IQNA

Sanaa ya Kiislamu inatoka ndani roho na imani ya kweli

10:04 - March 05, 2011
Habari ID: 2090157
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sanaa za Kiislamu cha Tabriz (magharibi mwa Iran) akiwa pamoja na wasaidizi, wanachama wa jopo la kielimu, wakuu wa vitengo mbalimbali na wasanii wa chuo hicho mapema leo wamekutana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei. Katika mkutano huo kumezinduliwa Qur'ani yenye thamani kubwa iliyofumwa juu ya zulia.
Kazi hiyo yenye thamani kubwa ya kisanii inakusanya juzuu zote 30 za Qur'ani Tukufu katika vipande 76 vyenye maandishi katika pande mbili. Wasanii wa Tabriz wametumia miaka sita kamili kufuma zulia hilo lenye sura zote za Qur'ani chini ya usimamizi wa Chuo Kikuu cha Sanaa za Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa zulia hilo lenye maandishi ya Qur'ani ni fahari itakayobakia hai na kumbukumbu adhimu ya utawala wa Jamhuri ya Kiislamu. Amesema kazi hiyo ya kisanii imetokana na upendo na mahaba makubwa ya wasanii wa nchi hii na kwamba majina ya wafumaji wake yatakumbukwa kwa karne kadhaa zijazo.
Amewashukuru wasanii wote walioshiriki katika kufanikisha kazi hiyo kubwa na akasema: "Qur'ani hii itatolewa zawadi kwa jumba la makumbusho la Haram ya Imam Ali bin Mussa al Ridha (as) (katika mji mtakatifu wa Mash'had) ili ibakie hai na kuwafaidisha watu wote.
Amesema sanaa ya Kiislamu ni suala muhimu mno na huku akiashiria tofauti iliyopo baina ya sanaa ya Kiislamu na isiyo ya Kiislamu, Ayatullah Khamenei amesema, tofauti ya sanaa ya Kiislamu na sanaa nyingine imo katika roho ya sanaa hiyo, kwani sanaa ni suala linalomhusu mwanadamu na inatokana na ilhamu na hisia za ndani ya nafsi. Amesisitiza kuwa wakati sanaa hiyo inapotoka ndani ya roho, itikati na imani halisi, ndipo inapotengeneza sanaa ya Kiislamu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa sanaa ya Kiislamu haiwezi kutengenezwa kwa kutoa amri bali ni matokeo ya mtazamo sahihi wa roho na mtazamo wa msanii.
Ayatullah Khamenei amesisitiza juu ya kutiliwa maanani sanaa za kazi za mikono katika maeneo mbalimbali ya Iran na akawausia viongozi kuwahamasisha wasanii wakongwe ili wadumishe na kuendeleza sanaa hiyo ambayo aghalabu hutimia kwa mashaka na kazi nzito.
Mwanzoni mwa mkutano huo Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sanaa za Kiislamu cha Tabriz Dakta Keinejad ametoa ripoti kuhusu shughuli za chuo hicho na akasema kuwa Chuo Kikuu cha Sanaa za Kiislamu cha Tabriz kinapokea wanafunzi katika vitengo 22 vya shahada ya digri, vitengo 10 vya shahada ya uzamili na vitengo viwili vya shahada ya uzamivu. Amesema katika kipindi cha miaka 11 ya shughuli zake, chuo hicho kimefanikiwa kutumia walimu bingwa na kufaidika na uwezo wao mkubwa katika kuhuisha sanaa za kijadi.



captcha