibuniwe na kupangiliwa vyema kwa namna ambayo kitaiongoza jamii ya Kiirani kuelekea kwenye jamii ya wanafikra yenye kuchipua yenyewe fikra na mawazo yenye kujenga.
Aidha ametaka kubainishwe mikakati ya mambo ya lazima ya maendeleo katika suala zima la fikra na kutiliwa maanani nyenzo zake ikiwa ni pamoja na suala zima la elimu na malenzi pamoja na vyombo vya habari katika suala hilo la kubuni na kuchora kigezo hicho cha maendeleo.
Suala la elimu ni kadhia ya pili ambayo Kiongozi Muadhamu ameitaja kuwa ni muhimu sana katika kubuniwa na kutungwa kigezo cha maendeleo nchini.
Amesema, ubunifu na harakati nzuri iliyopo nchini katika upande wa kujitegemea kielimu inabidi iendelee kwa kasi ya hali ya juu kabisa na inabidi kigezo hicho cha maendeleo kibainishe njia mbali mbali za maendeleo ya pande zote, kwa kina na kwa misingi madhubuti ya kielimu.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema ni jambo la dharura na muhimu kuzingatiwa masuala ya namna na njia kuu za maisha kama vile usalama, uadilifu, ustawi, uhuru, utawala, istikilali, kujitegemea na heshima ya taifa katika kadhia nzima hiyo ya Kigezo cha Maendeleo cha Kiislamu - Kiirani na kuongeza kuwa, kigezo hicho inabidi kilipe umuhimu wa kutosha suala la maisha.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja umaanawi kuwa ni sulala la nne muhimu ambalo linapaswa kuzingatiwa katika kazi ngumu, nzito, inayohitajia umakini wa hali ya juu na yenye malengo ya muda mrefu ya kubuni, kuchora na kutunga Kigezo cha Maendeleo cha Kiislamu - Kiirani akisema kuwa, umaanawi ndiyo roho ya maendeleo ya kweli katika nyuga na mambo yote.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbusha kuwa maisha ya mwanaadamu katika kipindi cha kudhihiri Imam wa Zama, Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake) ni mfano kamili wa maisha bora ya mwanaadamu na ameongeza kuwa, licha ya mwanaadamu kupitisha maelfu ya miaka katika maisha yake lakini bado anakabiliwa na misukosuko na matatizo mengi na kwamba binaadamu ataweza kupata maendeleo ya juu kabisa wakati wa kudhihiri Imam Mahdi AS, tab'an inabidi juhudi zisizosita ziendelee kufanyika katika uga huo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameendeleza hotuba yake katika mkutano wa kwanza kwa fikra za kiistratijia uliofanyika mjini Tehran kwa kutilia mkazo suala la kuzingatiwa Uislamu kama msingi mkuu wa kigezo cha maendeleo.
Amesema, suala la kutiliwa maanani kikamilifu tawhidi ni jambo la dharura kabisa katika kigezo hicho cha maendeleo na kuongeza kuwa, kama tawhidi, kumwamini Mwenyezi Mungu na kuheshimu vilivyo imani hiyo kutasambaa na kuenea katika vipengee vyote vya maisha ya kila siku ya mwanaadamu, basi matatizo yote ya jamii ya binaadamu yataweza kutatuliwa na kutaweza kufunguliwa njia ya kupatikana maendeleo ya kweli ya mwanaadamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, kuzingatiwa Siku ya Kiama na Siku ya Hesabu katika kigezo hicho cha maendeleo kutapelekea kukubalika kiakili na kimantiki suala la kuvumilia matatzo yote na kuendelezwa fikra za kujitolea kwa ajili ya kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu. Amekumbusha kuwa, mafhumu hiyo ya kimsingi na muhimu mno, inabidi ipate maana yake halisi katika Kigezo cha Maendeleo cha Kiislamu - Kiirani.
