Ameyasema hayo katika kikao cha pili cha fikra za kiistratijia katika Jamhuri ya Kiislamu kilichofanyika Jumanne asubuhi, Mei 17, 2011. Kikao hichi kilikuwa cha kubadilishana mawazo na fikra kati ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na makumi ya wanafikra, wasomi, wahadhiri na watafiti wa Vyuo Vikuu na Hawza (Chuo Kikuu cha kidini).
Mwanzoni mwa kikao hicho kilichodumu kwa muda wa masaa manne, watu 10 kati ya wasomi, wanafikra na watu muhimu katika jamii wametoa mitazamo na fikra zao kwa awamu mbili kuhusiana na misingi, maana, vipengee, utekelezaji na mambo ya dharura ya suala zima la uadilifu.
Kikao cha kwanza cha fikra za kiistratijia katika Jamhuri ya Kiislamu kilifanyika mwezi Disemba mwaka jana kikiwa na maudhui ya "Kigezo cha Maendeleo ya Kiislamu-Kiirani."
Miongozo ya Kiongozi Muadhamu katika Kikao hicho
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza katika kikao hicho ya fikra za kiistratijia juu ya udharura wa kufanyika juhudi na bidii za dhati na kutumiwa fikra tofauti za wasomi na wanafikra kwa ajili ya kupatikana nadharia safi ya Kiislamu kuhusiana na uadilifu. Vile vile amesema, kazi zilizofanyika katika upande wa kuleta uadilifu wa kijamii nchini Iran katika kipindi cha miaka 30 iliyopita ni nzuri lakini amesisitiza pia kuwa licha ya kuweko juhudi za kutekeleza uadilifu nchini hivi sasa lakini hali iliyopo si ya kuridhisha kabisa kwani inachotaka Jamhuri ya Kiislamu ni kutekeleza uadilifu kwa kiwango cha juu kabisa na kusimamisha uadilifu kikamilifu yaani uadilifu wenye maana ya kutekeleza matukufu na thamani mutlaki za uadilifu katika pande zake zote.
Amesema fikra zilizotolewa katika suala hilo ni muhimu na zenye faida sana na kuongeza kuwa, kikao cha leo ni mwanzo tu wa kufanyika kazi kubwa zaidi. Amesema ana matumaini kuwa suala la uadilifu litakuwa ni ajenda kuu ya watu muhimu na wenye vipaji nchini hasa kwa kuzingatia idadi kubwa ya wasomi na wanafikra waliopo katika kila pembe ya Iran. Amesema anatumai juhudi za kusimamisha uadilifu zitaendelea na kufuatiliwa vile inavyotakiwa ili hatimaye ziweze kuzaa matunda bora.
Amesema, suala la kusimamisha uadilifu ndicho kilio cha siku zote cha mwanaadamu na huku akiashiria fikra za wasomi mbali mbali waliozungumzia suala la uadilifu katika vipindi tofauti vya historia amesema, uchunguzi wa kina unaonesha kuwa, licha ya kuweko fikra nyingi tofauti za wasomi kuhusiana na uadilifu, lakini nafasi ya dini za Mwenyezi Mungu katika suala hilo ni ya kipekee na haina mfano wake.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ushahidi kwa kutumia aya za Qur'ani Tukufu na kusisitiza kuwa, kusimamisha uadilifu ndilo lengo kuu la dini za Mwenyezi Mungu. Ameongeza kuwa, uadilifu ndilo lengo la mfumo wa kijamii unaokusudiwa na dini za Mwenyezi Mungu katika kumfanya mwanaadamu aishi kwa mujibu wa mafundisho ya kidini na umuhimu huu mkubwa ambao dini inalipa suala la uadilifu haupatikani katika aidiliojia na vyuo vyote vya fikra za kibinaadamu.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa ufafanuzi zaidi kubainisha tofauti iliyopo baina ya fikra za dini na aidiliojia zinazotolewa na wanaadamu kuhusu uadilifu akisema, mbali na Manabii na Mitume wa Mwenyezi Mungu kubainisha na kufundisha uadilifu, walipambana kivitendo pia na mataghuti na madhalimu kwa ajili ya kusimamisha uadilifu na siku zote walikuwa wakiwaunga mkono watu wanaodhulumiwa na walisimama imara kupambana na madhalimu, lakini aidiolojia zinazotolewa na wanaadamu kuhusu uadilifu, zinaishia kwenye maneno tu.
