IQNA

Mwamko wa Kiislamu kamwe hautazimwa

12:59 - May 21, 2011
Habari ID: 2125311
Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya Tehran amesema mwamko wa Kiislamu kamwe hautazimwa na kwamba madola ya kibeberu yatatumbukia katika kinamasi kadiri siku zinavyosonga mbele.
Ayatullah Mohammad Emami Kashani ameongeza kuwa badala ya mashirika ya kimataifa kuondoa dhulma na ukosefu wa uadilifu yanachukua hatua dhidi ya wanaodhulumiwa. Amesema vitendo kama hivyo vinaibua ukosefu wa matumani katika jamii ya mwanadamu.
Akihutubia maelfu ya waumini katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Tehran, Ayatullah Kashani ameashiria matukio kadhaa ya kieneo na hasa matukio ya Bahrain. Amesema matukio hayo ni mtihani mkubwa kwa Waislamu ambao utabainisha ni kiasi gani watawasaidia wanaodhulumiwa na kiasi gani walivyo na ubinafsi.
Ayatullah Kashani ameukumbusha ulimwengu wa Kiislamu kuwa una jukumu la kusubiri kudhihiri Imamu Mtoharifu wa 12 katika Nyumba ya Mtume wa Uislamu SAW, Imam Mahdi, Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake. Amesema kwa kuzingatia hilo, harakati za mwamko zinapata nguvu na ukosefu wa matumaini unaangamia kwani Mwenyezi Mungu yuko pamoja na waliodhulumiwa.
Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran amewataka maulamaa wa kidini kuchukua tahadhari kufuatia vurugu zinazozushwa na Wazayuni na madola ya kibeberu yakiongozwa na Marekani. Amesema Maulamaa wanapaswa kutetea uadilifu kwani kupitia sauti zao, mwamko wa Kiislamu unapata nguvu.
Kwingineko katika hotuba yake, Ayatollah Kashani ameashiria Mkutano wa Pili wa Fikra za Kistratijia nchini Iran uliofanyika katika kikao kilichohudhuriwa na Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei. Amesema nadharia ya uadilifu inapaswa kuzingatiwa, kufafanuliwa na kutekelezwa kivitendo kwa msingi wa kimataifa wa Kiislamu.

795097
captcha