IQNA

Ayatullah Khamenei:

Matatizo ya jana na leo ya umma wa Kiislamu yanatokana na kutoshukuru neema kubwa ya kupewa utume Nabii Muhammad (saw)

4:11 - July 01, 2011
Habari ID: 2146950
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa matatizo na mashaka ya jana na leo ya umma wa Kiislamu yanatokana na kutoshukuru neema kubwa ya kupewa utume Nabii Muhammad (saw).
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei mapema leo amehutubia hadhara kubwa iliyojumuisha viongozi wa mfumo wa Kiislamu wa Iran na matabaka mbalimbali ya wananchi akitoa mkono wa heri na baraka kwa taifa la Iran na umma mzima wa Kiislamu kwa mnasaba wa kukumbuka tukio la kubaathiwa na kupewa utume Nabii Muhammad (saw). Ayatullah Khamenei amelitaja tukio la kupewa utume Nabii Muhammad kuwa ni neema kubwa zaidi ya Mwenyezi Mungu na siku yenye baraka kubwa zaidi kati ya siku za mwaka mzima. Amesisitiza kuwa mwamko wa Kiislamu wa mataifa ya kaskazini mwa Afrika na Mashariki ya Kati ni harakati inayofuata nyayo za Nabii Muhammad (saw). Amesema kuwa mataifa ya Kiislamu na taifa la Iran hayatairuhusu Marekani na Wazayuni kupotosha harakati hiyo adhimu au kudandia mawimbi yake kupitia njia ya kuzusha hitilafu na hila nyinginezo.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameshiria athari muhimu na kubwa za kipindi cha miaka 23 ya kufikisha ujumbe Mtume wa mwisho wa Mwenyezi Mungu katika historia na hatima ya mwanadamu na akasema: “Katika kipindi hicho kifupi ambacho miaka kumi yake ilitumiwa katika kuasisi mfumo wa utawala wa Kiislamu, Nabii Muhammad (saw) alijenga jamii adhimu kwa msingi wa imani, mantiki, jihadi na heshima na hata ustaarabu wa mwanadamu wa sasa umefaidika na ustaarabu wa Kiislamu uliojengeka juu ya misingi hiyo.
Amesema kuwa matatizo na mashaka ya jana na leo ya umma wa Kiislamu yanatokana na kutoshukuru neema kubwa ya kupewa utume Nabii Muhammad (saw). Ameongeza kuwa iwapo mataifa ya Waislamu yataimarisha imani yao katika moyo na matendo, yakatumia vyema mantiki na akili ya kibinadamu kama hadiya kubwa ya Mwenyezi Mungu, yakatekeleza jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kwenye medani za kijeshi, kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni na yakatumia vizuri heshima na izza yao ya kibinadamu, hapana shaka kwamba yatafikia nafasi ya juu yanayostahiki.
Ayatullah Khamenei ameyataja matukio ya sasa katika baadhi ya nchi za kaskazini mwa Afrika na Mashariki ya Kati kuwa ni ishara kwamba mataifa ya Waislamu yametilia maanani neema inayompa ufanisi mwanadamu ya Uislamu. Amesema mwamko mkubwa wa Kiislamu nchini Misri na katika nchi nyingine unaonesha kwamba mlingano wa kidhalimu na wa kudunisha uliolazimishwa na mabeberu wa Magharibi na watawala tegemezi kwa mataifa ya eneo hilo katika kipindi cha miaka 150 iliyopita umevurugika na sasa kumefunguliwa ukurasa mpya katika historia ya maeneo hayo.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, kwa baraka zake Mola, mustakbali wa maeneo hayo uko wazi na unatoa bishara njema. Ameashiria mwenendo wa madola ya kibeberu ya kukana na kuficha sura ya Kiislamu ya mageuzi ya sasa na akasema Wamarekani, Wazayuni, vibaraka wao na wenzao katika kanda hii wanatumia nguvu zao zote kwa shabaha ya kupotosha harakati adhimu ya mataifa na kurejesha tena mlingano wa kidhalimu wa miaka iliyopita kwa kuwapachika madarakani watu tegemezi; hata hivyo pindi taifa linapoamka na kupiga moyo konde kwa kuingia kwenye medani ya mapambano, haiwezekani kulishinda.
Ametilia mkazo pia udharura wa mataifa na wasomi wa ulimwengu wa Kiislamu kuamka, kuwa macho na kuona mbali mkabala wa njama na mipango tata ya Marekani na utawala wa ghasibu wa Israel na akasema, harakati za mabeberu hao zitayasababishia baadhi ya matatizo mataifa yaliyoamka, lakini njia yenye mwanga iliyoanza katika kanda hii itaendelea kwa nguvu kubwa inshaallah kutokana na baraka za kuwa macho wananchi na wasomi wa umma wa Kiislamu.
Katika uwanja huo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbusha njama mbalimbali zilizofanywa na maadui wa Uislamu dhidi ya ushindi wa mapinduzi nchini Iran na akasema kuwa miongoni mwa harakati zilizofeli za mabeberu kwa ajili ya kudhoofisha harakati kubwa ya taifa la Iran ni pamoja na kuzusha hitilafu, kupenya ndani ya nchi, kutekeleza mauaji ya kigaidi, kuzusha mapigano ya kikaumu na kidini, kuzusha fitina na kumchochea adui wa kigeni ili aishambulie kijeshi Iran. Amesisitiza kuwa njama hizo hizo na nyinginezo zitabuniwa na kutekelezwa dhidi ya mataifa yaliyoamka.
