Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa kusherehekea maulidi ya Mtume Muhammad SAW na Imam Jafar Sadiq AS na kusisitiza kwamba mwamko wa wananchi katika baadhi ya nchi za eneo ni ishara ya kuongezeka uwezo wa mwanaadamu wa kustafidi zaidi na nyota yenye nuru ya Uislamu na Bwana Mtume Muhammad SAW.
Ameongeza kuwa, mateso yanayoyakabili mataifa ya eneo hili yataweza kuondoka pale mkono wa shetani mkubwa Marekani utakapokatwa katika maamuzi ya mustakbali ya mataifa mengine.
Amekutaja kuzaliwa Bwana Mtume Muhammad SAW kwamba kulikuwa ni kuchomoza alfajiri angavu katika maisha ya mwanaadamu na kuoingeza kuwa, kadiri ufahamu na welewa wa mwanaadamu unavyozidi kuwa mkubwa katika kipindi chote cha historia ndivyo baraka za kubaathiwa kutukufu kwa Mtume wa Uislamu zinavyozidi kuonekana na kwamba hivi sasa ishara za uhakika huo mng'avu zinaonekana katika eneo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, mwamko wa Waislamu katika baadhi ya nchi za eneo ikiwa ni pamoja na Misri na Tunisia ni ishara ya kuchoshwa mataifa ya nchi hizo kulikowafanya wasimame hivi sasa kupinga "kudhalilishwa, dhulma na kipindi cha kiza" na kwamba mashinikizo na uingiliaji wa madola ya kiistikbari yakiongozwa na Marekani katika maisha ya kijamii, kiuchumi, kiutamaduni na kisiasa ya nchi hizo kumewachosha wananchi na sasa wameamua kupambana na jambo hilo.
Ayatullah Udhma Khamenei amefafanua zaidi suala hilo akisema, malalamiko ya wananchi yanaonekana wazi hata katika nchi za Magharibi kutokana na wananchi hao kuchoshwa na ustaarabu wa kimaada usio wa kimaanawi. Amesema kama Waislamu wataweza kuutangaza vizuri Uislamu kwa walimwengu kwa kutumia maneno na vitendo vyao basi bila ya shaka yoyote walimwengu wataweza kuingia katika Uislamu kwa makundi. Amesema kuwa, uhakika huo unalifanya jukumu la Waislamu kote duniani la kuangalia upya mitazamo na vitendo vyao lizidi kuwa kubwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema, kitendo cha wananchi wa eneo hili cha kuonyesha kukasirishwa na suala la kuwepo mabeberu katika eneo ni matunda ya kwanza kabisa ya mwamko wa Waislamu katika baadhi ya nchi za eneo. Amekumbusha kuwa, Wamarekani wanafanya juhudi kubwa za kukwepa athari za harakati hii adhimu lakini bila ya shaka yoyote watashindwa tu kwani mataifa ya eneo hili yameshaelewa kwamba siasa za Marekani na vibaraka wake ndiyo sababu kuu inayopelekea kushuhudiwa udhalilishaji, kuzuka hitilafu na kuweko hali ya undumilakuwili kati ya wananchi. Hivyo amesema, ufunguo wa kuweza kutatua matatizo ya Waisalmu ni kufukuzwa Marekani katika eneo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, kuzusha mpasuko kati ya wananchi na tawala zao ni matokeo mengine ya siasa za Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati na kuongeza kuwa, kujitokeza wananchi katika medani kutaweza kung'oa mizizi ya madola ya kibeberu na kama tawala za eneo hili zitakubali kutekeleza matakwa ya wananchi, basi bila ya shaka si Marekani tu, bali dola lolote jingine la kibeberu halitaweza kuzitwisha nchi hizo malengo yake.
Vile vile amelitaja dola pandikizi la Kizayuni kuwa ni donda ndugu la kensa na ndilo linalosababisha kuzuka maradhi mengine katika eneo kama vile kudumaa kisiasa na kiuchumi na kwamba madola ya kibeberu yanatumia nguvu zao zote kulilinda donda hilo linaloeneza vita na ugomvi katika eneo lakini hasira za watu wa eneo hili zimekuwa kubwa sana hivi sasa dhidi ya donda hilo la kensa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema, maulamaa wa kidini na watu muhimu kisiasa, kielimu na Vyuo Vikuu wana jukukmu kubwa la kuliongoza vizuri wimbi hili kubwa la kuenea mwamko wa Kiislamu katika eneo na amesisitiza kwamba, watu muhimu katika nchi za eneo wanapaswa kusimama imara na wasiruhusu madola ya kibeberu ambayo yanatumia hila na ujanja tofauti, kuipora harakati hii adhimu ya wananchi.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la kuwa macho na kuongoza vizuri harakati ya mwamko wa Kiislamu ili iweze kufanikisha malengo yake matukufu kuwa ni maandalizi ya kushuhudiwa mustakbali angavu katika eneo na kwa uma mzima wa Kiislamu.
Huku akiashiria sifa za kipekee za kijamii na kijiografia za Waislamu bilioni 1.5 duniani ameongeza kuwa, inabidi hali mbaya inayoukabili uma wa Kiislamu hivi sasa ibadilike na bila ya shaka mabadiliko hayo yataweza kushuhudia karibuni tu kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu na baraka za Uislamu.
Vile vile ametoa ushahidi kutoka kwenye Qur'ani Tukufu na kusema kwamba kutawakali kwa Mwenyezi Mungu, kunyenyekea mbele Yake, kuhurumiana Waislamu ambao ni ndugu na kuwa imara mbele ya mabeberu na madhalimu ni miongoni mwa sifa anazopasa kuwa nazo kila Muislamu na kila jamii ya Kiislamu.
Ameongeza kuwa, taifa azizi la Iran litaendelea na njia yake hiyo ya ufanisi kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu na kwamba mataifa mengine ya Kiislamu nayo pole pole yanaingia kwenye njia hiyo ili ahadi ya Mwenyezi Mungu iweze kutimia aliposema: و العاقبه للمتقين yaani mustakbali mwema ni wa watu wenye taqwa na wacha Mungu.
Mwanzoni mwa mkutano huo, Rais Ahmadinejad wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria sifa za kipekee za Bwana Mtume Muhammad SAW kama vile subira, muqawamah, ibada, busara, hekima, uadilifu, kumtetea mnyonge pamoja na heshima na utukufu mkubwa na kuongeza kuwa, mafundisho ya Bwana Mtume Muhammad SAW ni malengo matukufu duniani na ni kitu kinachohitajiwa na walimwengu wote. Amesema, baadhi ya jamii za mwanaadamu zimesimama kidete kupambana na udhalilishaji, dhulma na uporaji unaofanywa na mabeberu, baada ya jamii hizo kupata nuru ya ukweli.
Rais Ahmadinejad ameongeza kuwa, pamoja na kuwepo njama nyingi tata za waistikbari na mabeberu lakini mataifa yanazidi kuamka hivi sasa kuelekea kwenye njia ya Manabii na Mitume wa Mwenyezi Mungu na kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mlinganiaji mkubwa wa njia ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuandaa mazingira ya kusimamishwa serikali ya Imam Mahdi AS.
751444