IQNA

Ayatullah Khamenei:

Kushindwa njama za maadui na taufiki ya taifa la Iran ni alama ya kutimia ahadi ya Mwenyezi Mungu

13:22 - April 28, 2011
Habari ID: 2113421
Ayatullah Khamenei amesema kushindwa njama za maadui na taufiki na mafanikio ya kila leo ya taifa la Iran ni alama ya kutimia ahadi ya Mwenyezi Mungu. Amesema taifa, serikali na viongozi wa Iran wataendeleza jitihada zao katika njia ya Mwenyezi Mungu na Yeye Mola Karimu ataendelea kuliteremshia rehma na baraka zake taifa hili.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei mapema leo alihutubia mkusanyiko mkubwa wa wafanyakazi kutoka kote nchini Iran akisema kuwa maendeleo na ustawi ndiyo hatima na matunda ya taifa la Iran. Ayatullah Khamenei ameashiria nafasi na hadhi kubwa na muhimu mno ya mfanyakazi katika Uislamu na katika mantiki na busara na akasema kuwa kushikamana sekta zote za serikali na zisizokuwa za serikali na kaulimbiu ya mwaka mpya wa Jihadi ya Kiuchumi kutaleta vuguvugu na harakati nchini Iran na kulipa fahari taifa hili.
Katika mkutano huo uliofanyika kwa mnasaba wa kukaribia maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wafanyakazi, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa katika mtazamo wa mantiki na busara, 'kazi na mfanyakazi' ni sehemu muhimu mno katika kudhamini mahitaji ya kimaisha ya mtu binafsi na jamii.
Akieleza zaidi kuhusu nafasi ya kazi na mfanyakazi, Ayatullah Khamenei amesema mfanyakazi ana nafasi ya juu pia katika Uislamu kwani dini hiyo inaitambua kazi kuwa ni ibada na amali njema, na Mtume Mtukufu wa Uislamu alikuwa akibusu mikono ya wafanyakazi akiitambua kuwa ni mikono ambayo haitachomwa na moto wa Jahannam.
Ayatullah Khamenei ameashiria pia mchango wa jamii ya wafanyakazi katika kufanikisha mapambano ya taifa la Iran dhidi ya utawala wa kidhalimu wa Shah na akasema: "Katika kipindi cha mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran watu wa mrengo wa kushoto wa zama hizo yaani Wakomunisti, walifanya jitihada kubwa za kuiweka jamii ya wafanyakazi mkabala wa Uislamu na utawala wa Kiislamu nchini, lakini wafanyakazi waliitambua sauti ya dini kuwa ndiyo sauti yao na inayofaa na wakasimama kukabiliana na njama hiyo."
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa kushiriki kwa wingi tabaka la wafanyakazi katika vita vya kujitetea kutakatifu na baadaye katika medani za kuchapakazi na juhudi za maendeleo na ustawi ni miongoni mwa alama za kushikamana kwa jamii hiyo na Uislamu, Mapinduzi ya Kiislamu na Iran. Ameongeza kuwa mfanyakazi mwenye ghera na hadhi ya Kiirani hutambua kazi kuwa ni mapambano na hutumia kazi, ubunifu na kipawa chake cha Kiirani kwa ajili ya kukabiliana na mabeberu na wale wote wanaotaka kuyumbisha na kukwamisha uchumi wa Iran.
Amesema kuwa siasa kuu za serikali ya Kiislamu na viongozi hapa nchini ni kujenga ushirikiano na upendo kati ya wadau wa sekta ya kazi. Amesisitiza kuwa hata hivyo kuna watu hapa nchini wanaowadhulumu wafanyakazi na kupuuza haki zao japokuwa siasa kuu za mfumo wa Kiislamu ni kujenga hali ya ushirikiano na maelewano kati ya mfanyakazi, mwajiri na vyombo husika.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria hatua na mipango muhimu ya serikali kwa ajili ya kutatua masuala ya jamii ya wafanyakazi na akaongeza kuwa hatua na mipango mbalimbali inapaswa kutekelezwa kwa njia ambayo itaiwezesha jamii ya wafanyakazi na kuboresha hali yao.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria mwaka huu uliopewa jina la mwaka wa Jihadi ya Uchumi na akasema kuwa pamoja na kuendeleza njama zake katika nyanja za utamaduni, usalama, siasa na kadhalika, adui anauhujumu Uislamu na Jamhuri ya Kiislamu kwa kulenga uchumi ili aweze kuweka ufa na mtengano kati ya wananchi, serikali na utawala wa Kiislamu; kwa sababu hiyo kuna udharura wa kupigana jihadi dhidi ya adui kwa uwezo wote sambamba na kuwa na ikhlasi, uoni mpana na mtazamo wa kina.