Kushikamanisha na kutotenganisha baina ya dunia na Akhera na suala la mwanaadamu kuwa mhimili mkuu katika mtazamo wa Uislamu ni nukta nyingine ambazo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezitilia mkazo katika suala zima la mambo ya Kiislamu yanayotakiwa kuwemo kwenye kigezo hicho cha maendeleo.
Amesema suala la mwanadamu kuwa kigezo katika mtazamo wa Kiislamu na kwenye falsafa za kimaada za Magharibi ni mambo mawili yanayotofautiana kikamilifu na kukumbusha kuwa, lengo kuu la Uislamu ni kumuongoza mwanaadamu kwenye njia sahihi ambapo kwa mtazamo huo, masuala yote yakiwemo ya uadilifu, ustawi, usalama na ibada ni utangulizi na ni malengo ya awali tu kwa ajili ya kumfikisha mwanaadamu kwenye lengo kuu nalo ni kumpa ufanisi wa kweli kiumbe huyo.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema, mwanaadamu kwa mtazamo wa Uislamu ni kiumbe chenye khiari, mukalafu (mwenye majukumu ya kutekeleza kidini), na anayetakiwa kuwa kwenye uongofu wa Mwenyezi Mungu. Aidha amesisitiza juu ya wajibu wa kufanywa jambo hilo lionekane wazi katika kigezo hicho cha maendeleo na kusema, kwa mtazamo huo, suala la demokrasia pamoja na kwamba ni haki ya wananchi lakini pia ni takilifu na wajibu wa kidini wa wananchi hao na mtu hawezi kusema kuwa haumuhusu ufanisi au uharibifu wa jamii.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema suala la utawala kwa mtazamo wa Kiislamu ni jambo jingine ambalo inabidi lipewe uzingatiaji wa kutosha katika Kigezo cha Maendeleo cha Kiislamu - Kiirani.
Ameongeza kuwa ustahiki wa kila mtu katika Uislamu ni jambo muhimu mno kiasi kwamba mtu yeyote anayetaka kuchukua uongozi na jukumu la kuongoza sekta fulani anapaswa kwanza ajijengee sifa za kumpa ustahiki wa jambo hilo na kama atachukua majukumu bila ya kustahiki atakuwa anafanya jambo lisilokubalika kwa mujibu wa sheria za dini.
Ayatullah Udhma Khamenei amebainisha nukta nyingine katika mtazamo wa Kiislamu kuhusiana na utawala akisema, katika Uislamu watu wenye ubinafsi na wanaojiona bora kuliko wengine ambao wanajikumbizia wao kila kitu, hawana haki ya kutaka kupewa uongozi, na wananchi nao hawana haki kwa mujibu wa sheria za Uislamu ya kuwachagua watu wa namna hiyo na kwamba mtazamo huu wenye kuleta mafanikio inabidi uwemo na upewe nafasi ya kutosha katika Kigezo cha Maendeleo cha Kiislamu - Kiirani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema ni jambo la dharura pia kuzingatiwa suala la uchumi na iktisadi katika kigezo hicho cha maendeleo. Ameongeza kuwa, katika kigezo hicho cha maendeleo ambacho kitatungwa na kupangiliwa kwa itifaki ya mitazamo ya wanafikra na juhudi za watu wenye vipawa nchini, inabidi suala la uadilifu lizingatiwe kama nguzo kuu kwani katika Uislamu uadilifu ni kipambanuzi cha haki na batili ni ndicho kigezo cha uhalali na uharamu wa serikali.
Huku akigusia nukta nyingine ya dharura katika kubuni, kuchora na kuandaa Kigezo cha Maendeleo cha Kiislamu - Kiirani, Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria juu ya mtazamo usio wa kimaada wa uchumi na kukumbusha kuwa, Uislamu unalipa umuhimu suala la kuwa na utajiri na unawataka Waislamu wazalishe utajiri lakini kwa sharti kwamba utajiri huo usipatikane wala kutumika katika masuala ya ufisadi, ubeberu na israfu.
