IQNA

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Umewadia wakati wa kukomeshwa tawala za kibeberu

8:55 - February 09, 2011
Habari ID: 2078097
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Khamenei amesema kuwa harakati kubwa ya mataifa katika baadhi ya nchi na mwamko wa Kiislamu katika Mashariki ya Kati vimeathiriwa na harakati kubwa ya Kiislamu ya taifa la Iran katika kipindi chote cha miaka 32 iliyopita. Amesema sasa umewadia wakati wa kutoweka taratibu kipindi cha tawala za kibeberu na kiukandamizaji.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei ambaye jana alihutubia mkusanyiko mkubwa wa makamanda na maafisa wa Jeshi la Anga la Jamhuri ya Kiislamu akisema kuwa kusimama kidete kwa taifa la Iran katika misingi na thamani hususan za Kiislamu ndiyo sababu ya kubakia hai Jamhuri ya Kiislamu na kuwa kigezo cha kuigwa na mataifa mengine. Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa harakati kubwa ya mataifa katika baadhi ya nchi na mwamko wa Kiislamu katika Mashariki ya Kati vimeathiriwa na harakati kubwa ya Kiislamu ya taifa la Iran katika kipindi chote cha miaka 32 iliyopita. Amesema sasa umewadia wakati wa kutoweka taratibu kipindi cha tawala za kibeberu na kiukandamizaji.
Katika hadhara hiyo iliyokusanyika kwa mnsaba wa kuadhimisha tukio la kihistoria wakati makamanda wa Jeshi la Anga walipojiunga na harakati ya Mapinduzi ya Kiislamu na kumpa Imam Khomeini mkono wa utiifu hapo tarehe 8 Februari 1979, Amiri Jeshi wa majeshi ya Iran amesema kuwa harakati hiyo itakayobakia hai na ya kishujaa, ilitayarisha uwanja mzuri wa matukio mawili muhimu. Ameongeza kuwa moja ya matunda ya hatua hiyo ya makamanda wa Jeshi la Anga ilikuwa ni kuarifisha utambulisho mpya wa jeshi na kuainisha utambulisho wa jeshi la Jamhuri ya Kiislamu hapo tarehe 8 Februari 1979.
Amesema kuwa matunda mengine ya hatua hiyo ya kihistoria yalikuwa kuasisi harakati imara. Amesema hapana shaka kuwa tukio la tarehe 8 Februari 1979 lililotokea mbele ya Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu) lilitia ari katika harakati mpya ya taifa la Iran na kuwa na taathira kubwa katika tukio kubwa la tarehe 11 Februari 1979.
Amiri Jeshi wa majeshi yote ya Iran amesema makamanda wa Jeshi la Anga la Iran walitayarisha uwanja wa kukombolewa nchi katika hatua yao ya tarehe 8 Februari 1979 na kuongeza kuwa nchi kubwa ya Iran yenye historia na utamaduni wa muda mrefu na uwezo mkubwa ilitekwa na kudhalilishwa na madola ya kidhalimu kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu, lakini harakati ya wananchi hapo tarehe 11 Februari na ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu vilivunja jinamizi hilo.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema sifa muhimu zaidi ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran baada ya kupita miaka 32 sasa ni kusimama kidete na kushikamana barabara na misingi na thamani. Amesisitiza kuwa thamani muhimu zaidi ya mapinduzi hayo ni Uislamu ambao daima unapaswa kulindwa na kutiliwa mkazo, kwani mambo kama kujitawala, uhuru, maendeleo ya kimaada, umoja wa kitaifa na kuchanua vipawa yote yanawezekana chini ya kivuli cha Uislamu.
Ayatullah Khamenei amekumbusha sisitizo la mara kwa mara la Imam Khomeini juu ya umuhimu wa Jamhuri ya Kiislamu na kusema: "’Jamhuri’ ina maana ya kutegemea wananchi, na ni muhali kuwapo utawala wa Kiislamu bila ya wananchi kuwa na imani na utawala huo; kwa msingi huo Jamhuri ya Kiislamu ndiyo msingi na nguzo katika mapinduzi ambayo inapaswa kulindwa."
