IQNA

Ayatullah Khamenei:

Iran inatengeneza silaha kwa ajili ya kujilinda mbele ya hujuma za maadui

13:54 - June 23, 2011
Habari ID: 2143128
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi yote hapa nchini ametembelea na kukagua maonyesho ya matunda ya jihadi ya elimu na uwezo wa kujihami wa jeshi la Iran.
Baada ya kuwasili katika maonyesho hayo, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu alifika katika eneo lililotengwa kwa ajili ya kuwakumbuka mashahidi wa vita vya kujitetea kutakatifu akawasomea al Fatiha na kuwaombea daraja za juu peponi.
Maonyesho hayo yana zaidi ya matunda 300 ya sayansi, teknolojia na zana za kujilinda za jeshi la Iran, kikosi cha Gadi ya Mapinduzi ya Kiislamu, kikosi cha polisi na Wizara ya Ulinzi. Baadhi ya mafanikio hayo ya kijeshi yanayoonyeshwa ni pamoja na mizinga, ndege za kivita, helikopta, ndege zisizokuwa na rubani, meli na nyambizi za kivita, aina mbalimbali za rada za kisasa, zana za mawasiliano ya kijeshi, zana za kukabiliana na vita vya elektroniki, zana za vita vya mtandao wa intaneti, bidhaa mbalimbali za kitiba za kujilinda na kadhalika.
Amir Jeshi Mkuu wa Iran alikagua pia maonyesho ya utengenezaji magari mepesi yanayotumiwa vitani, magari ya deraya, kizazi kipya cha kifaru cha Dhul Fiqar, utengenezaji wa makombora ya ardhi –anga, ardhi-ardhi, na anga-ardhi yanayotumia fueli mango na fueli ya kawaida na kadhalika.
Jeshi la polisi pia limeonyesha mafanikio yake katika teknolojia ya mawasiliano, uchapishaji wa nyaraka na hati za elektroniki kama pasi na hati za kuendeshea magari, udhibiti wa mipaka, barabara na kadhalika.
Vilevile vijana wa jeshi la kujitolea la Basij wameonyesha uwezo wao wa kielimu katika masuala ya leza, antena za nano na kadhalika.
Sehemu nyingine ya maonyesho hayo ilihusu matunda ya uhakiki wa jeshi kuhusu uwezo wa makombora wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Sehemu hiyo ilijumuisha aina mbalimbali za makombora ya masafa marefu kama Sijjil lenye uwezo wa kupiga umbali wa kilomita 2000, kombora la Qiyam linalopiga umbali wa masafa ya kilomita 750 na aina tofauti za makombora ya Fatih yenye uwezo wa kupiga masafa mbalimbali.
Vilevile kulikuwepo makombora ya balestiki yanayotumia fueli mango na ya kawaida, makombora ya majini na makombora yanayotumiwa kupiga meli za kivita.
Sehemu nyingine ilihusu maonyesho ya makombora yanayotumiwa kutuma satalaiti angani kama Safir, Omid, Rasad na miradi ya baadaye ya majaribio ya makombora ya aina hiyo na mifumo ya zana za anga.
Jumla ya mafanikio hayo ya kielimu yamepatikana kutokana na juhudi za vituo vya uhakiki vya jeshi kwa kushirikiana na wasomi wa vyuo vikuu na mashirika ya kisayansi hapa nchini.
Baada ya kukagua maonyesho hayo Ayatullah Khamenei amewashukuru wasimamizi wake na akasema uhakiki ndio nguzo kuu ya uzalishaji wa bidhaa mpya. Amesisitiza kuwa vituo vya uhakiki na uchunguzi vya jeshi vinapaswa kudumisha harakati yao ya kusonga mbele kwa kasi na nguvu kubwa zaidi.
Amesema ni jambo lenye faida kubwa kuwepo vituo vya uhakiki katika taasisi mbalimbali za jeshi na kuongeza kuwa vituo hivyo vinapaswa kukamilishana na kujiepusha kufanya kazi zinazoharibu bure rasilimali za kimaada na kibinadamu.
Amiri Jeshi Mkuu amevihimiza vituo hivyo pia kufanya jitihada za kuongeza kiwango cha elimu na teknolojia.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ametilia mkazo suala la kuimarishwa vituo vya uhakiki vya jeshi na kulindwa wataalamu na wahakiki.
Ayatullah Khamenei amesema, lengo kuu la kutengeneza silaha na zana za kivita katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kujilinda na kukabiliana na maadui na madhalimu, wakati ambapo lengo kuu la uzalishaji silaha katika nchi za Magharibi ni biashara na kuzidisha utajiri wa mabepari wanaomiliki viwanda na makampuni ya silaha.
Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa vikwazo vilivyowekwa na nchi za Magharibi dhidi ya Iran vitakuwa na madhara kwa maadui wa taifa hili kutokana na juhudi kubwa za jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ayatullah Khamenei pia aliongoza swala za Adhuhuri la Alasiri katika eneo la maonyesho hayo ya kielimu na uwezo wa kujilinda wa Iran. 813677


captcha