Katika sehemu ya mwisho ya miongozo yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza tena juu ya udharura wa kuendelea silisila ya vikao na mikutano kama hiyo ya fikra za kiistratijia na kuongeza kuwa, katika kubuni Kigezo cha Maendeleo cha Kiislamu - Kiirani kunaweza kukahitajia kufanyika makumi ya mikutano na vikao na kubuni na kuanzisha makumi ya duru za kielimu na kifikra katika Vyuo Vikuu na Hawza lakini kiujumla jambo lililo muhimu ni kuwa harakati hii imeanza na inabidi suhula na fursa zote za watu wenye vipaji nchini zitumike kuendeleza suala hilo ili Inshaallah harakati hii iweze kufika kwenye nukta inayotakiwa.
Vile vile ameashiria kuwa, kubuniwa Kigezo cha Maendeleo cha Kiislamu - Kiirani kutokana na kuwa kwake ni kigezo kilicho juu kabisa hakukuyumkinika kufanywa na Serikali na wala Bunge. Pia amesema ni jambo la dharura kuanzisha taasisi maalumu ya kufuatilia lengo hilo la kiistratijia. Ameongeza kuwa, tab'an kazi hii muhimu mno na harakati hii adhimu haiwezi kujifunga kati ya majimui moja tu ya watu bali ni jambo linalopaswa kuwahusisha wanafikra, wasomi na wataalamu wote nchini.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, uundaji wa taasisi na chombo cha kufuatilia kazi hiyo inabidi urahisishwe kwa kuwaunga mkono na kuwasaidia watu wenye vipaji na wanafikra ili iwezekane kufikia malengo muhimu mno ya kubuniwa na kuundwa Kigezo cha Maendeleo cha Kiislamu - Kiirani.

Hotuba na Makala za Wanafikra
Mwanzoni mwa mkutano huo wa fikra za kiistratijia ambao maudhui yake ilikuwa ni Kigezo cha Maendeleo cha Kiislamu - Kiirani, Dk. Mas'ud Derakhsan, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Allama Tabatabai cha mjini Tehran ndiye aliyeanza kutoa fikra na mitazamo yake.
Makala yake ilikuwa na anwani isemayo: "Kuangalia Misingi ya Maendeleo ya Kiuchumi ya Kiislamu - Kiirani" na amesema kuwa, Kigezo cha Maendeleo cha Kiislamu - Kiirani sambamba na kutakiwa kushikamana vilivyo na misingi ya mafundisho ya Mwenyezi Mungu na sheria za Kiislamu, kinatakiwa kutilia maanani pia sifa uliyo nayo uchumi wa Kiirani ambao una historia ya nusu karne ya kutegemea mapato yatokanayo na mafuta.
Dk. Derakhsan ameongeza kuwa, maendeleo ya kweli ni yale yatokayo ndani ya jamii na kwamba jambo hilo linahitajia kuweko nia ya kweli ya taifa zima, ya watu wa kawaida na viongozi wa asasi zote za kiserikali na zisizo za kiserikali sambamba na kutumiwa vizuri uwezo wa ndani ya nchi.
