IQNA

Ayatullah Khamenei:

Harakati za wananchi ni mwanzo wa mabadiliko makubwa

17:19 - June 26, 2011
Habari ID: 2144731
Ayatullah Khamenei amesema harakati za hivi karibuni za wananchi katika Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika ni mwanzo wa mabadiliko ya kimsingi katika nchi za Kiislamu na eneo hili zima.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei kabla ya adhuhuri ya leo amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Umar al Bashir wa Sudan na ujumbe anaoandamana nao hapa nchini. Ayatullah Khamenei amesema harakati za hivi karibuni za wananchi katika Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika ni mwanzo wa mabadiliko ya kimsingi katika nchi za Kiislamu na eneo hili zima. Ameongeza kuwa kuna matarajio ya kushuhudiwa muungano madhubuti zaidi wa Kiislamu huko kaskazini mwa Afrika.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameelezea kufurahishwa kwake na mwamko wa Kiislamu katika nchi za Misri, Tunisia na Libya na kusema kuwa harakati hizo ni kinyume na matakwa na maslahi ya Marekani, nchi za Magharibi na Wazayuni; kwa msingi huo tunapaswa kuwa macho ili Marekani na nchi za Magharibi zisikwamishe harakati hiyo ya wananchi na hatimaye kuiteka nyara.
Ayatullah Khamenei amesema Marekani na Magharibi haziwezi kufanya lolote katika kipindi cha muda mfupi lakini tunapaswa kuwa makini kuhusu upotofu au njama yoyote ya kuteka harakati za wananchi katika eneo la Kaskazini mwa Afrika na Mashariki ya Kati.
Ameitaja maudhui ya Misri kuwa ni muhimu mno na kuongeza kuwa ngome imara ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel nchini Misri imesambaratika na Marekani na baadhi ya serikali vibaraka zinafanya jitihada za kubadili mwelekeo katika kipindi cha muda mrefu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria historia ya kubadilishwa watu na harakati za kimapinduzi kadiri muda unavyopita na akasisitiza kuwa jambo hilo halipaswi kuruhusiwa kutokea kuhusu masuala ya maeneo hayo yaliyotajwa.
Kuhusu masuala ya Libya, Ayatullah Khamenei amesema: "Tuna wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya Libya kwani harakati ya wananchi wa Libya ni harakati halisi na ya kweli lakini Wamagharibi hawataki kuona harakati hiyo ikikamilika."
Ameutaja uingiliaji wa majeshi ya nchi za Magharibi huo Libya kuwa unafanyika kwa lengo hilo na akaongeza kuwa Wamagharibi wana woga mkubwa juu ya kuasisiwa serikali yenye mwelekeo wa Kiislamu nchini Libya na jirani ya Ulaya na wameazimia kuzuia jambo hilo.
Katika sehemu nyingine ya matamshi yake Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria masuala ya Sudan na mashinikizo ya nchi za Magharibi dhidi ya nchi hiyo na akasema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono serikali ya Kiislamu, utawala na taifa la Sudan lililoazimia kulinda uhuru, Uislamu na ardhi yake yote.
Ayatullah Khamenei amesema kusimama kidete na mapambano ya serikali na taifa la Sudan mbele ya njama na mashinikizo ya Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel na Magharibi yanapaswa kupongezwa.
Amesema katika kipindi cha sasa makundi na vyama vyote vya Sudan vinapaswa kuwa macho na kuungana.
Kwa upande wake Rais Omar Hassan al Bashir wa Sudan amesema katika kikao hicho ambacho pia kimehudhuriwa na Rais Ahmadinejad kwamba uhusiano wa Khartoum na Tehran ni mzuri na imara na ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa misaada na uungaji mkono wake kwa watu wa Sudan. al Bashir amesema, serikali na taifa la Sudan limesimama imara mbele ya mashinikizo hayo na lina matumaini ya mustakbali mwema licha ya mashinikizo ya nchi za Magharibi.
Rais wa Sudan ameongeza kuwa mageuzi yanayotokea katika eneo la kaskazini mwa Afrika na Mashariki ya Kati yanatia moyo na yatakuwa na maslahi kwa nchi za Kiislamu. Amesema hali ya mambo katika maeneo hayo haitarejea katika kipindi cha kabla ya harakati za wananchi na Marekani na utawala ghasibu wa Israel ndizo zitakazopata hasara zaidi kutokana na mabadiliko hayo. 815530



captcha