Amesmea itikadi ya dini zote za Mwenyezi Mungu kuhusiana na historia ya mwanaadamu ni kumalizikia kwenye kusimamishwa uadilifu na hiyo ni tofauti nyingine iliyopo kati ya fikra za dini na aidiliojia za wanaadamu kuhusiana na uadilifu. Ameongeza kuwa, wakati wote dini za Mwenyezi Mungu zinazungumzia suala la uadilifu katika safari yote ya tangu kuumbwa mwanaadamu hadi kufikia mwisho wa maisha yake yaani siku ya kiama na kurejea kwa Mola Mwenyezi lakini hilo halionekani kwenye aidiliojia zinazotolewa na wanaadamu ni hilo ni jambo jengine la kipekee linaloshuhudiwa katika fikra za dini ya Mwenyezi Mungu kuhusiana na uadilifu.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, ni kutokana na mtazamo huo wa dini ndio maana suala la uadilifu likazingatiwa sana na Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran tangu yalipopata ushindi na ndio maana uadilifu ukapewa umuhimu wa kipekee katika kaulimbiu za taifa - Katiba - katika miongozo na fikra za Imam Khomeini (quddisa sirruh) na katika kipindi chote cha miaka 32 ya umri wa Jamhuri ya Kiislamu na kufanya kuwa ni matukufu mutlaki ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kusimamisha uadilifu kuwa ndiyo ajenda kuu ya kila siku ya Jamhuri ya Kiislamu na huku akiashiria juu ya kazi nyingi sana zilizofanywa katika suala zima la kusimamia uadilifu wa kijamii nchini ameongeza kuwa, licha ya kufanyika kazi kubwa katika uwanja huo lakini bado haitoshi kwani kwa mtazamo wa Uislamu, lengo na shabaha kuu ni kusimamisha kikamilifu uadilifu na kuangamiza kikamilifu dhulma hivyo inabidi kazi kubwa zaidi na ya pande zote ifanyike kwa ajili ya kupunguza pengo kubwa lililopo hadi kufikia kwenye kusimamisha uadilifu unaotakiwa wa kijamii.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria sisitizo kubwa linalotolewa na Jamhuri ya Kiislamu hivi sasa kuhusiana na suala zima la kupatikana nadharia safi ya Kiislamu kuhusiana na uadilifu na kuongeza kuwa, hadi sasa kumetolewa maana nyingi za jumla kuhusiana na uadilifu lakini kinachotakiwa kufanyika hivi sasa ni kuongeza bidii kufanikisha uadilifu kwa maana ya kisasa itakayokuwa na faida wakati wote katika nyanja na sekta zote nchini na iwe ndiyo marejeo ya watu muhimu nchini, viongozi na wananchi hususan vijana katika mambo yao yote.
Akifafanua zaidi kuhusiana na lengo la kufanyika kikao cha fikra za kiistratijia kuhusiana na uadilifu amesema, inabidi kupatikane mbinu na njia mpya za kuweza kupunguza pengo lililopo hivi sasa hadi kufikia kwenye kiwango cha juu cha uadilifu na jambo hilo halitawezekana ila kwa kuweko fikra na mitazamno inayolingana.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa kipindi cha kufanyia majaribio na kufanya makosa katika suala la utekelezaji wa uadilifu kimeshapitwa na wakati na kukumbusha kuwa, katika kipindi cha miaka 32 iliyopita, utekelezaji wa uadilifu umefanyiwa majaribio mengi katika mambo tofauti nchini lakini kuanzia sasa na kuendelea inabidi utekelezaji wa uadilifu nchini ufanyike kwa njia makini zilizodurusiwa vyema.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la harakati ya Iran katika njia ya maendeleo ya haraka na ya kimapinduzi kuwa ni sababu nyingine inayoongeza umuhimu wa kutekelezwa uadilifu kwa umakini mkubwa na kuongeza kuwa, kuendelea harakati hiyo yenye kasi kubwa kunahitajia kuchukuliwa maamuzi makubwa na mazito na kama maamuzi hayo yatachukuliwa bila kuzingatiwa uadilifu na mfungamano uliopo baina ya uadilifu na maendeleo, basi hasara itakayopatikana itakuwa kubwa sana.
