IQNA

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Kuongoza vyema kipindi cha kihistoria cha sasa kutatatua matatizo ya ulimwengu wa Kiislamu

12:51 - February 21, 2011
Habari ID: 2084217
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei leo amezungumza na wageni na wanafikra wa Kiislamu wanaoshiriki katika Mkutano wa 24 wa Kimataifa wa Umoja baina ya Waislamu mjini Tehran akisema kuwa kipindi cha sasa katika ulimwengu wa Kiislamu ni kipindi nyeti na muhimu mno cha kihistoria.
Amesema kuwa kutambua vyema kipindi hiki muhimu, kuimarisha imani ya kidini ya wananchi, kulinda umoja, kutotishika na udhibiti wa Marekani na kuwa na dhana nzuri kwa ahadi ya nusra na msaada wa Mwenyezi Mungu vinatayarisha uwanja mzuri wa mafanikio na ushindi wa harakati kubwa ya mamilioni ya wananchi katika dunia ya Kiislamu.
Akibainisha hali ya sasa ya ulimwengu wa Kiislamu, Ayatullah Khamenei amesema sababu ya umuhimu wa kipindi cha kihistoria cha sasa imo katika ukweli kwamba iwapo kitaeleweka kwa njia sahihi na kuongozwa vyema, matatizo ya ulimwengu wa Kiislamu yatatatuliwa, na iwapo hakitaeleweka na kutumiwa vyema basi kitatayarisha uwanja wa kujitokeza matatizo mapya katika ulimwengu wa Kiislamu.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa mahudhurio ya mamilioni ya wananchi katika medani ya mapambano katika kipindi cha sasa kwenye ulimwengu wa Kiislamu hayana kifani. Amesema ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran pia ulitokana na mahudhurio makubwa ya wananchi na mahudhurio hayo ya mamilioni ya wananchi hayawezekani bila ya kuwepo imani ya kidini.
Amesema kuhudhuria wananchi katika medani mbalimbali hadi wakati wa kupatikana ushindi na kisha kulinda matokeo ya mahudhurio hayo ni mambo mawili muhimu sambamba na mahudhurio yenyewe ya wananchi. Ameongeza kuwa maadui wanafanya njama za kudhihirisha harakati za wananchi wa Misri, Tunisia na maeneo mengine ya ulimwengu wa Kiislamu kuwa si za Kiislamu ilhali hapana shaka kwamba harakati hizo za wananchi ni za Kiislamu na zinapaswa kutiwa nguvu zaidi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa Marekani ndio tatizo kuu la ulimwengu wa Kiislamu. Amesisitiza kuwa tatizo hilo linapaswa kuondolewa katika ulimwengu wa Kiislamu na kuidhoofisha Marekani. Ameongeza kuwa njia pekee ya kufikia hilo ni kuwa na matumaini kwa Mwenyezi Mungu na kuwa na dhana nzuri kwa ahadi yake ya kuwanusuru Waislamu.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa matukio ya zama za awali za Uislamu ni sawa na ubao wenye mchoro mgumu mno wa sanaa unaoakisi hali tofauti ya umma wa Kiislamu hadi zama hizi. Ameashiria hali ya Waislamu katika vita vya Ahzab na akasema: “Kama ambavyo katika vita vya Ahzab baadhi ya watu walitishika na nguvu za adui na wengine wakasimama kidete kupambana na adui huyo kwa kuwa na dhana nzuri kuhusu ahadi ya nusra na msaada wa Mwenyezi Mungu, hii leo pia wako watu waliotishika na udhibiti na nguvu za kijeshi, kidiplomasia, kipropaganda na misaada ya kifedha ya Marekani na wanaamini kwamba ni muhali kuweza kupambana na nchi hiyo; hata hivyo Mwenyezi Mungu Muweza ameahidi kuwasidia wanaonusuru dini yake.
Akiashiria kudhoofika Marekani ikilinganishwa na miaka ya huko nyuma, Kiongozi Muadhamu amesema matokeo ya kuwa na matumaini na ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kusimama kidete na kufanya harakati za kusonga mbele, na matokeo ya kukata matumaini na ahadi za Mwenyezi Mungu ni kutishika na kusalimu amri mbele ya adui.
Ayatullah Khamenei amesema mafanikio na ushindi mkubwa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi cha miaka 32 iliyopita ni matokeo ya kuwa na matumaini na ahadi ya nusra na msaada wa Mwenyezi Mungu. Amesisitiza kuwa mbali na kuvuka vikwazo vya kiuchumi na kushinda vita vya kulazimishwa vya miaka minane, taifa la Iran sasa limepata maendeleo makubwa katika medani za sayansi na teknolojia, na teknolojia ya nyuklia ni mfano wa maendeleo hayo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa maendeleo ya kisayansi ya Iran hususan katika medani ya teknolojia ya nyuklia yametokana na juhudi kubwa za kielimu za wasomi vijana, wenye imani na ikhlasi. Amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeweza kutatua suala la teknolojia ya nyuklia na kupiga hatua mbele katika medani hiyo licha ya mashinikizo mbalimbali.
