IQNA

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu: Harakati kubwa zaidi za umma zitaibuka katika eneo

0:12 - April 04, 2011
Habari ID: 2099988
Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, katika siku za usoni kutashuhudiwa harakati kubwa zaidi za wananchi katika eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika.
Ayatullah Khamenei ameyasema hayo, Jumapili Aprili 3, 2011, mjini Tehran wakati aliponana na makamanda wa ngazi za juu wa jeshi na maafisa wa Polisi wa Jamhuri ya Kiislamu. Ameongeza kuwa, harakati za mataifa mbali mbali zinaweza kupata baraka kadiri siku na miaka inavyopita kutokana na kufanyakazi bila kuchoka, kuwa na ubunifu, kutumia vizuri vipaji vyake taifa husika, kuwa na mtazamo wa mbali sambamba na kutawakali kwa Mwenyezi Mungu.

Amesisitiza kuwa, harakati iliyojaa baraka ambayo imeanza leo hii katika eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika, ni sehemu ya matunda ya kusimama kidete, kuwa na imani thabiti na ushujaa wa taifa la Iran pamoja na mataifa ya eneo kuingia kwenye medani, yakiwa imara, yaliyojaa hamasa na imani ya kweli. Aidha amesema kwamba, kutashuhudiwa mabadiliko makubwa zaidi katika siku za usoni.


Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia sifa maalumu ya msimu wa machipuo na mwaka mpya unaokwenda sambamba na kumea upya mimea na kuongeza kuwa, wanaadamu nao wanaweza kutangamana na ulimwengu wa maumbile na kutumia fursa hiyo kwa ajili ya kuzifanya nafsi zao zimee upya na kupata utukukfu ili wazidi kupata nguvu za ubunifu, kufanya kazi kwa idili na kuchanua fikra zao.

Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, kufanya harakati kwa nia ya kufanikisha malengo ya Mwenyezi Mungu na kuwa na imani na msaada wa Allah huandaa mazingira ya kumea upya nafsi ya mwanaadamu na kupata utukufu. Ameongeza kwamba, kuwa na yakini na msaada wa Mwenyezi Mungu, kumwamini Allah na kutovunjika moyo mbele ya mashaka na matatizo pamoja na kuwa na muono mpana na wa kihistoria ndiyo siri ya maendeleo, hivyo kuna haja ya kuimarishwa moyo wa namna hiyo kadiri inavyowezekana.

Ameutaja ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusimama imara taifa la Iran mbele ya matatizo na mashinikizo mengi yanayolikabili taifa hili kuwa ni mfano mmoja wa harakati yenye umeefu na utukufu na ameongeza kuwa, takriban wasomi wote wa dunia wanakiri kuwa, harakati za wananchi zinazoshuhudiwa hivi sasa katika eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika zinatokana na mapambano ya taifa la Iran.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia juu ya taathira za ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika mabadiliko na milingano ya kieneo na kimataifa ikiwemo kadhia ya Palestina na kuvunjwa-vunjwa kiburi, majigambo na haiba ya mabeberu duniani na kuongeza kuwa, harakati za hivi sasa za wananchi wa eneo hili zinatokana na kurundikana pole pole na kwa muda mrefu misukumo, fikra na maamuzi ya wananchi hao na hivi sasa ndipo yameripuka. Amesema, haya yote yanatokana na istiqama na kutotetereka taifa la Iran sambamba na mataifa ya dunia hususan ya eneo hili kuona dalili nyingi nzuri za maendeleo ya Iran ya Kiislamu.

Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni mithili ya mti wenye baraka ambao matunda yake ya kusimama kidete kwa muda wa miaka 32 yanaendelea kuoneka kwenye kalibu ya kuzidi kupata heshima taifa la Iran, kuzidi kuimarika kisiasa utawala wa Kiislamu, kuzidi kupata maendeleo na ustawi katika nyanja mbali mbali za kisayansi na kiuchumi na kutolegeza kamba mbele ya madola ya kibeberu. Amesema, hivi sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa kigezo bora kwa mataifa ya eneo hili.

Amesema, kadhia ya nyuklia ni moja ya mifano ya kusimama kidete taifa la Iran mbele ya mashinikizo ya mabeberu na kukumbusha kuwa, madola ya kibeberu yametumia nguvu zao zote za kisiasa, kipropaganda na kiuchumi ili kupambana na kadhia ya nyuklia ya Iran na waistikbari wanaendelea kufanya njama nyingi kwa namna tofauti ili kuilazimisha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iachane na miradi yake ya amani ya nyuklia lakini hivi sasa na baada ya kupita miaka minane ya kuweko njama na mashinikizo hayo ya mabeberu katika suala hilo la nyuklia, Iran ya Kiislamu imefanikiwa kushinda njama na mashinikizo yote ya waistikbari na wakati huo huo imepiga hatua kubwa za kimaendeleo katika kadhia yake ya nyuklia na imewathibitishia kivitendo walimwengu kuwa, nguvu za irada na kutotetereka vitani ni kubwa na imara zaidi ikilinganishwa na mabavu ya madola ya kibeberu duniani.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, katika vita vyake vya miaka 32 na madola ya kibeberu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran si tu haijalegeza kamba wala kusalimu amri mbele ya mfumo wa kimataifa wa dhulma, lakini pia imepiga hatua kubwa za kimaendeleo katika kipindi hicho cha miaka 32 huku hivi sasa maadui wakiongozwa na Marekani wakiwa wamezidi kuwa dhaifu na wanazidi kufeli katika mambo na njama zao.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei ambaye ndiye Amirijeshi Mkuu wa Majeshi yote ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amevitaka vikosi vya ulinzi nchini kujiimarisha zaidi kiimani, kikazi na kwa juhudi zisizochoka na kusisitiza kuwa, kumeanza harakati nzuri katika vikosi vya ulinzi nchini ambapo inabidi kasi ya harakati hiyo iongezwe ili iendelee kushuhudiwa harakati na nishati zaidi katika vikosi hivyo.

Vile vile amesisitiza juu ya ulazima wa kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja kadiri inavyowezekana, kunyanyua kiwango cha mafunzo, kujiimarisha zaidi vikosi hivyo kama taasisi, kuongeza uwezo wake wa mapambano na zana za kivita na kuongeza kuwa, vikosi vya ulinzi katika utawala wa Jamhuri ya Kiislamu ni uzio na ngao ya wananchi hivyo inabidi ngao hiyo iwe imara wakati wote.

Katika mkutano huo, Meja Jenerali Dk. Firuzabadi, Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa ripoti kuhusu juhudi na kazi zilizofanywa na vikosi vya ulinzi vya Iran katika mwaka uliopita (wa Kiirani wa 1389 Hijria Shamsia) na kusema kuwa, kuwasilishwa mpango mkuu wa vikosi na taasisi za ulinzi, kuboreshwa uwezo wa ulinzi, kujiimarisha kimapambano katika asasi mbali mbali ikiwa ni pamoja na anga, anga za juu na baharini na maendeleo ya mpango wa mabadiliko ya Sepah ni miongoni mwa kazi zilizofanywa mwaka huo na vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Mwishoni mwa mkutano huo, Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, amewasalisha hadhirina sala za Adhuhuri na Alasiri.
768101
captcha