IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amwambia Rais wa Uturuki:

Kujitenga na utawala wa Kizayuni kumeikurubisha Uturuki kwa umma wa Kiislamu

20:48 - February 15, 2011
Habari ID: 2081641
Ayatullah Khamenei amesema kuwa nafasi ya sasa ya Uturuki katika ulimwengu wa Kiislamu inatofautiana sana na ile ya miaka ya huko nyuma. Ameongeza kuwa siasa huru za Uturuiki mkabala wa Magharibi, kujitenga na utawala wa Kizayuni wa Israel na kuwatetea wananchi wa Palestina ni miongoni ma masuala muhimu yaliyoikurubisha Uturuki kwa umma wa Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei mapema leo amemkaribisha ofisini kwake Rais Abdullah Gul wa Uturuki na ujumbe anaoandamana nao na kusema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Uturuki ni nchi mbili za Kiislamu marafiki na ndugu. Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa uhusiano wa sasa wa Iran na Uturuki katika nyanja za kisiasa na kiuchumi ni wa aina yake ikilinganishwa na kipindi cha miaka mingi iliyopita na kuna udharura wa kutumiwa fursa hii ya kihistoria kwa ajili ya kustafidi na uwezo mkubwa wa nchi hizi mbili.
Ameashiria azma ya Iran na Uturuki ya kuzidisha mara tatu kiwango cha mabadilishano yao ya kibiashara na kusema Tehran inaamini kwamba nchi jirani zinaweza kuendeleza pamoja ushirikiano wao wa kisiasa na kiuchumi ili ziweze kuwa na taathira kubwa zaidi.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa nafasi ya sasa ya Uturuki katika ulimwengu wa Kiislamu inatofautiana sana na ile ya miaka ya huko nyuma. Ameongeza kuwa siasa huru za Uturuiki mkabala wa Magharibi, kujitenga na utawala wa Kizayuni wa Israel na kuwatetea wananchi wa Palestina ni miongoni ma masuala muhimu yaliyoikurubisha Uturuki kwa umma wa Kiislamu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa siasa hizo ni siasa sahihi na kadiri Uturuki inavyojikurubisha zaidi kwa ulimwengu mkubwa wa Kiislamu, ndivyo inavyopata faida na kunufaisha pia ulimwengu wa Kiislamu.
Akiashiria suala la kukurubiana mitazamo ya Iran na Uturuki kuhusu masuala ya kieneo hususan kadhia ya Afghanistan, Iraq, Lebanon na Palestina, Ayatullah Khamenei amesema mabadiliko ya hivi karibuni nchini Misri ni miongoni mwa masuala muhimu mno ambayo yanaweza kuwa na kheri kwa wananchi wa Misri na Mashariki ya Kati kwa ujumla.
Amesema kuwa udhibiti wa miongo kadhaa wa Marekani na utawala ghasibu wa Israel huko Misri na kudhalilishwa wananchi wa nchi hiyo ndiyo sababu kuu ya harakati ya mabadiliko ya wananchi. Ameongeza kuwa wananchi wa Misri ni Waislamu wenye ari na misimamo madhubuti ya Kiislamu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa wakati wananchi wanapojitosa katika medani hali ya mambo hubadilika na nyenzo za kawaida za kisiasa na kijeshi huwa butu. Amesisitiza kuwa wananchi wa Misri sasa wako katika medani.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa Wamarekani wanataka kuteka harakati kubwa ya wananchi wa Misri na kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapinga uingiliaji wa nchi za kigeni huko Misri na inaamini kwamba wananchi ndio wanaopaswa kujichukulia maamuzi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa maudhui muhimu zaidi katika dunia ya Kiislamu ni kulinda na kuimarisha umoja wa umma wa Kiislamu na kuepuka mtego wa wageni wanaotaka kuzusha hitilafu na migawanyiko. Ameongeza kuwa iwapo ulimwengu wa Kiislamu utatambua vyema uwezo na suhula zake kubwa, basi hali ya mambo itabadilika sana na ulimwengu wa Kiislamu unaweza kuwa nguvu yenye taathira kubwa katika masuala ya kimataifa.
Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa serikali ya Uingereza ndiyo sababu kubwa zaidi inayozusha hitilafu kati ya Waislamu. Huku akitilia mkazo kwamba siasa na mipango yote ya nchi za Kiislamu inapasa kuwa katika mkondo wa kujenga na kuzidisha uwezo wa ulimwengu wa Kiislamu, Ayatullah Khamenei amesema: "Nchi za Magharibi daima zimekuwa zikiudhalilisha ulimwengu wa Kiislamu, na nchi au taifa lolote linalotaka kupambana na udhalilishaji huo na kudhihirisha uwezo wake hukabiliwa na upinzani na vizingiti vya Magharibi."
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbusha ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kuwanusuru Waislamu na akasema iwapo tutatazama vyema hali ya sasa ya Mashariki ya Kati na ya madola ya kibeberu na kulinganisha na hali ya huko nyuma, tutaona kikamilifu ishara za msaada wa Mwenyezi Mungu.
Amesema kuwa miaka 30 iliyopita Marekani na nchi zenye majingambo mengi za Magharibi zililifanya eneo la Mashariki ya Kati kuwa medani yao lakini sasa nchi hizo zina hali gani? Je, hali ya sasa ya utawala wa Kizayuni wa Israel iko je ikilinganishwa na hali ya utawala huo ghasibu miaka 30 iliyopita? Hebu linganisha Iran ya sasa na ile ya miaka 30 iliyopia. Tazama tofauti ya Uturuki ya leo na Uturuki ya miaka 30 iliyopita. Tazama tofauti kubwa iliyopo kati ya Iraq na Palestina ya sasa na Iraq na Palestina ya miaka ya huko nyuma. Ayatullah Khamenei amemalizia kwa kusema: "Hayo yote ni ishara za msaada wa Mwenyezi Mungu, na hali hiyo itasonga mbele kwa kasi kubwa zaidi."
Katika kikao hicho Rais Abdullah Gul wa Uturuki ameelezea kufurahishwa na kukutana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusema kuwa uhusiano wa Uturuki na Iran ni wa miaka mingi na wa kihistoria. Rais Gul amesema katika kikao hicho ambacho pia kimehudhuriwa na Rais Mahmoud Ahmadinejad kwamba mazungumzo yake na mwenyeji wake yamekuwa na mafanikio na kwamba anatarajia kuwa ushirikiano wa pande hizo mbili katika nyanja mbalimbali hususan katika sekta ya watu binafasi, utatayarisha uwanja nzuri wa kufanyika kazi kubwa zaidi.
Rais wa Uturuki ameashiria pia hali ya hivi sasa katika Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika na akasema ushahidi unaonyesha kuwa hali ya mambo katika eneo hilo inabadilika na kuna matarajio kwamba mabadiliko hayo yatawanufaisha wananchi na nchi zote za eneo hilo.
Vilevile ametilia mkazo juu ya udharura wa kulindwa umoja wa nchi za Kiislamu. 748410
captcha