IQNA

Ayatullah Khamenei:

Kupuuza uwezo wa Qur'ani Tukufu wa kuwaunganisha Waislamu ni mghafala mkubwa wa mataifa ya Kiislamu

16:52 - July 05, 2011
Habari ID: 2149567
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa kupuuza uwezo wa Qur'ani Tukufu wa kuwaunganisha pamoja Waislamu ni mghafala mkubwa wa mataifa ya Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo mapema leo alipokutana na kuhutubia walimu, majaji, makarii na mahafidhi wa Qur'ani walioshiriki katika Mashindano ya 28 ya Kimataifa ya Qur'ani mjini Tehran na wapenzi wa kitabu hicho kitukufu. Ayatullah Khamenei amesema katika hotuba hiyo kwamba Qur'ani ndiyo wenzo na sababu muhimu zaidi ya kuimarisha umoja, heshima na uwezo wa umma wa Kiislamu. Amesema kuwa harakati ya mataifa ya kaskazini mwa Afrika na Mashariki ya Kati ni ishara ya kutimia ahadi za Mwenyezi Mungu Mtukufu katika kitabu cha Qur'ani.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa mashindano ya kimataifa ya Qur'ani ni ishara ya uwezo mkubwa wa kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu katika kuwakutanisha na kujenga umoja baina ya Waislamu. Ameongeza kuwa mataifa yote ya Waislamu yananyenyekea mbele ya hadiya hiyo isiyokuwa na kifani ya Mwenyezi Mungu na kupata elimu na maarifa yake, na jambo hilo ni fursa muhimu sana kwa ajili ya kuwaunganisha Waislamu.
Amesema kuwa kupuuza uwezo wa Qur'ani Tukufu wa kuwaunganisha pamoja Waislamu ni mghafala mkubwa wa mataifa ya Kiislamu na kuongeza kuwa mghafala mwingine katika uwanja huo ni kutokuwa na imani na maana ya aya za Qur'ani na ahadi za Mola Mlezi, jambo ambalo linazuia umoja, heshima na nguvu ya umma wa Kiislamu.
Akifafanua suala la kutimia ahadi za Mwenyezi Mungu lililozungumziwa ndani ya Qur'ani, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria mabadiliko makubwa yaliyotokea ndani ya taifa la Iran na akasema: "Sisi, taifa la Iran tumetekeleza kivitendo aya tukufu ya Qur'ani inayosema: "Mwenyezi Mungu habadili hali ya watu hadi pale watu wenyewe watakapobadilisha yaliyomo katika nafsi zao" na tumeona kikamilifu nusra na msaada wa Mwenyezi Mungu baada ya kusimama na kupambana katika njia yake."
Ayatullah Khamenei ameitaja Iran ya kipindi cha utawala wa kishetani wa Shah kuwa ilikuwa "Iran ya Marekani" na Iran tegemezi kwa Wazayuni. Amesema kuwa kubadilika Iran na kuwa kituo madhuburti cha kupambana na ubeberu na Uzayuni ni muujiza na kutimia kwa ahadi ya nusra ya Mwenyezi Mungu iliyobashiriwa na Allah katika Qur'ani Tukufu.
Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa harakati za mageuzi za mataifa ya Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika ni ishara nyingine ya kutimia ahadi za Mwenyezi Mungu katika Qur'ani. Ameongeza kuwa Marekani, kambi habithi ya Wazayuni na waitifaki wao wa kisiasa katika kanda hii hawakuwa tayari hata kufikiria uwezekano wa wananchi wa Misri kusimama kidete na kuanzisha harakati ya mageuzi, lakini taifa hilo lilisimama kwa nara ya "Allah Akbar" na sala za Ijumaa na jamaa na kuingia katika medeni kwa ajili ya kuinusuru dini ya Allah na likapata nusra na msaada wa Mwenyezi Mungu. Amesisitiza kuwa suala hilo limethibitisha kwamba pale Mwenyezi Mungu anapomnusuru mja, hakuna nguvu yoyote inayoweza kumshinda.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake Ayatullah Ali Khamenei amesema kuhifadhi Qur'ani kichwani humpa mja fursa kubwa zaidi ya kutafakati kwa kina ndani ya kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu. Amewausia vijana kuhifadhi Qur'ani na akasema: "Kutadabari na kutafakati kwa kina ndani ya Qur'ani ndio ufunguo mkuu wa kuelewa maana ya kina ya kitabu hicho na kuhifadhi aya za Qur'ani huzidisha fursa hiyo."
Mwanzoni mwa mkutano huo mwakilishi wa Kiongozi Muadhamu ambaye pia ni mkuu wa Jumuiya ya Wakfu na Masuala ya Kheri ya Jamhuri ya Kiislamu Hujjatul Islam Walmuslimin Muhammadi ametoa ripoti kuhusu Mashindano ya 28 ya Kimataifa ya Qur'ani ya Tehran na akasema kuwa makarii na mahafidhi 96 wa Qur'ani kutoka nchi 61 na majaji 13 wameshiriki katika mashindano hayo yaliyofanyika katika kipindi cha siku tano.
Sheikh Muhammadi amesema kuwa shughuli nyingine zilizofanyika wakati wa mashindano hayo ya Qur'ani ni pamoja na utafiti wa masuala ya Qur'ani kupitia njia ya uandishi wa makala, kongamano la wanaharakati wa kike wa masuala ya Qur'ani, warsha za mafunzo ya kitaalamu ya kiraa na hifdhi, maonyesho ya bidhaa mbalimbali zinazohusiana na Qur'ani na vikao vya kiraa. 820615
captcha