Mtu wa pili aliyetoa hotuba yake katika mkutano huo ni Dk. Mustafa Salimifar, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Firdousi cha Mashhad. Msomi huyo ameanza kwa kujadili mwenendo wa mabadiliko ya kifikra na kinadharia ya suala zima la ustawi katika karne za hivi karibuni na kuongeza kuwa, kuna aina na modeli mbali mbali za ustawi zimetolewa duniani lakini zote zimeshindwa kudhamini malengo hasa ya jamii za mwanaadamu kutokana na mitindo yote hiyo ya ustawi kutotegemea fikra za kidini na mafundisho ya Mwenyezi Mungu na kutegemea tu fikra ya humanism ( yaani utaratibu wa fikra ambao unaichukulia dhana ya utu na ubinadamu kama ndio msingi na lengo lake kuu. Dhana hiyo inawataka watu wajitenge na wajiweke mbali na Mwenyezi Mungu, Muumba wao, na washughulike na maisha na utu wao tu. Kamusi ya Kiingereza iitwayo Common Dictionary inaliainisha neno "humanism" kuwa ni mfumo wa itikadi uliojengwa juu ya msingi wa maadili, sifa na tabia ambazo zinaaminika kuwa bora zaidi kwa vigezo vya binadamu wenyewe bila kutegemea muongozo wowote kutoka kwa Mwenyezi Mungu). Pia amesema, mbali na kuweko tofauti kubwa za kiaidiolojia katika ya mitindo hiyo ya ustawi ya Magharibi na vile unavyotaka Uislamu, jiografia ya maendeleo ya Iran nayo inatofautiana kabisa na modeli hizo za ustawi na kwamba ni jambo la dharura kuchorwa na kubuniwa Kigezo cha Maendeleo cha Kiislamu - Kiirani.
Hujjatul Islam Walmuslimin, Dk. Sayyid Husain Mir Ma'azi mmoja wa watafiti wa masuala ya kiutamaduni na fikra za Kiislamu naye amesema katika mkutano huo kwamba, istilahi ya "Kigezo cha Maendeleo ya Kiislamu - Kiirani inaonyesha kuweko udharura wa kuhakikisha kuwa, Kigezo cha Maendeleo ya Kiislamu kinatabikiana na kuoana kikamilifu na hali na sifa maalumu ya kiutamadunia, kijamii, kisiasa na kiuchumi ya Iran.
Dk. Mir Ma'azi pia amesema, kukusanywa pamoja hazina zilizopo za kielimu, kubuniwa na kufanyika duru za masomo ya shahada za uzamifu na fauka ya uzamifu ya masomo ya utafiti pamoja na kuundwa makundi ya utafiti wa falsafa ya Humaniora ya Kiislamu yaani somo la Sayansi ya Jamii (humanities) akisema kuwa, kufanya hivyo kunaweza kuandaa mazingira na uwanja bora kabisa wa kuweza kubuniwa na kutungwa Kigezo cha Maendeleo cha Kiislamu - Kiirani.
Dk. Zahra Nasrullahi, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Yazd naye ametoa hotuba katika mkutano huo wa fikra za kiistratijia na huku akitilia mkazo udharua wa kuweko Kigezo cha Maendeleo cha Kiislamu - Kiirani amesema kwamba, takriban mitindo na modeli zote za ustawi zilizobuniwa na Magharibi zimejaribiwa nchini Iran lakini zimeshindwa kuzaa matunda yanayotakiwa.
Bi Zahra Nasrullahi ameongeza kuwa, masuala kama vile kuifanya dhahiri ya Uislamu kuwa asili, kutokuweko miundombinu makini, kukosekana welewa wa kutosha kuhusu Magharibi, Uislamu na Iran, kufuata mkumbo kila yanapotokea mabadiliko, kukosekana sifa kamili ya kujiamini katika jamii ya kielimu nchini, kutokuweko mnyambuliko unaotakiwa na kutopewa uzito wa hali ya juu suala la kukabiliana na michuano ya kielimu kimataifa ni katika vizuizi vikuu vya kuweza kupatikana kigezo sahihi cha maendeleo.
Msomi mwingine aliyezungumza katika mkutano huo ni Hujjatul Islam Walmuslimin, Dk. Hamid Parsaniya ambaye sambamba na kuwasilisha makala amesema kuna udharura wa kuangaliwa upya muundo wa ustawi wa kisasa kwa kuzingatia misingi ya kinadharia na nyuga zake za kijamii na kihistoria.
