IQNA

Ayatullah Ali Khamenei:

Tunapaswa kukosoa mitazamo isiyokuwa sahihi ya Magharibi kuhusu masuala ya wanawake

12:59 - May 23, 2011
Habari ID: 2127047
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Ali Khamenei amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapaswa kushambulia na kukosoa vikali, waziwazi na bila ya kusita misingi isiyokuwa sahihi ya Magharibi kuhusu suala la mwanamke na kutekeleza majukumu yake katika kutetea nafasi na hadhi halisi ya wanawake.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei mapema Jumapili tarehe 22 Mei alihutubia mjumuiko mkubwa wa wasomi wa kike wa vyuo vikuu, vyuo vya kidini na wataalamu wa nyanja mbalimbali akimtaja mwanamke katika mtazamo wa Kiislamu kuwa ndiye mkuu wa nyumba na ua la mrehani katika familia. Ayatullah Khamenei ameashiria mgogoro wa mwanamke katika jamii za Magharibi na akasema, katika mfumo wa Kiislamu wa Iran kumefanyika kazi nyingi kwa ajili ya kuhuisha nafasi halisi ya mwanamke lakini hadi sasa kuna matatizo mengi hasa kuhusu jinsi ya kuamiliana na mwanamke katika familia, matatizo ambayo yanapaswa kutatuliwa kwa kubuni na kutekeleza sheria.
Katika mkutano huo uliofanyika kwa mnasaba wa kukaribia maadhimisho ya siku ya kuzaliwa Bibi wa wanawake wa duniani na akhera Fatima al Zahra (as) ambayo imepewa jina la Siku ya Mwanamke nchini Iran, Ayatullah Khamenei ametoa mkono wa heri na baraka za siku hiyo kwa Waislamu wote na kusema kuwa kufanyika kikao hiki kinachohudhuriwa na wasomi na wanafikra wa kike hapa nchini na mtazamo wao wa kina kuhusu masuala mbalimbali likiwemo suala la wanawake na familia, ni ishara ya harakati adhimu ya wanawake kuelekea kwenye ukamilifu. Amesisitiza kuwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umefanikiwa kulea wanawake wasomi na wanafikra katika masuala muhimu mno ya jamii.
Amesema kuwa chanzo cha matatizo ya dunia ya sasa kuhusu suala la mwanamke ni mtazamo usiokuwa sahihi wa Magharibi kwa nafasi na hadhi mwanamke katika jamii na ufahamu potofu kuhusu maudhui ya familia. Ameongeza kuwa matatizo hayo mawili yamelifanya suala la mwanamke kuwa mgogoro duniani.
Akifafanua zaidi kuhusu mtazamo wa kidhalimu wa Magharibi kwa mwanamke, Ayatullah Ali Khamenei amesema, katika mtazamo usiokuwa sahihi ambao unahubiriwa na kuenezwa taratibu na nchi za Magharibi katika jamii mbalimbali, wanadamu wamegawanywa katika sehemu mbili, upande wa wanaume ambao ndio wenye maslahi na unaofaidika na upande wa wanawake unaotumiwa na kufaidiwa.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: "Kwa mujibu wa mtazamo huo usiokuwa sahihi, iwapo mwanamke anataka kudhihiri na kupata shakhsia na hadhi yake analazimika kuwa na mwenendo anaoutaka na kuuridhia mwanaume, yaani mwenye maslahi na anayefaidika; udhalilishaji huu ndiyo dhulma kubwa zaidi katika haki ya wanawake."
Ayatullah Khamenei ameashiria juhudi zinazofanyika kwa mpangilio maalumu na hatua kwa hatua za wapangaji wa siasa za kistratijia huko Magharibi kwa ajili ya kueneza utamaduni huo potofu katika fikra za mataifa mbalimbali na akasema kuwa kwa sababu hiyo hii leo iwapo mtu atalaani mwenendo na tabia ya kudhihirisha mvuto wa kike katika mazingira ya umma basi atashambuliwa na kuzushiwa makelele mengi na vyombo vya kipropaganda na kisiasa vya nchi za Magharibi.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa upinzani wa waziwazi wa vazi la hijabu katika nchi za Magharibi ni miongoni mwa matokeo ya mtazamo wa kidhalimu kwa kadhia ya mwanamke. Ameongeza kuwa Wamagharibi wanadai kuwa vazi la hijabu ni suala la kidini ambalo halipasi kuonekana katika jamii isiyokuwa ya kidini; hata hivyo sababu halisi ya upinzani wa Magharibi dhidi ya hijabu ni kuwa inazuia na kutoa changamoto kwa siasa za kistratijia na kimsingi za Magharibi kuhusu mwanamke, yaani kuwafanya wanawake wawe mafisadi na asherati.
