Kushiriki wanawake katika Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Wanachuo Waislamu yaliyopangwa kufanyika nchini Iran na kuanzishwa vitengo vipya kama vile ufahamu wa Qur'ani, adhana na qaswida ni mambo yatakayoiunua kiwango cha mashindano.
Hayo yamesemwa na Muntahaa Ibrahim Kenny, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Qur'ani ya Afrika Kusini ambaye pia amewapongeza viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa juhudi zao za kustawisha shughuli za Qur'ani kitaifa na kimataifa.
Ameongeza kuwa: ‘Umuhimu ambao viongozi wa Iran wameonyesha umezaa matunda kwani hivi sasa taifa la Iran ni mfano wa kuigwa na linaishi kwa msingi wa Qur'ani Tukufu. Kama alivyosema Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Khamenei, Qur'ani ndio msingi wa mafanikio ya Mapinduzi ya Kiislamu. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na watu wake wameshika nafasi ya kwanza katika utekelezaji wa mafundisho ya Qur'ani katika dunia iliyogubikwa na uovu na kiza”.
Kijana huyo Muislamu kutoka Afrika Kusini amesema Mashindano ya Tatu ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Wanachuo Waislamu ni hatua muhimu katika kuimarisha umoja wa umma wa Kiislamu chini ya mwavuli Qur'ani.
Mashindano ya Tatu ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Wanachuo Waislamu yatafanyika kuanzia Januari 9-11 katika mji mtakatifu wa Mash'had kaskazini mashariki mwa Iran ambapo nchi 40 zitashiriki.
716281