Amesema makelele ya Wamagharibi kuhusu suala hilo hayana tena taathira yoyote kwani sasa wamebakia nyuma, na kupita kwa wakati kutaifaidisha zaidi Iran.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa tajiriba na uzoefu wenye mafanikio wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kwa ajili ya nchi zote za Kiislamu. Ameongeza kuwa sasa wananchi wa Misri wenye maarifa na historia inayong’ara ya Kiislamu wameingia katika medani na kuna udharura wa kuwa macho ili adui asipotoshe harakati yao na kupandikiza kibaraka mwenye mfungamano na utawala wa firauni wa Misri.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kazi ya kulinda harakati ya wananchi wa Misri katika daraja ya kwanza ni wadhifa wa wananchi, maulamaa, wanafikra na shakhsia wa Misri kisha umma nzima wa Kiislamu. Ameongeza kuwa moja ya taathira kubwa za umoja baina ya Waislamu ni hisi ya kuwajibika mataifa ya Kiislamu kuhusu masuala yanayuhusiana na Waislamu wenzao.
Ayatullah Khamenei amesema, kuzusha hitilafu kati ya Waislamu na mivutano ya Shia na Suni ni miongoni mwa njama za maadui ambazo tunapaswa kuzishinda. Amesema: “Harakati ya sasa katika ulimwengu wa Kiislamu itasonga mbele na sisi tuna imani na ahadi ya Mwenyezi Mungu na tuna matumaini kwamba Mwenyezi Mungu atawasaidia wanadamu wenye imani.”
Mwanzoni mwa mkutano huo Allamah Sheikh Ahmad al Khalili Mufti wa Oman, Ja’far Abdul Salam ambaye ni Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyuo Vikuu vya Ulimwengu wa Kiislamu, Waziri wa zamani wa Utamaduni wa Jordan Munir Shafiq, Kamal al Halbawi ambaye ni miongoni mwa viongozi wa harakati ya Ikhwanul Muslimin ya Misri, Muhyiddin Kabiri ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama cha Kiislamu cha Tajikistan, Mshauri wa Waziri wa Wakfu wa Syria Nabiil Sulaiman, Mwenyekiti wa Baraza la Mashauriano la Sudan Abdurrahman Umar, Mwenyekiti wa Jumuia ya Maulamaa wa Kiislamu wa Lebanon Sheikh Ahmad Zein, Sheikh Khalid Mulla ambaye ni miongoni mwa wanazuoni wa Kisuni wa Iraq, Mufti Mkuu wa Bosnia Mustafa Sarich na Sheikh Bilal Said Shaaban ambaye ni Mwenyekiti wa Harakati ya Tauhidi ya Lebanon wameeleza mitazamo yao kuhusu masuala mbalimbali ya ulimwengu wa Kiislamu.
Pamoja na kusisitiza juu ya udharura wa kuimarishwa umoja na mshikamano kati ya Waislamu, wanafikra hao wamekitaja kipindi cha sasa katika ulimwengu wa Kiislamu kuwa ni muhimu mno na cha kihistoria. Wamesisitiza kuwa harakati ya mamilioni ya wananchi katika ulimwengu wa Kiislamu hususan Misri na maeneo mengine ni mwangwi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran chini ya uongozi wa Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu) ambao unadhihiri sasa baada ya kupita zaidi ya miaka 30.
Maulamaa na wanafikra hao wa Kiislamu pia wameashiria nafasi na mchango mkubwa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika dunia ya Kiislamu na maendeleo makubwa ya kisayansi ya Iran na kusema kuwa matukio ya sasa katika ulimwengu wa Kiislamu yatatayarisha uwanja nzuri wa kuundika kambi mpya ya Kiislamu kandokando ya nguvu kubwa ya Iran, na suala hilo litabadili mlingano wa kimataifa.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu Ayatullah Muhammad Ali Taskhiri pia amehutubia kikao hicho akiashiria mkutano wa sasa wa 24 wa Umoja kati ya Waislamu. Amesema kuwa sehemu moja ya ajenda ya mkutano huo imechunguza njia za kinadharia na kivitendo za kukurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu na sehemu nyingine imechunguza matukio ya hivi karibuni katika ulimwengu wa Kiislamu. Ameongeza kuwa wanafikra mia nne wa Kiislamu kutoka ndani na nje ya nchi wameshiriki katika Mkutano wa 24 wa Kimataifa wa Umoja kati ya Waislamu. 751219

captcha