IQNA

Ayatullah Khamenei:

Harakati ya mwamko itaendelea kusonga mbele hadi barani Ulaya

21:48 - May 04, 2011
Habari ID: 2117575
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei amesema harakati ya mwamko inayoshuhudiwa kwa sasa magharibi mwa Asia na kaskazini mwa Afrika ni muendelezo wa harakati adhimu ya taifa la Iran na kwamba harakati hiyo ya mwamko itasonga mbele hadi katikati mwa Ulaya.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei ameyasema hayo mapema leo Jumatano tarehe 04 Mei akihutubia hadhara kubwa ya maelfu ya walimu kutoka maeneo yote nchini na kuongeza kuwa kazi muhimu zaidi ya elimu na malezi ni kutayarisha wanadamu waliokufu na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na harakati kubwa ya taifa la Iran. Amesisitiza kuwa kwa msingi huo sekta ya elimu na malezi inapaswa kufanyiwa mabadiliko kwa mujibu wa kigezo huru na cha kisasa cha Kiirani na Kiislamu ambacho matokeo yake yatakuwa ni kutayarisha wanadamu wenye imani, wenye kutawakali kwa Mwenyezi Mungu, wenye izza, mashujaa, wabunifu, wenye subira na matumaini ya mustakbali mwema, wenye maadili na akhlaki njema na waliotayari kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za kuingia kwenye medani mpya.
Ayatullah Khamenei ambaye amehutubia hadhara hiyo kwa mnasaba wa kuadhimisha Siku ya Mwalimu hapa nchini na kumkumbuka Ustadh Shahidi Murtadha Muttahari, amesema Shahidi Muttahari alikuwa mwanadamu adhimu, aliyeona mbali na kuhisi matatizo ya watu. Amesema kuwa shakhsia huyo mkubwa aliyekuwa na sifa hizo alikuwa chanzo cha baraka nyingi katika nyanja za elimu, utamaduni na kutoa mafunzo na malezi na hatimaye Mwenyezi Mungu alimlipa mema kwa kupata daraja ya kuuawa shahidi na kubakia hai milele.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha mchango na nafasi ya mwalimu na akasema kuwa, mwalimu ni mtu ambaye mustakbali wa nchi na malezi ya watu adhimu, wapiganaji wa jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu na shakhsia watakaoongoza nchi yako mikononi mwake; kwa msingi huo wananchi wote wanapaswa kutambua thamani na umuhimu wa mwalimu na kumpa heshima yake. Amesisitiza kuwa vyombo vya habari na viongozi wa serikali pia wana nafasi kubwa katika kueleza na kuweka wazi nafasi na hadhi halisi ya mwalimu.
Ayatullah Khamenei ameashiria suala la marekebisho katika sekta ya elimu na malezi na kubainisha sababu ya kuwepo haja ya marekebisho hayo. Amesema, kwa kuwa mfumo wa sasa wa elimu umetoka nje ya nchi na haukuzingatia mahitaji, mazingira na utamaduni wa taifa la Iran, hapana budi kwamba sekta ya elimu na malezi inahitaji mabadiliko.
Ayatullah Ali Khamenei amesema, sharti la mabadiliko hayo ni kuwepo kigezo huru na cha kisasa cha Kiirani-Kiislamu ambacho lengo lake litakuwa ni kulea wanadamu kufu na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Amesisitiza kuwa iwapo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka kubeba bendera ya Uislamu na kutengeneza dunia na akhera yake na kuwa msaidizi, shahidi na mtoa bishara njema kwa mataifa mengine, inalazimika kulea wanadamu wenye imani, wanaomtegemea Mwenyezi Mungu, wenye hadhi, wabunifu, mashujaa, wakarimu na wenye vipawa vikubwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa sharti la kuweza kulea watu kama hao ni kutekeleza mafundisho ya Uislamu na maarifa ya Qur'ani.
Ayatullah Khamenei amesisitiza juu ya udharura wa kuainisha mwelekeo na dira katika marekebisho ya sekta ya elimu na akasema kuwa miongoni mwa masharti muhimu ya mabadiliko hayo ni kuwa na mtazamo mpana na mpango kamili na wa pande zote.
Amesema, kadiri uwekezaji katika sekta ya elimu na marekebisho ya sekta hiyo unavyokuwa mkubwa ndivyo matunda yake yanavyokuwa makubwa zaidi, kwa msingi huo wananchi wote wanapaswa kuiangalia sekta hiyo kwa mtazamo huo.
Akikumbusha kazi kubwa iliyofanywa na taifa la Iran chini ya uongozi wa hayati Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu) katika kipindi cha historia, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema nchi ya Iran inahitajia elimu na malezo yanayolingana na hadhi ya taifa hili.
Amebainisha pia harakati kubwa ya taifa la Iran na kusema, katika kipindi ambacho madola makubwa ya kibeberu duniani yalikuwa yakitumia uwezo na suhula zao zote dhidi ya thamani za Kiislamu na kibinadamu, taifa la Iran lilisimama peke yake kwa ajili ya kuhuisha thamani hizo na likapata mashaka mengi likiwa peke yake na sasa limepata ushindi na mafanikio makubwa.
Ayatullah Khamenei amesema harakati ya mwamko inayoshuhudiwa kwa sasa magharibi mwa Asia na kaskazini mwa Afrika ni muendelezo wa harakati adhimu ya taifa la Iran. Ameongeza kuwa bila shaka harakati hiyo ya mwamko itasonga mbele hadi katikati mwa Ulaya na mataifa ya bara hilo yatasimama kidete kupambana dhidi ya wanasiasa na watawala wao ambao wamewafanya wasalimu amri kikamilifu mbele ya siasa za kiutamaduni na kiuchumi za Marekani na Wazayuni.
Amesisitiza kuwa mwamko huo utashuhudiwa pia barani Ulaya na kusema, mwamko wa sasa ni harakati kubwa ya taifa la Iran na iwapo tunataka harakati hiyo iendelee kwa kasi kubwa zaidi, tunalazimika sambamba na kustawisha vipawa na kulea wanadamu wakakamavu, tuimarishe imani, muono wa mbali, maarifa na elimu na kutia nguvu umoja na mshikamano.
Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Ali Khamenei amesisitiza kuwa, kwa baraka za hima kubwa, imani madhubuti na watu wenye ikhlasi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itafanikiwa kukwea vilele vya saada na maendeleo kimoja baada ya kingine.
Mwanzoni mwa mkutano huo Waziri wa Elimu wa Iran Haji Babai ametoa hotuba fupi akieleza mipango na juhudi zilizofanyika kwa ajili ya mabadiliko ya kimsingi katika sekta ya elimu hapa nchini.786767

captcha