Ayatullah Khamenei ameashiria ripoti za vituo rasmi vya kimataifa na akasema kudhoofika kwa misingi ya familia, ustawi wa biashara chafu, ya kuaibisha na kuhuzunisha ya wanawake, ongezeko la wana haramu na tabia ya mwanamke na mwanaume kuishi pamoja bila ya kufunga ndoa ni miongoni mwa matunda maovu ya mtazamo wa Magharibi unaotumia vibaya kadhia ya mwanamke. Ameongeza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapaswa kushambulia na kukosoa vikali, waziwazi na bila ya kusita misingi isiyokuwa sahihi ya Magharibi kuhusu suala la mwanamke na kutekeleza majukumu yake katika kutetea nafasi na hadhi halisi ya wanawake.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja mtazamo usiokuwa sahihi kuhusu taasisi ya familia kuwa ni tatizo la pili linalosababisha migogoro katika suala la wanawake kwenye jamii za Magharibi.
Ayatullah Khamenei amesema, kinyume na Magharibi, mtazamo wa Uislamu kuhusu familia na nafasi ya mwanamke uko wazi kabisa na Mtume Muhammad (saw) na Maimamu watohaifu katika kizazi chake wamesisitiza mno juu ya nafasi hiyo ya juu ya familia na mwanamke.
Amesisitiza kuwa kutekelezwa mtazamo na matakwa ya Uislamu kuhusu mwanamke na familia kunahitajia msaada wa sheria na dhamani ya utekelezaji wake. Ameongeza kuwa licha ya kazi kubwa iliyofanyika baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran lakini bado kuna mapungufu mengi kuhusu suala la mwanamke na mwenendo wa watu katika familia, mambo ambayo yanapaswa kuondolewa.
Amesema mazingira ya familia yanapaswa kuwa eneo la amani, heshima na utulivu kwa ajili ya mwanamke ili aweze kutekeleza vyema wajibu wake mkubwa ambao ni kulinda familia.
Ayatullah Khamenei ameashiria mtazamo na harakati ya kutisha iliyokuwa imeenea kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kusema kuwa mwanamke wa Kiirani aliweza kushinda wimbi hilo kubwa la uharibifu kutokana na johari ya imani yake mkubwa na akawa moja na vituo muhimu vya ushindi na kudumu Mapinduzi ya Kiislamu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, mwenendo wa ustawi wa nafasi na hadhi ya mwanamke hapa nchini unatia matumaini. Ameashiria maendeleo makubwa na ya kusifiwa na wanawake katika nyanja mbalimbali za kisiasa, kijamii na kiutamaduni hususan katika medani ya elimu na sayansi na akasema, katika kilele cha fahari ya mwenendo huo kuna akinamama na wake wa mashahidi, wapiganaji na vilema wa vita vitakatifu ambao ni vigezo vya kuigwa katika subira, uvumilivu na kusimama kidete kama mlima na ambao wamekuwa wakitoa darsa na somo la kujitolewa na imani kwa watu wengine.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa mtazamo huo mzuri kuhusu mustakbali mwema wa mwanamke na familia haupasi kufumba macho yetu na kutuzuia kuona udhaifu na nakisi zilizopo bali tunapaswa kupeleka mbele tena kwa kasi zaidi mwenendo wa mafanikio ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika medani ya maswala ya wanawake kwa kutambua vyema mapungufu na matatizo hayo na kufanya juhudi za kuyaondoa. Amesisitiza pia juu ya kufanya juhudi za kushinda utamaduni mbovu wa nchi za Magharibi katika dunia ya leo.
Ayatullah Ali Khamenei amesema, kazi muhimu zinazohusiana na masuala ya wanawake zinapaswa kutatuliwa kwa uchunguzi na juhudi kubwa za kifikra za wanawake na kuwasilisha njia za utekelezaji wa fikra hizo ili kwa Baraka zake Mola wanawake na vijana wa kike waweze kupiga hatua kubwa zaidi na Iran ya Kiislamu ikaribie zaidi malengo yake aali.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa suala la mwanamke ni miongoni mwa maudhui muhimu za kuhakiki, kuchunguza na kutafakari na akaongeza kuwa kwa msingi huo moja ya vikao vya fikra za kistratijia katika Jamhuri ya Kiislamu kitajadili kadhia ya mwanamke.
Amewataka wanafikra wote wa kike kushiriki kwa bidii katika mjadala huo na akasema masuala yanayohusiana na mwanamke yanapaswa kujadiliwa katika kikao cha fikra za kistratijia kwa njia za kitaalamu na kisayansi na kwa kutegemea vyanzo vya Kiislamu na fikra safi za kimapinduzi na matokeo yake yawe msingi wa mipango na ratiba ya utekelezaji.
Mwanzoni mwa mkutano huo wasomi na wanafikra kumi wa kike wametoa hotuba wakibainisha mitazamo yao kuhusu masuala mbalimbali ya kiutamaduni, kijamii na kisiasa. 796406

captcha