IQNA

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu asema Umoja wa Kiislamu unapaswa kuimarishwa zaidi

12:39 - December 21, 2010
Habari ID: 2050707
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Qatar ni mzuri na kuongeza kuwa uhusiano huo unapaswa kupanuliwa zaidi kwa maslahi ya pande mbili na eneo zima kwa ujumla.
Ayatullahil Udhma Ali Khamenei ameyasema hayo leo katika mazungumzo yake na Amir wa Qatar Sheikh Hamad bin Khalifa Al Thani. Ameashiria umuhimu wa amani na usalama katika Mashariki ya Kati hususan Ghuba ya Uajemi na akasema kuwa amani ya eneo la Ghuba ya Uajemi inafungamana na haiwezi kutenganishwa kwani iwapo eneo hili litakuwa na amani, nchi zote za eneo zitafaidika na suala hilo, lakini iwapo awani hiyo itatiwa dosari nchi zote za eneo hilo zitakosa amani na kupata madhara.
Ayatullahil Udhma Khamenei amezilaumu baadhi ya nchi za eneo hili ambazo hazitilii maanani umuhimu mkubwa wa kuwepo amani katika eneo la Ghuba ya Uajemi na akasema, inasikitisha kwamba Wamarekani na Wazayuni wanasisitiza zaidi fikra hiyo katika nchi hizo na kuzidisha hali ya kupuuzwa umuhimu wa amani na usalama wa eneo hili.
Amelitaja suala la umoja kati ya Waislamu wa Shia na Suni kuwa lina umuhimu mkubwa na kusema: "Mashia na Masuni wa eneo hili wamekuwa wakiishi kwa amani na upendo kwa miaka mingi lakini baadhi ya watu wanafaya njama za kuvuruga hali hiyo na wengine wamezibadili hitilafu za kiitikadi za Shia na Suni na kuzifanya hitilafu za kijamii.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa inasikitisha kwamba kuna watu wenye taasubi, chuki za kimadhehebu na vibaraka katika pande zote mbili, suala ambalo linapaswa kudhibitiwa katika upande wa kiitikadi na kiusalama.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia matamshi ya Amir wa Qatar kuhusu hali tete ya Lebanon na uwezekano wa kutolewa hukumu ya mahakama inayoshughulikia kesi ya waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo Rafiq al Hariri na akasema mahakama hiyo ni ya kimaonyesho tu na maamuzi yake yote hayawezi kukubalika.
Kwa upande wake Amiri wa Qatar Sheikh Hamad bin Khalifa Ali Thani amesema katika kikao hicho ambacho pia kimehudhuriwa na Rais Ahmadijenad kwamba misimamo ya kisiasa ya nchi hizo mbili inakurubiana mno na kwamba anatarajia kuwa uhusiano wa Tehran na Doha utaimarishwa zaidi katika nyanja nyingine.
Amesema kuwa suala la usalama wa eneo la Ghuba ya Uajemi na umoja kati ya Shia na Suni vina umuhimu mkubwa. Ameashiria hali ya Lebanon na akasema: “Baadhi ya watu wanataka kuzusha fitina mpya nchini humo lakini sisi tunafanya jitihada kwa kushirikiana na nchi za eneo hilo ili kuzuia fitina hizo kwa mujibu wa maslahi ya eneo zima.”
715414
http://www.leader.ir/
captcha