IQNA

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu: Wamisri na Watunisia wanataka Uislamu, Uhuru

19:41 - February 04, 2011
Habari ID: 2074969
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kutaka Uislamu na uhuru ndio motisha muhimu zaidi kwa watu wa Misri , Tunisia na eneo.
Ayatullahil Udhma Sayyed Ali Khamenei ameyasema hayo katika hotuba za sala ya Ijumaa mjini Tehran ambapo amebainisha misingi ya matukio katika nchi za kieneo zikiwemo Misri na Tunisia. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa pamoja na kuwepo matatizo ya kiuchumi, sababu kuu ya mwamko wa wananchi wa Misri na Tunisia ni kuwa wamehisi kwamba wamedhalilishwa na tabia za viongozi wao.
Kuhusu matukio ya Tunisia, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria namna mtawala aliyetumuliwa wa nchi hiyo, Ben Ali, alivyokuwa tegemezi kwa Marekani na shirika la kijasusi la CIA. Aidha amekumbusha namna utawala wa Ben Ali ulivyokuwa na chuki dhidi ya Uislamu na kuongeza kuwa Watunisia hawangevumilia kuwa na kiongozi aliye kibaraka rasmi wa Marekani na ambaye kwa miaka mingi alienda kinyume na maslahi ya wananchi ikiwa ni pamoja na dini yao. Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuwa mabadiliko ya Tunisia ni ya juu na kuelezea matumaini yake kuwa, kutokana na uangalifu na mwamko wa wananchi, nchi hiyo itashuhudia mabadiliko ya kimsingi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia ameashiria mwamko wa watu wa Misri na historia ya nchi hiyo katika kupigania Uislamu, kusimama kidete mbele ya utamaduni wa Kimagharibi na vile vile kupambana dhidi ya utawala wa Kizayuni. Amesema pamoja na hayo, katika kipindi cha miaka 30 iliyopita Husni Mubarak amelidhalilisha taifa kubwa la Misri kwani amekuwa adui wa uhuru wa wananchi na ameendelea kuwa mshirika na mtumwa wa Wazayuni. Kiongozi Muadhamu amesema Misri ni nchi ambayo ilikuwa ilhamu kwa nchi za Kiarabu kutokana na mapambano yake dhidi ya Wazayuni lakini kwamba katika kipindi cha Mubarak imelidhulumu taifa la Palestina na kushirikiana na Israel katika kuuzingira Ukanda wa Ghaza.
Ayatullahil Udhma Sayyed Ali Khamenei amesisitiza kuhusu nara na kaulimbiu zenye misingi ya kidini na Kiislamu za taifa la Misri katika matukio ya hivi karibuni na kusema kuwa: ‘Katika hali hii Marekani na Israel zimepigwa na butwaa kutokana na kuwa ushindi wa taifa la Misri ni pigo kubwa kwa sera za Marekani katika eneo.'
captcha