Ayatullah Khamenei ameashiria haja ya Idara ya Vyombo vya Mahakama hapa nchini kwa nguzo mbili muhimu yaani uwezo na imani ya wananchi na akasema: “Hatua yoyote au kitendo cha kutilia shaka shughuli, ripoti na takwimu zinazotolewa na viongozi wa ngazi za juu wa vyombo vikuu vitatu vya dola hususan Idara ya Vyombo vya Mahakama ni makosa na hatua isiyokuwa sahihi, inayoondoa imani ya wananchi kwa vyombo vya dola na ni kinyume cha maslahi ya taifa. Amesisitia kuwa viongozi wote, wamiliki wa vyombo vya mawasiliano ya umma na vyombo vya habari wanapaswa kulizingatia kikamilifu suala hilo muhimu.
Hadhara hiyo ilikusanyika kwa mnasaba wa kukumbuka tukio la kigaidi la kulipuliwa ofisi za chama cha Jamhuriye Islami tarehe 7 Tir mwaka 1360 Hijria Shamsia (28 Juni 1981) na kuuawa shahidi Mkuu wa zamani wa Idara ya Vyombo vya Mahakama vya Iran Ayatullah Dakta Muhammad Beheshti na wanamapinduzi wengine 72 na imehudhuriwa pia na familia za mashahidi wa tukio hilo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewakumbuka mashahidi wa shambulizi hilo la kigaidi hususan Ayatullah Muhammad Beheshti na akasema tukio hilo lilikuwa janga kubwa lakini taifa la Iran, kutokana na subira na uwezo wa kumaizi baina ya haki na batili na kuona mbali lilioupata kutoka kwa hayati Imam Khomeini, lilibadili janga hilo na kuwa neema na kurejesha wimbi hilo upande wa adui.
Ayatullah Khamenei amesema darsa hiyo ambayo taifa la Iran lilifuzu mtihani wake ndiyo sababu kuu ya maendeleo na harakati ya kusonga mbele nchi hii. Ameongeza kuwa kutokana na malengo yake aali ambayo ni kufikia kwenye thamani za Kiislamu na kutekeleza misingi ya Kiislamu katika jamii na kuieneza kote duniani, taifa la Iran daima limekuwa likikabiliana na madhalimu, wakoloni, madikteta na mashaka wanayoyasababisha; kwa msingi huo tunapaswa kukabiliana na mashaka kwa subira na kuwa na uwezo wa kumaizi na kutumia machungu mbalimbali kama ngazi ya kufikia maendeleo na ustawi.
Sehemu nyingine ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika hadhara hiyo iligusia maswala ya Idara ya Vyombo vya Mahakama.
Ayatullah Khamenei amesema uwezo na imani ya umma ni nguzo mbili kuu zinazohitajiwa na Idara ya Vyombo vya Mahakama hapa nchini na kuongeza kuwa nguvu na uwezo wa idara hiyo unapatikana kwa kutayarishwa miundombinu mizuri ya kibinadamu na kiufundi.
Amesema kutayarisha watu wanaostahiki, bora, waaminifu na watenda mema kwa ajili ya kazi za mahakama, ubunifu, kuweka sheria sahihi na kutumia vyema na kwa mujibu wa mwongozo wa akili na busara maendeleo mbalimbali ya kiufundi kutatayarisha uwanja mzuri wa kuimarika zaidi Idara ya Vyombo vya Mahakama.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, sharti la kupata imani ya taifa ambayo ni nguzo muhimu ya pili inayohitajiwa na Idara ya Vyombo vya Mahakama, ni kudhaminiwa uadilifu. Amesisitiza kuwa kutekelezwa uadilifu daima katika Vyombo vya Mahakama kunahitaji kuwa na ucha-Mungu, kuyatazama mambo yote makubwa na madogo bila ya upendeleo na kutekeleza sheria kwa uangalifu mkubwa na kwa mujibu wa hekima na busara.
Ayatullah Khamenei ameashiria suala la kuharibiwa imani ya umma kwa taasisi za dola na akakosoa tabia ya baadhi ya watu ya kutilia shaka bila ya sababu shughuli, ripoti na takwimu zinazotolewa na vyombo vikuu vitatu vya dola yaani Mahakama, Serikali na Bunge. Amesema kwamba kutilia shaka kazi kubwa na ripoti rasmi zinazotolewa na viongozi wa ngazi za juu wa mfumo wa Kiislamu katika vyombo vikuu vitatu vya dola na kuharibu imani ya wananchi kwa vyombo hivyo ni makosa na kitendo kisichokuwa sahihi, hivyo viongozi wote, wamiliki wa vyombo vya mawasiliano ya umma na vyombo vya habari wanapaswa kulitilia maanani suala hilo muhimu.
Ameashiria pia uwezekano wa kuwepo makosa katika baadhi ya ripoti au takwimu hizo na akasema haipasi kuharibu imani ya wananchi kwa kupanua makosa kama hayo na kueneza shaka miongoni mwa wananchi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia suala la kuzungumziwa katika vyombo vya habari tuhuma zinazowakabili watu mbalimbali na kusema kuwa kutuhumiwa mtu hakuna maana kwamba ni mhalifu, kwa msingi huo hakuna mtu mwenye haki ya kutangaza tuhuma zinazowakabili watu mbalimbali katika Idara ya Mahakama au vyombo vya habari hadi pale tuhuma hizo zitakapothibitishwa.
Ayatullah Khamenei amekosoa baadhi na mashinikizo yanayotolewa dhidi ya Idara ya Vyombo vya Mahakama kwa ajili ya kuitaka idara hiyo ifichue majina na baadhi ya watuhumiwa wa kesi mbalimbali na kusema kuwa hakuna ulazima wowote wa kuchukuliwa hatua kama hiyo na hakuna mtu anayeruhusiwa kumvunjia heshima Muislamu.
Amesema kuwa katika sheria za Kiislamu kuna kesi makhsusi ambapo inatolewa ruhusa ya kuchapichwa au kutangazwa majina na mtu aliyehukumiwa na akaongeza kuwa hata katika kesi ambazo makosa ya mtu yanathibitishwa mahakamani, basi jina la mhalifu halipaswi kutangazwa na kuchapishwa katika vyombo vya habari, kwani familia yake inakuwa chini ya mashinikizo na kukumbwa na matatizo.
Mwishoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria maendeleo yaliyopatikana katika Idara ya Vyombo vya Mahakama hapa nchini tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hadi sasa na akasema katika kipindi cha sasa pia kuna shakhsia wakubwa katika upande wa elimu, ubunifu na hima katika uongozi wa idara hiyo na kumefanyika kazi nzuri za kusifiwa.
Mwanzoni mwa kikao hicho Mkuu wa Idara ya Vyombo vya Mahakama hapa nchini Ayatullah Sadiq Amoli amewakumbuka mashahidi wa tarehe 28 Juni 1981 hususan Ayatullah Dakta Beheshti na akatoa ripoti kuhusu kazi zilizofanyika katika idara hiyo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Ayatullah Larijani amezungumzia pia utendaji wa Idara ya Vyombo vya Mahakama katika kukabiliana na watu waliohusika na fitina za baada ya uchaguzi wa rais miaka miwili iliyopita na akasisitiza juu ya udharura wa kukabiliana na mirengo mingine iliyopotoka. Amesema kuwa Idara ya Mahakama itadumisha mapambano yake makubwa na ya kiadilifu dhidi ya wahalifu wa jinai makhsusi, ulanguzi wa dawa za kulevya, wezi wanaotumia silaha, wabakaji na mafisadi.
816190