Amiri Jeshi wa majeshi ya Iran amesema sharti la kupata mafanikio katika nyanja mbalimbali ni kujikurubisha zaidi katika maana halisi na ya kina ya Jamhuri ya Kiislamu. Ameongeza kuwa kunahitajika hima kubwa na kazi mara dufu ili kuweza kufikia kwenye Jamhuri ya Kiislamu na utawala halisi wa Kiislamu, na kwa kuzingatia jina la mwaka huu, taathira za hima kubwa zinaonekana katika kazi na hatua za viongozi.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa kuasisiwa utawala wa Jamhuri ya Kiislamu iliyopiga hatua katika nyanja za kimaada na kiroho hapa nchini kumetayarisha uwanja mzuri wa taifa la Iran kuwa kigezo cha kuigwa na kusema, katika kipindi cha miaka 32 iliyopita taifa la Iran limekuwa kigezo kwa mataifa mbalimbali kutokana na istiqama na kusimama imara kwenye Uislamu na utawala wa Kiislamu na maendeleo yake makubwa yaliyopatikana katika fremu hiyo.
Akiashiria harakati kubwa za mataifa mbalimbali zinazoshuhudiwa hivi sasa katika baadhi ya nchi, Ayatullah Ali Khamenei amesema harakati hizo hazitokei kwa sadfa na ghafla bali ni matokeo ya rundo la matakwa ya muda mrefu ambayo yanadhihiri sasa. Amesema, hapana shaka kwamba kusimama kidete kwa taifa la Iran kumechangia mno katika kutokea harakati hizo.
Amesema kuwa hii leo mataifa ya Mashariki ya Kati na ulimwengu wa Kiislamu yameamka na umewadia wakati wa kutoweka taratibu madola ya kibeberu na ya kiukandamizaji.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema taifa la Iran daima limekuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na mabeberu na madhalimu na kwamba fahari hiyo imechanganyika na fikra na roho za taifa la Iran kutokana na baraka za utamaduni wa Iran na dini ya Uislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia juu ya udharura wa kutiliwa maanani nafasi muhimu ya taifa la Iran na ulazima wa kudumishwa mwenendo wa ustawi na maendeleo na akasema kuwa katika njia hiyo tunapaswa kujiepusha na jambo lolote linalokwamisha harakati na maendeleo. Ameongeza kuwa moja ya vizuizi hivyo ni kupuuza thamani; kwa msingi huo kuna udharura wa kusisitizwa na kutiliwa mkazo daima juu ya thamani za mapinduzi na Uislamu.
Ayatullah Khamenei amesema moja ya vizuizi vya harakati ya maendeleo na malengo makuu ya adui katika vita laini (vita vya kipropaganda) ni njama za kuzusha ufa na migawanyiko katika safu za taifa la Iran na viongozi wake. Ameongeza kuwa kuzusha hitilafu na migawanyiko kati ya wananchi, viongozi na sehemu mbalimbali za utawala wa Kiislamu na vilevile kati ya utawala wa Kiislamu na wananchi ni miongoni mwa malengo makuu ya adui kwa ajili ya kuvuruga uwiano na mshikamano uliopo hapa nchini, suala ambalo linapaswa kupigwa vita kwa njia zote. Amesisitiza kuwa njia pekee ya kupambana na jambo hilo ni kulinda na kupanua maarifa na uwezo wa kuona mbali na pia kutilia maanani umuhimu na nafasi nyeti ya sasa ya taifa la Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa nafasi yenye taathira kubwa ya taifa la Iran inapaswa kulindwa kwa kuona mbali na kujiepusha na hitilafu.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Khamenei amepongeza maendeleo na mafanikio ya Jeshi la Anga katika sekta za utengenezaji vipuri, zana za kijeshi, mafunzo na uratibu na akasema kuwa harakati hiyo inapaswa kukamilishwa bila ya kusimama wala kutosheka na kiwango maalumu.
Amesema sharti la kudumishwa harakati hiyo ni kutegemea imani, hima na vijana na akaongeza kuwa kumtegemea Mwenyezi Mungu, kuegamia nguvu, fikra, ubunifu na kujiamini kwa vijana hufanya muujiza katika sekta zote.
Mwishoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa baadhi ya nakisi zilizopo hazipaswi kukwamisha harakati na maendeleo bali kuna ulazima wa kushinda nakisi hizo kwa kutilia maanani hali na suhula za wakati huo.
Brigedia Jenerali Shah Safavi Kamanda wa jeshi la Anga la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alihutubia pia mkusanyiko huo akikumbusha harakati ya kihistoria ya makamanda wa Jeshi la Anga hapo tarehe 8 Februari 1979 na kusema hatua hiyo ya kishujaa ilikuwa ishara ya uaminifu wa kikosi cha anga kwa Faqihi Mtawala. Amesisitiza kuwa makamanda na wafanyakazi wa kikosi cha Jeshi la Anga wametetea na kulinda Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kwa maarifa na imani katika vipindi mbalimbali ikiwa ni pamoja na wakati wa vita vya kujitetea kutakatifu. Amezungumzia pia mafanikio ya kikosi hicho katika kutengeneza zana mbalimbali za kijeshi. 744529
captcha