Aidha amesema: Lengo letu ni kufikia kwenye nadharia safi na halisi ya Uislamu kuhusiana na uadilifu na ili kuweza kufikia kwenye lengo hilo muhimu mno, inabidi turejee kwenye mafundisho ya Kiislamu tukiwa na mtazamo wa kibunifu na wa kina sana ili kwa kutumia njia na mbinu maalumu katika jambo hilo, tuweze kupata nadharia halisi, safi na bora kabisa kuhusu uadilifu.
Amesisitiza kuwa, inabidi kujiepusha kikamilifu na nadharia za kuokota na za kuigiza, bali nadharia hiyo inabidi itoke kikamilifu kwenye marejeo halisi na yenye itibari ya Uislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, maana ya uadilifu katika kila chuo cha kifikra hutokana na misingi mikuu ya chuo hicho na kuongeza kuwa: Ni kwa sababu hiyo ndio maana suala la kutoa nadharia ya Kiislamu kuhusu uadilifu halipaswi kutegemea chuo chochote kingine cha kifikra ghairi ya Uislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei amefafanua zaidi akisema: Uadilifu katika Uislamu unatokana na misingi ya haki na kwamba suala la kupigania usawa na uadilifu ni jukumu la kidini katika Uislamu wakati ambapo jambo hilo halishuhudiwi katika aidiolojia za kibinaadamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, ni jambo muhimu sana kuweko fikra zinazokwaruzana katika kazi ya kupata nadharia sahihi na safi ya Uislamu kuhusu uadilifu. Ameongeza kuwa, mtu yeyote pia hapaswi kudhani kuwa lengo lake Kiongozi Muadhamu ni kutaka kutumiwa mitazamo yake kuhusu suala hilo, bali anachosisitiza yeye ni umuhimu wa kuweko fikra zinazokwaruzana na kupingana kielimu katika jambo hilo ili natija yake iwe ni kupatikana nadhari bora na sahihi kabisa.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa: Fikra za kielimu zinazokinzana katika suala hilo inabidi ziendelee kuwepo hata baada ya kupatikana nadharia safi na halisi ya Uislamu kuhusu uadilifu.
Ameongeza kuwa, inabidi juhudi kubwa zifanyike katika suala hilo ili kuweze kupatikana fikra jumla, moja, makini na iliyosimama juu ya hoja madhubuti kuhusu uadilifu ili kuweze kuandaliwa mipango ya muda mrefu kwa kutegemea mambo hayo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, baada ya kupatikana fikra hiyo jumla itabidi kufanyike utafiti mwingine mpya wa kipekee kuhusu njia za matumizi na mbinu za utekelezaji wa nadharia hiyo na hapa panaweza kutumika fikra na uzoefu wa watu wengine katika kufanikisha hatua hiyo.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema ni jambo la dharura pia kuweko somo la uchunguzi na utafiti wa uadilifu katika Vyuo Vikuu na Hawza kwani jambo hilo linaweza kuhesabiwa kuwa ni uwezekaji mzuri na wenye faida kubwa wa kuweza kutia nguvu fikra ya uadilifu na kulea nguvu kazi bora. Ameongeza kuwa, kazi nyingine muhimu katika suala hilo ni kupatikana kigezo na kielelezo cha kupimia kiwango wa utekelezaji wa uadilifu wa kijamii.
Amekumbusha kuwa, baadhi ya vielelezo vinavyotolewa kwenye nadharia za Magharibi vinaweza kutumika katika baadhi ya sehemu maalumu lakini vielelezo vilivyo vingi vya Magharibi ni pungufu na vingi vyake ni ghalati na ni makosa kikamilifu, hivyo inabidi kuwa na vielelezo huru kwa ajili ya kusimamisha uadilifu kwa kutegemea fikra na mtazamo wa Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema, ni jambo la wajibu na la dharua kwa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) na Baraza la Kulinda Katiba nchini kuzingatia vilivyo uadilifu katika kila hatua inayochukuliwa katika utungaji sheria na kuongeza kuwa, inabidi kazi kubwa ifanyike kwa ajili ya kutekeleza uadilifu wa kijamii kwa namna inayotakiwa.
