IQNA

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Jamhuri ya Kiislamu imezima njama za adui kwa kupiga hatua za maendeleo

22:00 - May 09, 2011
Habari ID: 2119497
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa mafia na zimwi la kipropaganda la adui limefanya kila liwezekanalo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tangu mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, lakini utawala wa Kiislamu umezima na kubatilisha njama hizo kivitendo kwa kupiga hatua za kimaendeleo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei ameyasema hayo leo akihutubia wawakilishi wa wananchi wa mkoa wa Kurdistan, familia za mashahidi, maulamaa na viongozi wa mkoa huo. Ameutaja mkoa wa Kurdistan kuwa ni ardhi ya elimu, fasihi na sanaa, usafi wa moyo na uaminifu, ushujaa na uungwana. Amesema kuwa taifa la Iran limeweza kufikia nafasi ya juu zaidi kuliko huko nyuma katika masuala ya kisayansi, kijamii, hadhi ya kisiasa na ya kitaifa.
Ayatullah Khamenei ameitaja safari aliyofanya miaka miwili iliyopita katika mkoa wa Kurdistan kuwa ilikuwa na mafanikio, ya kuvutia na yenye kumbukumbu nyingi. Ameashiria mapokezi makubwa na ukarimu wa wananchi wa eneo hilo na kuongeza kuwa mapenzi na uaminifu wa wananchi wa Kurdistan kwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ni wa aina yake na unashuhudiwa kwa nadra mno katika maeneo mengine.
Ameashiria pia mashinikizo ya baadhi ya makundi na anga ya hofu na woga iliyoanzishwa na makundi hayo katika eneo la Kurdistan katika kipindi cha mwanzoni mwa Mapinduzi ya Kiislamu na akasema, wananchi wa Kurdistan daima wameonyesha uaminifu wao kwa utawala wa Kiislamu hapa nchini na sifa hiyo yenye thamani haijaathiriwa na propaganda tata zinazofanywa na adui.
Ayatullah Ali Khamenei amewapongeza maulamaa na wakuu wa Kurdistan hususan Shahidi Sheikhul Islam na Bwana Mujtahidi na akasema kuwa maadui wa umoja wa kitaifa na maendeleo ya nchi hii walishindwa kustahamili ukweli na mafanikio ya safari ya Kurdistan kwa msingi huo waliamua kulipiza kisasi kwa kumuua shahidi na kwa njia ya uovu shakhsia huyo mkubwa.
Amesisitiza pia juu ya udharura wa kuandikwa historia ya mashahidi na maulamaa wa Kurdistan waliouawa katika njia ya umoja na fahari ya taifa.
Ayatullah Khamenei ameashiria kukiri kwa adui kuhusu uwezo mkubwa, hadhi na nafasi aali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika eneo la Mashariki ya Kati na akasema, mafia na zimwi la kipropaganda la adui limefanya kila liwezekanalo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu tangu mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, lakini utawala wa Kiislamu umezima na kubatilisha njama hizo kivitendo kwa kupiga hatua za kimaendeleo.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: "Sasa jina la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na malengo yake vinatajwa kwa fahari na adhama kati ya mataifa mbalimbali na nchi hii ina hadhi na heshima kubwa katika nyoyo za mataifa hayo."
Amesema nguzo ya maendeleo na ustawi wa Iran ni harakati ya bidii na juhudi kubwa zaidi, ya Kiislamu, yenye kushikamana na ibada na yenye muono wa wazi. Amesema kuwa taifa la Iran limefikia maendeleo hayo licha ya upinzani wa maadui na hali ya sasa ya Iran inatoa bishara ya mustakbali mwema.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia 'Mwongo wa Uadilifu na Maendeleo' hapa nchini na akasema kuwa nchi hii ina sifa ya mshikamano, maendeleo na ari ya kufanya harakati kubwa ya kisayansi. Amesisitiza kuwa kumefanyika kazi kubwa mno katika medani ya kutekeleza uadilifu hapa nchini.
Amesisitiza pia juu ya udharura wa kila mkoa kutoa mchango wake katika maendeleo ya taifa na akasema kuwa kila mkoa unapaswa kutoa hisa yake katika mashindano chanya ya jitihada kubwa za maendeleo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametilia mkazo juu ya udharura wa kutumiwa vipawa vya vijana wa Kurdistan na kutayarisha nafasi za kazi kwa ajili ya vijana hao. Amesema kuwa Kurdistan ni mkoa hai na wenye harakati na amewataka viongozi na wakuu wa mkoa huo kuwajali zaidi vijana.
Mwanzoni mwa mkutano huo mwakilishi wa Faqihi Mtawala katika mkoa wa Kurdistan Hujjatul Islam Walmuslimin Sayyid Muhammad Husseini Shahrudi amekumbusha mafanikio ya safari ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mkoa huo na mazungumzo yake na wananchi waaninifu na akasema, wananchi wa Kurdistan wamepiga hatua kubwa katika njia ya maendeleo na ustawi wa taifa kwa umoja na mshikamano wao na wamefanikiwa kubatilisha na kuzima njama za adui. 788893

captcha