IQNA

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu asema mwamko wa Kiislamu unaimarika

10:15 - February 17, 2011
Habari ID: 2082257
Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Jumatano, Februari 16, 2011, alionana na kundi la maelfu ya wananchi wa Azarbaijan (kaskazini magharibi mwa Iran) na huku akiashiria harakati inayozidi kustawi ya mwamko wa Kiislamu katika ulimwengu wa Kiislamu amesema kuwa harakati hiyo ni matunda matamu ya muqawamah na kusimama kidete taifa adhimu la Iran katika kipindi cha miaka 33 iliyopita.
Amesisitiza kuwa, leo hii kutokana na baraka za imani na Uislamu, uimara, heshima na maendeleo sambamba na athari nzuri za Iran ya Kiislamu zinang'ara zaidi kuliko wakati mwingine wowote na kwamba azma ya nia thabiti ya taifa la Iran imezidi kuongezeka hivi sasa hadi taifa hilo litakapofikia vilele vya heshima na utukufu.
Mkutano huo umefanyika wakati wa kukaribia maadhimisho ya harakati ya kihistoria ya tarehe 29 Bahman 1356 (Februari 18, 1978) ya wananchi wa Tabriz.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amewapongeza wananchi wa Azarbaijan kutokana na imani yao, ikhlasi, kusimama kidete na muono wa mbali wa kupigiwa mfano katika kipindi chote cha historia hususan katika vipindi mbali mbali vya mapambano ya Kiislamu na vya Mapinduzi ya Kiislamu.
Ameongeza kuwa, moja ya sifa ya kipekee ya harakati ya wananchi wa Tabriz ya tarehe 29 Bahman (Februari 18) ni kuwa kwake kigezo cha harakati za baadaye za wananchi wa Iran na laiti kama harakati hiyo ya wananchi wa Tabriz ya tarehe 29 Bahman 1356 (Februari 18, 1978) isingelitokea, basi harakati ya wananchi wa Qum ya tarehe 19 Dey (Januari 9, 1978) mwaka huo ingelisahaulika na harakati ya wananchi wa Iran ya mwamko wa Kiislamu ingelikwama.
Ayatullahil Udhma Khamenei amelitaja suala la kuwa kigezo Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kuwa ni miongoni mwa sifa za kipekee za mapinduzi hayo na amekumbusha kuwa, sababu kuu inayowafanya maadui waishinikize sana Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tangu awali kabisa ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hadi hivi sasa ni kutokana na harakati adhimu ya wananchi wa Iran kuwa kigezo kwa mataifa mengine.
Ameashiria pia vikwazo vya kiuchumi, kuuliwa kigaidi wataalamu na wasomi wakubwa wa Iran na kuituhumu Iran kwa mambo mbali mbali yasiyo na msingi katika suala la haki za binaadamu.
Amesisitiza kuwa, mashinikizo na propaganda zote hizi mbaya zinafanywa kwa lengo la kutaka kuikwamisha harakati ya taifa la Iran na kutaka kuwafanya wananchi wa eneo na duniani kiujumla wajiweke mbali na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lakini kinyume kabisa na wanavyotaka mabeberu duniani, Iran ya Kiislamu siku baada ya siku inazidi kuwa na nguvu na kupiga hatua kubwa za kimaendeleo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, miaka minane ya vita vya kujihami kutakatifu kumepelekea kujitokeza vijana shupavu na mashujaa nchini Iran na kwamba vikwazo vya kiuchumi na kielimu navyo vimepelekea kuzidi kuchanua vipaji vya vijana wa taifa hili.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, sifa maalumu kabisa ya wananchi wa Azarbaijan na Tabriz ni hamasa na hisia zao nzuri sambamba na tabasuri na kuona kwao mbali. Amesisitiza kuwa, inabidi vijana wa hivi sasa na vizazi vijavyo navyo virithishwe sifa hizo maalumu ikiwa ni pamoja na muono wa mbali na uwezo mkubwa wa kuchanganua mambo ili hali iendelee hivi hivi kama ilivyoendelea katika kipindi cha miaka 33 iliyopita.
Amesisitiza kuwa, ijapokuwa vijana wa hivi sasa hawakumuona Imam Khomeini (quddisa sirruh) na mashahidi Bakiri na wala hawakuwepo wakati wa kipindi kigumu cha miaka minane ya vita vya kujihami kutakatifu, lakini fikra, utambuzi na njia ya vijana wa leo ni sawa sawa kabisa na fikra na njia ya miaka ya awali ya Mapinduzi ya Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya amesisitiza kwamba, kuwa na imani thabiti na muono wa mbali humfanya mtu kupata uhai mpya wenye kuzaa fikra bora moyoni.
Ameongeza kuwa, sifa hiyo inabidi iendelee kuwepo daima kama ambavyo imeendelea kuwepo na kutoa arhari nzuri katika maeneo mbali mbali ulimwenguni.