Ameongeza kwamba, kuwa na imani na siku ya Kiyama na kuamini kuwa matendo yote ya wanaadamu yataonyeshwa na kuhesabiwa siku ya Kiyama huwaongezea nguvu na nishati watu wanaopigania uadilifu na kwa hakika haiwezekani kabisa kusimamisha uadilifu wa kweli katika jamii ambayo haiamini misingi ya siku ya Kiyama na kwenda kuhesabiwa amali za watu.
Ameongeza kuwa, kama kila mtu atakuwa na mtazamo wa kiadilifu kuhusu nafsi yake mwenyewe basi jambo hilo humfanya ajiweke mbali na madhambi na kupata nguvu za ucha Mungu na kunyenyekea mbele ya Mwenyezi Mungu na kwamba jambo hilo linasaidia sana katika kusimamia uadilifu wa kijamii.
Hotuba na Makala za Wanafikra
Hiotuba ya kwanza katika kikao hicho cha fikra za kiistratijia imetolewa na Dk. Husain Ivazlou, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Imam Sadiq AS. Dk. Ivazlou amesema kuhusu maana na vielelezo vya uadilifu wa kijamii na kiuchumi katika fremu ya kigezo cha maendeleo ya Kiislamu-Kiirani kwamba maana ya uadilifu wa kijamii ni kwamba kila mtu katika jamii aweze kupata haki anayostahiki kutokana na juhudi zake.
Msomi huyo wa Chuo Kikuu ameongeza kuwa, suala la kuwa na haki sawa katika vyanzo vya utajiri wa taifa hupimwa kwa mizani ya ushiriki wa watu katika uzalishaji na amelitaja suala la kutumika fedha na mali za uma katika njia sahihi kuwa ni katika vielelezo na vigezo vya uadilifu kwa mtazamo wa Uislamu.
Hujjatul Islam Walmuslim Abul Qasim Alidoust, mjumbe katika jopo la wahadhiri wa Hawza (Chuo Kikuu cha kidini) ya Qum ni mwanafikra mwingine ambaye ametoa fikra zake katika kikao cha pili cha Fikra za Kiistratijia katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na amezungumzia vipengee mbali mbali vya uadilifu kama hati, msingi, fikra na maana jumla inayoweza kutumika katika kugundua na kutekeleza hukumu na sheria za Kiislamu.
Mhadhiri huyo wa Hawza na Chuo Kikuu amesema: Si sahihi kulichukulia suala la uadilifu kwa uzito mwepesi bali suala hilo muhimu inabidi kuamiliana nalo kiutaalamu ili kwa njia hiyo liweze suala hilo kuwa ni marejeo na fikra kuu.
Hujjatul Islam Walmuslimin Alidoust amesema, uadilifu ni msingi na usuli katika fikihi na kuongeza kuwa: Uadilifu unapaswa kuhesabiwa kuwa ni kielelezo katika kuelewa dalili na kutoa hukumu za kidini, na katika kutekeleza hukumu za dini pia, uadilifu ni kielelezo na msingi unaosimamia matendo na maneno ya viongozi na watendaji.
Hotuba ya tatu katika kikao cha pili cha Fikra za Kiistratijia katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetolewa na Dk. Fahima Farahmandpour, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tehran. Dk. Farahmandpour ametoa mada iliyolenga kwenye mahitaji na fikra ya uadilifu wa kijinsia kwa mtazamo wa dini na kusema: Si sahihi kuupima uadilifu kwa kuangalia mgawanyo wa idadi ya fusa na kazi bali mtazamo sahihi kuhusu uadilifu unapaswa kupimwa kwa kuangalia tofauti za kimaumbile baina ya mwanamme na mwanamke.
Ameongeza kuwa, ustahiki wa watu ndio unaopaswa kuwa kigezo cha kutekelezea uadilifu hususan katika kazi za kitaalamu na kuna haja ya kuangaliwa upya kigezo kinachotumika hivi sasa nchini katika kuwapatia kazi watu wanaomaliza masomo ya Vyuo Vikuu.
