Ayatullah Khamenei ameyasema hayo, Alkhamisi asubuhi, Machi 10, 2011 alipoonana na Mkuu na wajumbe wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu linalomchagua Kiongozi Muadhamu na kusimamia kazi zake. Amelishukuru baraza hilo kwa hatua yake ya busara mno ya kuchagua viongozi wake wapya kwa hekima ya hali ya juu.
Huku akibainisha majukumu yenye hatari nyingi ya viongozi na wanasiasa nchini Iran katika kipindi hiki nyeti sana, ametoa ujumbe maalumu kwa wote na hususan vijana katika hotuba yake hiyo muhimu sana akisema: "Huu ndio ujumbe wangu; kuvunjiana heshima kwa aina yoyote ile na vitendo vyovyote visivyo vya kimaadili na vya udhalilishaji ni kinyume cha sharia, vinakinzana na mantiki ya kisiasa, ni pigo kwa Jamhuri ya Kiislamu na vinamkasirisha Mwenyezi Mungu."
Aidha amewashukuru sana wanavyuoni wanaounda baraza hilo la wataalamu na amegusia pia kushindwa njama za maadui katika zoezi la kuchaguliwa viongozi wapya wa baraza hilo. Ametoa shukrani zake za dhati wa wajumbe wa baraza hilo na hususan Bw. Hashemi Rafsanjani na kuongeza kuwa, maadui walikuwa wanasubiri kuona kunazuka mizozo na ugomvi kati ya wajumbe wa baraza hilo na walitaka kuufanya ushindani wa kuhudumia taifa na wananchi uonekane ni kitu kinachotokana na uchu wa madaraka lakini kwa baraka za ikhlasi za wanavyuoni wanaounda baraza hilo muhimu na akili na umakini katika vitendo na matamshi yao, suala la uchaguzi huo limepita salama kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu na limekuwa ni kwa manufaa ya Uislamu na Jamhuri ya Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria mwenendo wa Bw. Hashemi Rafsanjani katika suala hilo na kusema kuwa hakutarajia kitu kingine kutoka kwake zaidi ya busara aliyoionyesha hususan kutokana na historia yake ndefu ya kutumia busara na kutekeleza vizuri majukumu yake.
Ayatullah Udhma Khamenei aidha amesema kuwa, kuchaguliwa Ayatullah Mahdavi Kani kuwa mkuu mpya wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu ni hatua nzuri sana na kuongeza kuwa, Ayatullah Mahdavi Kani siku zote ameonyesha ustahiki wake katika masuala yote tangu awali ya Mapinduzi ya Kiislamu hadi hivi sasa tena katika nyanja zote ikiwa ni pamoja na kwenye masuala ya dini, siasa, masuala yanaondelea nchini, Hawza na Chuo Kikuu na katika nyuga nyinginezo mbali mbali nchini.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amesema, jukumu la Iran hivi sasa kwa kuzingatia matukio yanayoendelea kushuhudiwa katika eneo; ni nyeti mno; na ameongeza kuwa, kuna matukio adhimu sana yanaendelea kutokea katika nchi za eneo (la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika) na kwamba hivi sasa ndio kwanza ni mwanzo tu wa mabadiliko hayo na inabidi kuvitambua vizuri vipengee vyote vya matukio hayo ili kwa njia hiyo yaweze kutekelezwa vilivyo majukumu yanayojitokeza.
Ayatullah Udhma Khamenei pia amesisitiza kuwa, "kujitokeza vilivyo wananchi katika medani" na "kaulimbiu ya Kiislamu" ni masuala mawili muhimu sana ya mabadiliko yanayoshuhudiwa hivi sasa katika eneo na kuongeza kuwa, mchakato wa matukio hayo ulikuwa ndiyo matumaini ya muda mrefu ya Waislamu wote wakweli na wenye fikra pana nchini Iran na katika nchi nyinginezo duniani.