Ayatullahil Udhma Khamenei ameongeza kuwa, mwamko wa Kiislamu unaoshuhudiwa hivi sasa katika eneo umeathiriwa na harakati ya kiimani na azma ya kweli ya taifa la Iran. Amesisitiza kuwa, masuala muhimu sana ya Misri yanatokana na harakati ya mwamko wa Kiislamu na kudhalilishwa kwa miaka mingi wananchi wa nchi hiyo ambao wana utambuzi mpana, wana historia kongwe na wamestaarabika.
Amesema, harakati kubwa za kijamii si kitu kinachokuja ghafla bali huundika pole pole na huchukua miaka mingi kuundika kwake lakini wakati wake unapofika hujitokeza ghafla na mara moja. Ameongeza kuwa, udhalilishaji ambao umefanywa na utawala wa Misri kwa miaka mingi nyuma dhidi ya wananchi kutokana na utawala huo kuwa kibaraka wa Marekani na wa utawala wa Kizayuni hatimae umewafanya wananchi na vijana wa Misri wachoke kuvumilia, jambo ambalo limewapelekea wananchi hao waripuke ghafla moja na kufanya mapinduzi dhidi ya utawala huo kibaraka.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, vijana wa Misri walio na imani thabiti na wasiotetereka, wametoa mchango mkubwa katika kufanikisha harakati adhimu ya wananchi wa nchi hiyo na amekumbusha kuwa, harakati ya wananchi wa Misri ilianza kwa kujitokeza mbele vijana misikitini na kwenye sala za Ijumaa na hatimaye harakati hiyo ikaanza kuenea na kuwa ya wananchi wote.
Ayatullahil Udhma Khamenei ameongeza kuwa, kujitokeza kwa mamilioni wananchi katika harakati hiyo kulizivunja nguvu mbinu zote za kisiasa, kijeshi na kiuchumi za madola ya kibeberu na kwamba Wamarekani wanaweza kirahisi kuzishinikiza wanavyotaka tawala zisizo na uungaji mkono wa wananchi na wakati wote wanapoona viongozi wa tawala hizo hawana faida tena kwa mabeberu hao wanawatupa mara moja kama walivyofanya kwa Muhammad Reza Pahlavi (Mfalme wa Iran) na Ben Ali (Rais wa zamani wa Tunisia). Amesema, hata hivyo wakati wananchi wanapojitokeza kwa wingi kupambana na vibaraka hao Wamarekani wanashindwa kufanya chochote mbele ya misimamo imara ya wananchi.
Amesisitiza kuwa, hivi sasa kumetokea tukio muhimu sana nchini Misri, tab'an Marekani inafanya njama za kupotosha harakati ya wananchi wa Misri na kujaribu kuwakinaisha warejee majumbani na waachane na mapinduzi yao baada ya kupatikana baadhi tu ya mafanikio ya mapinduzi hayo, lakini ni jambo lililo mbali kudhani kwamba hila hizo zitaweza kuwasaidia Wamarekani hao mbele ya wananchi walioamka wa Misri na ambao wameona kwamba wanapoamua jambo basi wanaweza kulifanikisha.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, sababu kuu ya kupata heshima na maendeleo wananchi wa Iran ni imani yao kwa dini tukufu ya Kiislamu na amekumbusha kuwa, kujiimarisha kiimani, hima ya vijana na kufanya juhudi kwa ajili ya kufanikisha zaidi matunda ya Uislamu katika jamii ni mambo ambayo huandaa mazingira ya kupatikana heshima na maendeleo makubwa pamoja na kuyafanya bora maisha ya kimaada na kimaanawi ya wananchi.
Mwanzoni mwa mkutano huo, Ayatullah Mujtahid Shabestari, Mwakilishi wa Fakihi Mtawala ambaye pia ni Imamu wa Ijumaa wa Tabriz ametoa hotuba fupi na sambamba na kutoa pongezi kwa mnasaba wa maadhimisho ya hamasa ya tarehe 29 Bahman 1356 (Februari 18, 1978) ya wananchi wa Tabriz na nafasi kubwa ya wananchi wa Azarbaijan katika nyakati na vipindi tofauti vya Mapinduzi ya Kiislamu hususan harakati ya wananchi hao ya tarehe 8 Dey 1388 (Disemba 29, 2009) amesema kuwa, wananchi wa Azarbaijan hasa wa Tabriz siku zote wako macho na wamethibitisha kivitendo uungaji mkono wao mkubwa kwa Wilaya na Utawala wa Fakihi. Amekumbusha kuwa, katika maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka huu yaani Bahman 22 (Februari 11), wananchi hao walijiunga na wimbi kubwa la wananchi wenzao wa Iran na kushiriki vilivyo na kwa wingi mno katika maadhimisho hayo.
749146
captcha