Hujjatul Islam Walmuslimin Sayyid Abbas Nabavi, Mhadhiri katika Hawza na Chuo Kikuu alikuwa mzungumzaji wa nne katika kikao hicho na huku akiashiria juu ya amri iliyosisitizwa mno na Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu kuhusu kusimamisha usawa na uadilifu amesema: Sambamba na kutoa fikra na mitazamo kuhusiana na uadilifu, inabidi kutolewe pia vielelezo vya kuweza kupima utekelezaji wa uadilifu.
Hujjatul Islam Walmuslimin Nabavi ametaja suala la usawa katika kutoa fursa, kustawisha uwezo wa nchi na kutumiwa vizuri uwezo wa taifa kuwa ni vielelezo vitatu muhimu katika uadilifu wa kijamii na kuongeza kuwa, inabidi uadilifu wa kijamii uwe msingi wa masuala ya kijamii na amelisisitizia sana suala la kuwa na mipango makini ya ustawi pamoja na misingi madhubuti ya kuboresha utamaduni wa watu na kuongeza kuwa, inasikitisha kuona vyombo vilivyopewa jukumu la kusimamia utamaduni wa uma havilipi umuhimu unaotakiwa suala hilo kiasi kwamba hivi sasa Kiongozi Muadhamu na Jumuiya ya Wanachuo ndio wanaofuatilia suala hilo.
Mhadhiri huyo wa Hawza na Chuo Kikuu amesisitiza kuwa, katika Kigezo cha Maendeleo ya Kiislamu-Kiirani, suala la uadilifu lina umuhimu mkubwa sana na inabidi lizingatiwe ipasavyo katika masuala yote.
Mzungumzaji wa tano katika kikao cha pili cha Fikra za Kiistratijia katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu suala la uadilifu alikuwa ni Sayyid Muhammad Mir Sendusi, Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Imam Husain AS. Dk. Sendusi ameashiria misingi ya nadharia mbili kuu kuhusu uadilifu yaani ustahiki na mahitaji na kusema: Inabidi katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwe na nadharia inayokusanya mambo yote ambayo itaweza kuzingatia mahitaji yote ya watu na wakati huo huo izingatiwe kuwa, njia kwa ajili ya kutumiwa watu kulingana na ustahiki na juhudi zao nayo iko wazi.
Ameashiria suala la kukosekana nadharia moja na ya wazi kuhusu maana ya uadilifu nchini na kuongeza kuwa, ni kwa sababu hiyo ndio maana kila kiongozi anayeingia madarakani huzungumzia suala la uadilifu kwa mtazamo wake jambo ambalo baadhi ya wakati mtu anaweza kutofautiana na wenzake na wakati mwingine hata kukinzana nao kabisa.
Sehemu ya pili ya kikao hicho cha Fikra za Kiistratijia katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu uadilifu kimejadili suala la uadilifu na utekelezaji wake. Mwanzoni mwa sehemu hiyo, Hujjatul Islam Walmuslimin Sayyid Abbas Musaviyan, Mhadhiri katika Hawza amejadili nafasi ya uadilifu wa kiuchumi katika mfumo wa benki ya Kiislamu. Amesema, kugawanywa vyanzo vya benki ni fursa ya kiuadilifu katika kupambana na umaskini na inabidi suala la uzalishaji wa nafasi za kazi na kuongezeka suala la kutengwa vyanzo vya benki kwa sura bora, lipewe mazingatio yanayotakiwa.
Dk. Musaviyan amelitaja suala la kutengwa vyanzo kwa ajili ya miradi yenye faida zinazokuwa na kuongezeka, kugawanywa kwa mizani sawa vyanzo hivyo na kugawanywa kiuadilifu faida, kuwa ni miongoni mwa misingi na vigezo vya kugawanywa kiuadilifu vyanzo vya benki. Amesema, mfumo wa benki inabidi ujiepushe na faida za pembeni na uwe na faida ya kweli ya hesabu za benki.
Msemaji wa pili katika sehemu ya pili ya kikao hicho alikuwa ni Dk. Ilyas Naderian, Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Tehran.