Amesema, kujitokeza vilivyo na istikama ya mataifa ya eneo katika medani yenye hatari nyingi ya mapambano ndiko kunakotoa dhamana ya ushindi na amekumbusha kuwa, wakati wananchi wanapojitokeza kwenye medani kwa miili na nyoyo zao kama ilivyoshuhudiwa nchini Iran miaka 32 iliyopita, bila ya shaka yoyote nguvu za Mwenyezi Mungu huzifanya nia na azma za watu hao kuwa imara zaidi na huufanya ushindi wao kuwa kitu kisichoepukika.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, wakati Mwenyezi Mungu anapounga mkono nia za mataifa yaliyosimama imara kupigania haki zao, si tu watawala vibaraka, mafisadi na mabeberu hawawezi kufanya kitu, lakini hata Marekani na madola mengine ya kibeberu licha ya kuwa kiasili na kimaumbile yana tabia ya mauaji na ukatili mkubwa dhidi ya wananchi lakini mwishowe yatashindwa tu na ahadi za Mwenyezi Mungu zitatimia kama ambavyo tayari tumeshuhudia uhakika uliowashitua mabeberu kwenye baadhi ya matukio yanayoendelea katika eneo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameitaja "kaulimbiu ya Kiislamu" kuwa ni sifa nyingine maalumu ya mapambano ya wananchi katika eneo na kuongeza kuwa, bila ya shaka katika mapambano hayo ya wananchi iko pia misukumo mingine kama vile ya kiliberali, kikabila na misukumo mingineyo, lakini asili na dhati ya watu wa eneo hili ni Waislamu na ndio maana nara na kaulimbiu ya Kiislamu ikajitokeza wazi katika matukio yanayoendelea kushuhudiwa katika nchi mbali mbali za eneo.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la kuwa kigezo Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kuwa ni moja ya mambo yaliyochangia kushuhudiwa matukio muhimu sana ya eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika na amesisitiza kuwa, "kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu, kuundwa Jamhuri ya Kiislamu, kubakia, kuzidi kuwa imara na kila leo kuzidi kupata maendeleo makubwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran" kumeufanya mfumo huu wa Kiislamu kuwa kigezo kinachorejesha utambulisho na heshima ya mataifa ya Kiislamu katika eneo na bila ya shaka yoyote wananchi wa eneo hili wameathiriwa na jambo hilo.
Amesema njama zinazofanywa na maadui wa Uislamu na Iran za kujaribu kuzuia Jamhuri ya Kiislamu isiwe kigezo ni moja ya ushahidi wa wazi wa uhakika huo usiokanushika. Ameongeza kuwa, mabeberu wa dunia wanatumia hila na mbinu mbali mbali kama vile kukuza sana udhaifu unaojitokeza na kueneza uongo kwa njia ya moja kwa moja na isiyo ya moja kwa moja ili kupunguza kasi ya mataifa mengine duniani kuifanya Jamhuri ya Kiislamu kuwa ni kigezo kwao.
Amesema kuna sababu mbili za ndani na nje zinazoweza kudhoofisha suala la Jamhuri ya Kiislamu kuwa kigezo kwa mataifa mengine na ametaja sababu ya ndani kuwa ni pamoja na mapungufu, kuzembea mambo, kutotekeleza vizuri majukumu, mizozo, uchu wa madaraka, kukosa siasa makini na kupenda mambo ya dunia. Amesema mambo hayo yanaweza kuharibu sura ya Jamhuri ya Kiislamu mbele ya macho ya mataifa mengine na amesisitiza juu ya kuwa macho watu wote nchini ili kukabiliana vilivyo na mambo kama hayo. Amma kuhusu sababu ya nje ambayo amesema ni pamoja na propaganda mbaya za maadui amesisitiza kuwa, propaganda hizo zitashindwa tu kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu.
Aidha amewataka viongozi nchini, watu muhimu, wasomi, maulamaa na watu wote wenye ushawishi katika jamii wawe macho kikamilifu na waongeze juhudi zao katika kukabiliana masuala na sababu za ndani zinazoweza kudhoofisha nafasi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea na hotuba yake hiyo muhimu akizungumzia sababu za kuweza kudhoofika Jamhuri ya Kiislamu na kulaumu vikali sana vitendo visivyo vya kimaadili akisisitiza kwamba, anga ya kuvunjiana heshima na kashfa haikubaliwi na Uislamu, ni kinyume cha sharia, inakinzana na mantiki ya kisiasa na inamkasirisha Mwenyezi Mungu.
Amesema suala la kukosoa, kupinga, kutangaza wazi na kishujaa itikadi ya mtu ni jambo lisilo na tatizo lolote lakini ameongeza kuwa, inabidi mambo hayo yote yafanywe bila kuvunjiana heshima wala kukashifiana ili kuepusha kuharibu utulivu wa wananchi katika jamii na kwamba jukumu la kufanya hivyo ni la watu wote nchini.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kusema katika matamshi yake ya wazi yaliyowalenga watu wote na hususan vijana kwamba: "Ujumbe wangu kwa watu wote wanaotoa matamshi, au wanaoandika kwenye magazeti, au watu wa blogi na maeneo mengine yote ni kwamba kuna tofauti kubwa baina ya kupinga kitu, kukataa na kulaani fikra fulani ya kisiasa na kidini na kutumbukia kwenye vitendo visivyo vya kimaadili, vya kuvunjiana heshima na kuharibiana majina. Mimi ninapinga vikali na kikamilifu masuala yote yasiyo ya maadili mema na nasema (wazi kwamba) mambo hayo hayapaswi kufanywa."
