IQNA

Ayatullah Khamenei:

Kushikamana na misingi ya Mapinduzi ya Kiislamu kumetia matumaini katika nyoyo za Waislamu

12:48 - May 25, 2011
Habari ID: 2128380
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei leo amehutubia hadhara ya washairi na wasomaji wa tungo zinazotaja matukufu na sifa za Ahlulbaiti wa Mtume Muhammad (saw) waliokusanyika mjini Tehran kuadhimisha siku ya kuzaliwa Bibi Fatima al Zahra (as) na Imam Ruhullah Khomeini.
Katika hafla hiyo Ayatullah Khamenei ametoa mkono wa baraka na fanaka kwa Waislamu kwa mnasaba wa kuadhimisha siku ya kuzaliwa Bibi wa Wanawake Wote Fatima al Zahra (as) na akasema mtukufu huyo ndiye mtu bora zaidi asiyekuwa na kifani baada ya Mtume wa Uislamu Muhammad (saw) na Amirul Muuminin Imam Ali bin Abi Twalib (as). Ameongeza kuwa kutajwa mara kwa mara jina la Bibi Fatima al Zahra na Imam wa Zama Mahdi (as) katika kipindi chote cha Mapinduzi ya Kiislamu ni baraka za Mwenyezi Mungu na jambo lililotoka katika nyoyo zenye imani.
Ayatullah Khamenei amekutaja kukutana kwa matukio mawili ya kuzaliwa binti mtukufu wa Mtume Muhammad (saw) Bibi Fatima (as) na Imam Ruhullah Khomeini kuwa ni jambo la kufurahisha. Ameongeza kuwa Imam Khomeini (MA) ni mfano halisi wa hakika ya Bibi Fatima na alijipamba kwa imani, ikhlasi, ibada, ghera ya dini yake na kusimama kidete katika njia ya Mwenyezi Mungu.
Ayatullah Khamenei ameashiria pia njia iliyojaa mashaka, upinzani na mikasa ya aina mbalimbali ya kipindi cha miaka 32 ya baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusema kuwa kudumishwa njia hiyo iliyonyooka na kulindwa kaulimbiu na malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu kwa baraka za miongozo ya Imam Khomeini ni miongoni mwa sifa kuu za Mapinduzi hayo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa kutokana na harakati hiyo inayotia matumaini na hatua madhubuti, hakuna nguvu yoyote duniani itakayoweza kufunga njia ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa kusimama imara, kudumisha na kushikamana barabara na thamani na nguzo za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ndiyo sababu ya kuchanua maua ya matumaini katika nyoyo za mataifa ya Waislamu na wachambuzi wa kimataifa.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa sifa makhsusi na kubwa ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni kuwa, kwa baraka zake Mola, msimu huo wa machipuo haujazima na kutoweka hadi hii leo.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa iwapo taifa la Iran lingelegeza kamba mbele ya vitisho vya ubeberu wa kimataifa na kutupilia mbali nara na kaulimbiu zake basi maua ya matumaini katika nyoyo za mataifa mbalimbali yangenyauka.
Amesema kwa baraka za jina la Bibi Zahra (as) na Imam Mahdi (as) na vilevile baraka na dua za Maimamu watoharifu na kusimama imara taifa la Iran, miche hiyo ya matumaini imezaa matunda; kwa msingi huo hali hiyo na kuelekea kwa Mwenyezi Mungu daima vinapaswa kudumishwa.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza juu ya udharura wa kuchagua shairi, mahadhi na sauti ya kupendeza katika sanaa ya kuvutia ya mashairi na kusoma tungo zinazohusiana na Ahlulbaiti wa Mtume Muhammad (saw). Amesema tungo zinazosomwa zinapaswa kuchaguliwa kwa njia sahihi na kutiliwa maanani muundo wake wa dhahiri na batini.
Amesema kuwa tungo mbaya na zisizofaa kisheria hazipaswi kuingizwa katika sanaa hiyo lakini akasisitiza kuwa si vibaya kuchagua na hata kubuni mbinu mpya za usomaji wa tungo hizo.
Ayatullah Khamenei pia amesisitiza juu ya umuhimu wa kuchagua muhtawa na madhumuni inayofaa katika kutaja sifa na matukufu ya Maimamu watoharifu katika kizazi cha Mtume (saw) na akasema, kutaja matukufu yaliyothibitishwa kwa huja za kutegemewa kunazifurahisha nyoyo na kuzitia hamasa.
Ameashiria pia haja ya jamii kwa nasaha za Maimamu watoharifu katika kizazi cha Bwana Mtume (saw) na kutumia maneno na semi za watukufu hao katika kustawisha maadili mema na akaongeza kuwa moyo wa ushirikiano, udugu na upendo unapaswa kuimarishwa katika jamii kwa kueneza tabia njema. Vilevile amesisitiza juu ya kujiepusha na mitazamo finyu, ukosefu wa matumaini, kuwatakia mabaya watu na ubahili kwa kueneza tabia ya kujitolea, ushirikiano, subira, ihsani na uvumilivu.
Ayatullah Khamenei amewahimiza wasomaji tungo na mashairi ya kumsifu Mtume na Ahlulbait kusoma Qur’ani na hadithi kwa wingi na akawataka kutumia aya za Qur’ani na hadithi zenye nasaha katika tungo zao. Vilevile amewausia kusoma dua, kutawasali, kutekeleza swala za suna akisisitiza kuwa kunasahilisha kazi ngumu maishani.
Mwanzoni mwa hafla hiyo malenga kadhaa walisoma mashairi na tungo zao wakitaja sifa na matukufu ya Bibi Fatima al Zahra (as). 797890

captcha