IQNA

Ayatullah Khamenei:

Kushindwa siasa za Marekani ni ishara ya kutimia ahadi ya Mwenyezi Mungu

20:12 - May 31, 2011
Habari ID: 2131774
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran amesema kuwa kushindwa siasa za Marekani Mashariki ya Kati ni kielelezo cha kutimia baadhi ya ahadi za Mwenyezi Mungu kwa Taifa la Iran.
Ayatullah Ali Khamenei ameyasema hayo leo wakati wa kukagua gwaride la wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Maafisa wa Jeshi cha Imam Hussein mjini Tehran na kuongeza kuwa kushindwa kwa siasa za Shetani Mkubwa yaani Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati na kuhuishwa nara zinazotoa bishara njema za Kiislamu baina ya mataifa mbalimbali ni kielelezo cha kutimia sehemu moja ya ahadi za Mwenyezi Mungu kwa taifa la Iran. Amesisitiza kuwa kusimama kidete na imara katika njia hiyo kutafuatiwa na kutimia kikamilifu nusra ya Mwenyezi Mungu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran Shetani Mkubwa, Marekani alitumia nguvu zake kubwa za kijeshi, kifedha, kipropaganda na kisiasa kwa ajili ya kuvunja mapinduzi hayo na taifa la Iran, lakini ukweli wa mambo na hali ya kisiasa ya Iran na eneo zima la Mashariki ya Kati inaonesha kwamba Marekani imepiga magoti mbele ya Mapinduzi ya Kiislamu.
Ayatullah Khamenei amesema, hii leo baada ya kushindwa njama za mara kwa mara za mfumo wa kibeberu, Uislamu na Qur'ani imekuwa neno linalozungumzwa sana kati ya vijana na mataifa ya eneo hili na jambo hilo linaonesha picha ya kupepea bendera inayong'aa ambayo taifa la Iran liliipandisha juu mwaka 1979 katika nchi ya Iran.
Ayatullahil Udhmaa Ali Khamenei amekutaja kushindwa kwa Marekani katika kadhia ya Palestina kuwa ni ishara nyingine ya hali mbaya ya Shetani Mkubwa. Ameongeza kuwa vijana wa Kipalestina katika nchi mbalimbali za eneo hili walivunja mipaka ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Israel katika 'Siku ya Maafa' baada ya kupita miaka 60, na tukio hilo la kufurahisha ni mwanzo wa kutimia ahadi ya Mola Muweza ya kupata ushindi kamili dini ya Uislamu na Waislamu. 801875



captcha