Dk. Imad Ufrugh kutoka Chuo Kikuu cha Tarbiyat Modarris cha Tehran amesema katika mkutano huo pamoja na mambo mengine kwamba ni jambo muhimu na la dharura kuelewa maana halisi ya utandawazi na ameongeza kuwa, kutokana na mikinzano yake mingi ya ndani, mfumo wa kibepari hauwezi kuwa mfumo wa kimataifa na unaonekana ni wa kimataifa kutokana na kutumia mabavu tu lakini Uislamu unao uwezo wa kuwa na sifa hiyo ya kimataifa kwa sharti tu wasomi na mataifa ya Kiislamu yaweze kuzingatia vilivyo masuala ya uhakika na mahitaji ya kimataifa.
Naye Ayatullah Muhammad Mehdi Asefi, Mhadhiri katika Hawza za Najaf na Qum amesisitiza katika mkutano huo kwamba Kigezo cha maendeleo ya Magharibi si kigezo kinachoweza kufuatwa na jamii ya Kiislamu. Amesema, katika kubuni Kigezo cha Maendeleo cha Kiislamu - Kiirani inabidi ibainishwe wazi kwamba je kwa mtazamo wa Kiislamu maendeleo ni lengo au ni natija na matokeo? Amesisitiza kuwa, msingi na nguzo kuu ya maendeleo ni kunyanyua uwezo wa kielimu wa Vyuo Vikuu.
Kwa upande wake, Dk. Sayyid Habibullah Tabatabai, Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Allama Tabatabai amesema, kufanyika tathmini sahihi ya nchi nzima ni jambo la lazima na kuongeza kuwa, suala la kufanyika tathmini sahihi ya mara kwa mara ya nchi nzima kutapelekea kurekebishwa nukta dhaifu na kuimarishwa nukta zenye nguvu katika suala hilo zima.
Ayatullah Haeri Shirazi naye ni miongoni mwa wasomi waliohutubia katika mkutano huo wa fikra za kiistratijia ambaye pamoja na mambo mengine amesisitiza sana juu ya haja ya kutambua na kuelewa vizuri kanuni za maumbile kama njia ya kuandaa mazingira bora ya kupatikana maendeleo ya kweli.
Bibi Alasvand Mhadhiri wa Hawza na Chuo Kikuu ndiye aliyekuwa shakhsia wa mwisho aliyetoa hotuba kabla ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwenye mkutano huo wa Tehran na huku akisisitiza kuhusu wajibu wa kuzingatiwa familia katika maendeleo ya nchi, amesema, mtazamo wa kiistratijia wa Uislamu unayapa kipaumbele maendeleo yaliyojengeka juu ya umaanawi ambayo yanatilia mkazo sana masuala ya utamaduni sahihi. Amesema, inabidi kuwa macho na kuhakikisha neno maslahi kwa maana ya Uislamu halitumiki kwenye usekula na kupinga dini na inabidi pia kuwa na tahadhari sana ili tuweze kujiepushe kivitendo na miundo ya maendeleo ya Kimagharibi.
Mwanzoni kabisa mwa mkutano huo, Dk Vaiz Zadeh, Katibu wa Mkutano wa Fikra za Kiistratijia amebainisha namna mikutano kama hiyo inavyoweza kufanyika na kuongeza kuwa, fikra ya kwanza kabisa ya kufanyika mikutano kama hiyo ilitoka kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu karibu miezi 10 iliyopita na kwamba baada ya kuundwa sekretarieti na kufanyika mashauriano ya kina kati ya wasomi, wahadhiri, wanafikra na wananadharia wenye uzoefu, iliamuliwa kufanyika mkutano wa kwanza katika ya silisila za mikutano ya kiistratijia ya Kigezo cha Maendeleo cha Kiislamu - Kiirani.
Huku akizungumzia udharura wa kushirikishwa wanafikra na wananadharia pamoja na wasomi na wahadhiri wote katika kufanikisha suala hilo muhimu amesema, mbali na upande wa kinadharia, vikao vya kiistratijia vinatumika pia kuchunguza njia za kutekeleza kivitendo nadharia zinazotolewa.
www.khamenei.ir
705770



captcha