Amefafanua njia za kimsingi za kukabiliana na njama hizo akisisitiza juu ya udharura wa mataifa na wasomi wa ulimwengu wa Kiislamu kujiepusha na mijadala isiyokuwa na faida na yenye umuhimu mdogo, kutozingatia hitilafu za kimadhehebu, kikaumu na kimirengo na kutambua vyema adhama ya kihistoria ya mapambano ya mataifa ya Waislamu.
Akiashiria uungaji mkono wa siku zote wa utawala wa Kiislamu hapa nchini kwa harakati zote za kupigania uadilifu na dhidi ya ubeberu, Ayatullah Khamenei amesema: “Kila sehemu kunakofanyika harakati dhidi ya Marekani na Uzayuni na kila taifa linalopambana na udikteta wa kimataifa wa Marekani na madikteta wa ndani basi litapata uungaji mkono wa taifa lililopevuka la Iran.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, moja ya njama tata za Marekani ni ‘kufananisha vitu visivyoshabihiana’. Ameashiria matukio ya Syria na akasema kuwa Wamarekani wanafanya njama za kujaribu kuitumbukiza nchi hiyo iliyoko mstari wa mbele wa mapambano kwa kutaka kufananisha hali ya Syria na matukio ya Misri, Tunisia, Yemen na Libya. Amesisitiza kuwa matukio ya Syria yanatofautiana na matukio ya nchi nyingine za kanda hii.
Amesema hakika ya mwamko wa Kiislamu katika nchi za kanda hii ni kwamba ni harakati ya kupinga Uzayuni na Marekani, lakini mkono wa Israel na Marekani unaonekana waziwazi kabisa katika matukio ya Syria. “Mantiki na kigezo cha taifa la Iran ni kuwa mahala popote panapotolewa nara kwa maslahi ya Marekani basi hiyo itakuwa ni harakati iliyopotoka” amesisitiza Ayatullah Khamenei.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa kushikamana barabara kwa taifa la Iran na utawala wa Kiislamu hapa nchini na mantiki na kigezo hicho kunawakasirisha maadui na kuzidisha njama zao; hata hivyo taifa lililopata tajiriba na la wanamapambano la Iran halitalegeza kamba katika misimamo yake.
Ameashiria hali ya kudhulumiwa kwa taifa la Bahrain na akasema kuwa harakati ya wananchi wa Bahrain inashabihiana kidhati na harakati ya Misri, Tunisia na Yemen na ni jambo lisilokuwa na maana yoyote kutofautisha baina ya harakati zinazoshabihiana. Amesema kuwa inasikitisha kuona kwamba baadhi ya watu wanafuata njia ya maadui wa Uislamu badala ya kutilia maanani matakwa ya mataifa.
Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Ali Khamenei ametilia mkazo umuhimu wa kuchapa kazi na kufanya bidii zaidi katika taasisi mbalimbali kote nchini. Amesema kuwa suala la kuunganisha wizara na kupunguza ukubwa wa serikali lina umuhimu mkubwa sana. Ameashiria ushirikiano wa Serikali na Bunge katika suala hilo na akasema kuwa kazi kama hizo zinapaswa kudumishwa kwa bidii kubwa zaidi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria tamaa ya maadui kwa baadhi ya masuala na matukio ya ndani hapa nchini na akasema, taifa la Iran na viongozi wa mfumo wa Kiislamu watawafanya maadui wakate tamaa na kupoteza matumaini kutokana na wananchi kusimama kidete na kuwa kwao daima na matumaini ya kupata msaada wa Mwenyezi Mungu, na viongozi kushirikiana na kudumisha umoja.
Mwanzoni mwa mkutano huo uliohudhuriwa pia na mabalozi wa nchi za Kiislamu mjini Tehran, Rais Mahmoud Ahmadinejad amemtaja Mtume wa Mwisho Muhammad (saw) kuwa ni zawadi kubwa zaidi ya Mwenyezi Mungu kwa mwanadamu. Amesema kuwa kupewa utume Nabii Muhammad (saw) ni tukio kubwa zaidi la historia ambalo linaweza kumfikisha mwanadamu katika njia yenye nuru ya tauhidi na uhai wenye saada na ufanisi halisi.
Rais Ahmadinejad ameutaja ujinga na mghafala wa mwanadamu na dhulma na uonevu wa watawala waovu kuwa ndio vikwazo vikuu zaidi vinavyoizuia jamii ya mwanadamu kufaidika kikamilifu na ujumbe unaotoa uhai wa Mtume Mtukufu. Ameongeza kuwa shetani mkubwa, Marekani na mshirika wake utawala wa Kizayuni wa Israel zinazuia harakati ya jamii ya mwanadamu kuelekea katika njia iliyonyooka ya Mwenyezi Mungu. Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa mwanadamu wa leo anahitajia ujumbe wa Nabii Muhammad (saw) kuliko wakati wowote mwingine na akaongeza kuwa kudhihiri kwa Imam wa Zama Mahdi (as) kutakamilisha tukio la kihistoria la kupewa utume Nabii Muhammad (saw) na kutoa bishara njema ya saada na ufanisi halisi wa mwanadamu. 817886
captcha