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia juu ya kosa kubwa na mtazamo ulio ghalati kikamilifu akisema kuwa, baadhi ya vijana wenye ikhlasi, waumini na wazuri kwa bahati mbaya wanadhani kwamba wanapofanya mambo hayo ndio huwa wanatekeleza vilivyo majukumu yao lakini mambo hayo kwa kweli ni kinyume kikamilifu na utekelezaji unaotakiwa wa majukumu.
Amefafanua zaidi suala hilo akisema, ni jambo la dharura kuwa macho mbele ya uwezekano wa kujipenyeza maadui katika safu za watu na ametahadharisha akisema, kama ambavyo Imam Khomeini alikuwa akisisitiza mara kwa mara, baadhi ya wakati maadui hujipenyeza kwenye safu za watu waumini na wenye ikhlasi na kuwapotosha katika harakati zao, hivyo inabidi kutoghafilika pia na jambo hilo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia juu ya haja ya kujiepusha na mighafala inayotokana na hisia kali na kuongeza kuwa: Ninawaomba watu wote na hasa vijana azizi wasiruhusu kuendelea anga ya kutuhumiana na kuvunjiana heshima kwani kama anga hiyo itaendelea kuwepo, inaweza ikawa mithili ya maradhi ambayo yataenea katika mambo yote.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia baadhi ya vitendo visivyo vya kimaadili vinavyofanywa na baadhi ya watu na kusema kuwa vitendo hivyo ni ghalati ndani ya ghalati.
Amesema, vitendo visivyo vya kimaadili na vya kuvunjiana heshima havihudumii Mapinduzi ya Kiislamu na vinakinzana na malengo ya taifa bali vile vile hupelekea kuzuka mifarakano na utengano katika jamii kama ambavyo vinatoa pigo kwa mfumo wa Kiislamu hivyo amewausia vijana wajiepushe kikamilifu na vitendo kama hivyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia ametoa nasaha zake kwa wakubwa akisema, kuchukua misimamo sahihi, kutoa matamshi yakinifu na kuepuka kuathiriwa na habari za uongo ni miongoni mwa majukumu muhimu ambayo inabidi watu wazima wayazingatie barabara.
Ameongeza kukwa, kuna baadhi ya watu wanaziweka chini ya alama ya kuuliza kazi na juhudi zote za mfumo na jitihada yote ya usiku na mchana yenye tabu nyingi inayofanywa kwa ikhlasi na viongozi nchini hususan serikali, kwa kusikia habari moja tu ya uongo. Amesema mwenendo huo nao si sahihi na inabidi kujiweka mbali nao.
Mwanzoni mwa mkutano huo, Ayatullah Mahdavi Kani, Mkuu wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu ametoa hotuba fupi na kuzungumzia kufanyika vikao rasmi vya siku mbili vya baraza hilo siku chache zilizopita na kuhudhuriwa na wajumbe 81. Amesema, vikao hivyo vimechagua mkuu na jopo la uongozi wa baraza hilo jopo ambalo litafanya kazi kwa muda wa miaka miwili ijayo akisema kwamba jukumu la kuongoza baraza hilo amekabidhiwa yeye na amemshukuru Ayatullah Hashemi Rafsanjani kwa mapenzi na hekima kubwa alizozionyesha katika suala hilo.
Kwa upande wake, Ayatullah Yazdi, Naibu wa Kwanza wa Mkuu wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu ametoa ripoti fupi kuhusiana na vikao rasmi vya siku mbili vya hivi karibuni vya baraza hilo na kuongeza kuwa, miongoni mwa mambo yaliyozungumziwa katika vikao hivyo ni pamoja na kuwashukuru wananchi kutokana na hamasa kubwa waliyoionyesha katika maandamano ya Bahman 22 (Februari 11, siku ya kufikia kileleni maadhimisho ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran), suala la harakati za mataifa ya Kiislamu la kuifanya Jamhuri ya Kiislamu kuwa kigezo chao, mapambano dhidi ya ubeberu, wajibu na udharura wa kushikamana na njia ya Imam Khomeini (quddisa sirruh), udharura wa kuchukuliwa hatua kali za kisheria wahusika wakuu wa fitna na sisitizo juu ya wajibu wa watu wote nchini kuwa waangalifu katika maneno na matendo yao.
761536