Katika makala yake amezungumzia matatio ya kiuchumi na kijamii akisema kuwa, ingawa misimamo na hatua zilizochukuliwa nchini Iran kuhusu utekelezaji wa uadilifu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu zimesaidia katika kugawanywa vizuri mali za uma licha ya kuwepo matatizo ya hapa na pale lakini inabidi kazi kubwa zaidi ifanyike kwa ajili ya kuepusha matatizo katika siku za usoni.
Makala ya tatu katika sehemu ya pili ya kikao cha pili cha Fikra za Kiistratijia katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kilichohusiana na suala la uadilifu imezungumzia suala la uadilifu baina ya kizazi na kizazi kingine katika kutumia maliasili za umma. Makala hiyo imetayarishwa na kutolewa na Hujjatul Islam Said Farahanifar, Mhadhiri katika chuo cha Sayansi ya Kiuchumi.
Mchumi huyo amesema, kuainishwa kiuadilifu milki za serikali na umma katika utajiri wa maliasi, kuwa na mipango sahihi ya mgao wa awali wa maliasili na sherikali kuchukua hatua zinazotakiwa kwa ajili ya kulinda maliasili ni miongoni mwa misingi muhimu ya kusimamisha uadilifu baina ya vizazi mbali mbali katika kutumia maliasili za nchi. Amesema, kwa mtazamo wa Uislamu, serikali ina nafasi ambayo inaweza kufuatilia na kusimamisha uadilifu kwa kusimamia matumizi mazuri ya maliasili za nchi.
Dk. Majid Yasouri ni miongoni mwa waliotoa hotuba zao katika kikao hicho. Dk. Yasouri ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Gilan na amesema katika makala yake kwamba uadilifu wa mazingira ni njia nzuri ya kuleta ustawi wa kudumu wa taifa na kuongeza kuwa, vyanzo na mali za taifa katika maeneo tofauti ya kijiografia inabidi yagawanywe kiuadilifu kulingana na mahitaji ili kupunguza mwanya na pengo la kiuchumi na kijamii katika sekta mbali mbali nchini na ili watu waweze kuishi kwa raha na ustawi hata katika maeneo yaliyo nyuma kimaendeleo.
Mzungumzaji wa 10 na wa mwisho katika kikao cha pili cha Fikra za Kiistratijia katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambacho kimekuwa maalumu kwa ajili ya suala uadilifu alikuwa ni Dk. Muhammad Javad Larijani, Mhadhiri wa Chuo Kikuu. Ametoa mada iliyobeba anwani: "Hali ya Uadilifu na Haki za Binaadamu katika Upeo wa Kimataifa." Katika mada hiyo, Dk. Larijani ametoa ufafanuzi kuhusu misingi ya uadilifu katika mfumo wa kiliberali wa Magharibi na kuipima na misingi ya uadilifu katika dini tukufu ya Kiislamu.
Sehemu moja ya kikao cha pili cha Fikra za Kiistratijia katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa maalumu kwa ajili ya kuulizwa na kujibiwa maswali ya wasomi na wanafikra kuhusiana na mitazamo iliyotolewa.
Wahadhiri, watafiti na wasomi waliotoa mada zao katika kikao hicho wametumia fursa hiyo kujibu maswali yaliyoulizwa.
Mwanzoni mwa kikao hicho, Dk. Sadiq Vaizzadeh, katibu wa kikao hicho ameashiria ufuatiliaji wa maudhui ya kikao cha kwanza cha fikra za kiistratijia na kusema kuwa, hatua za awali za kuanzisha kituo cha kufuatilia na kusimamia ufanikishaji wa masuala yanayohusiana na Kigezo cha Maendeleo cha Kiislamu-Kiirani zimeshachukuliwa na kituo hicho kitakuwa na uwezo kamili na suhula zote zinazotakiwa kwa ajili ya kuandaa kigezo hicho cha kiistratijia.
Dk. Vaizzadeh ametoa maelezo na ufafanuzi kuhusu malengo ya kikao cha pili cha fikra za kiistratijia na kuahidi kkuwa, kutafanyika juhudi kubwa za kuandaliwa nadharia ya uadilifu kwa kutumia maelezo yaliyotolewa kwenye kikao hicho cha pili na kwa kustafidi na uwezo mkubwa uliopo nchini.
Mwishoni mwa kikao hicho, Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amewasalisha hadhirina sala za jamaa za Adhuhuri na Alaasiri.
793711