Ayatullah Khamenei amesisitiza juu ya majukumu mazito ya sekta zote za serikali, watu binafsi na wananchi katika mwaka wa Jihadi ya Uchumi na akaitaka jamii ya wafanyakazi kuboresha kazi. Amesema kazi zinapaswa kufanyika kwa uhodari, uangalifu mkubwa na kwa njia sahihi.
Vilevile amelitaja suala la kuboresha kiwango cha bidhaa zinazozalishwa hapa nchini kuwa ni miongoni mwa majukumu ya jamii ya wafanyakazi na waajiri. Amesema tunapaswa kufanya kazi vyema ili bidhaa za Iran ziwe bidhaa bora, zenye kudumu na kuvutia watumiaji wa Iran na wasiokuwa Wairani. Hata hivyo amesisitiza kuwa serikali pia inapaswa kuandaa mazingira mazuri ya kufikiwa lengo hilo ikiwa ni pamoja na kutoa elimu na mafunzo.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa mseto wa 'sanaa na uwezo' wa Kiirani unaweza kutayarisha uwanja mzuri wa kuboreshwa viwango vya bidhaa zinazozalishwa hapa nchini. Ameongeza kuwa baadhi ya bidhaa zinazozalishwa nchini zina uwezo wa kushindana na bidhaa za kigeni na hata baadhi ya bidhaa hizo ni bora zaidi kuliko za nje. Amesisitiza kuwa sifa hiyo inapaswa kupanuliwa na kuhusu bidhaa zote za vyakula, mavazi na nyezo za kimaisha.
Amesema medani ya uzalishaji bidhaa bora ndani ya nchi inapaswa kuwa medani nyingine ya kudhihirisha kivitendo kaulimbiu ya "Sisi Tunaweza" kwa hima ya wafanyakazi, wahandisi na wawekezaji.
Akiashiria baadhi ya watu ambao hulitambua jambo la kutumia bidhaa za kigeni kuwa ni sifa na alama ya kuwa bora zaidi na wengine, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, kutekwa na tabia ya kupenda bidhaa zilizozalishwa nje ya nchi na kupuuza juhudi za wafanyakazi wa Kiirani ni maradhi na ada mbaya ambayo humimina fedha na utajiri wa nchi katika mifuko ya wafanyakazi wa nchi za nje.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini ni sehemu ya juhudi kubwa za dharura katika mwaka huu wa Jihadi ya Uchumi. Ameongeza kuwa sambamba na wananchi kutumia bidhaa zilizozalishwa nchini, kuna udharura wa kuzidishwa ubora wa bidhaa hizo na kufikia kiwango cha kuridhisha.
Akifafanua wajibu na majukumu ya viongozi wa nchi katika mwaka huu, Ayatullah Ali Khamenei amelitaja suala la kutayarisha nafasi za kazi kuwa lina umuhimu mkubwa. Amesema kuwa kushughulikia miundombinu ya uchumi kote nchini na kutilia maanani kikamilifu suala la viwanda na kilimo ni miongoni mwa masuala muhimu sana na dhihirisho la jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu.
Katika sehemu ya mwisho ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia masuala ya Mashariki ya Kati na kufeli kwa maadui katika kukabiliana na Iran. Ameashiria njama za mara kwa mara za vyombo vilivyodhidi ya ubinadamu vya ubeberu kwa ajili ya kutoa pigo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na akasema mabeberu walitaka utawala wa Kiislamu ambao ni nembo ya adhama na utukufu wa Kiislamu na kibinadamu, usiwe kigezo kwa mataifa mengine kupitia njia ya kuitenga Iran; hata hivyo taifa la Iran na Jamhuri ya Kiislamu inapewa heshima kubwa na mataifa mengine katika wimbi la sasa la mapambano adhimu ya wananchi wa eneo hili, na serikali ya Marekani ndiyo inayochukiwa zaidi na mataifa hayo.
Ayatullah Khamenei amesema kushindwa njama za maadui na taufiki na mafanikio ya kila leo ya taifa la Iran ni alama ya kutimia ahadi ya Mwenyezi Mungu. Amesema taifa, serikali na viongozi wa Iran wataendeleza jitihada zao katika njia ya Mwenyezi Mungu na Yeye Mola Karimu ataendelea kuliteremshia rehma na baraka zake taifa hili.
Mwanzoni mwa mkutano huo Waziri wa Kazi na Masuala ya Jamii wa Iran Sheikhul Islami ametoa hotuba fupi akiashiria mchango mkubwa wa nguvu kazi ya binadamu katika maendeleo ya kiuchumi na akasema wizara hiyo ikishirikiana na wawakilishi wa wafanyakazi na waajiri imetayarisha Hati ya Taifa ya Ustahiki kwa lengo la kustawisha nafasi za kazi, kulinda wafanyakazi na kutetea haki za kazi na uzalishaji. Amesisitiza kuwa wizara hiyo imechukua hatua kubwa katika kurekebisha siasa, sheria na kanuni mbalimbali. 782395


captcha