IQNA

Ayatullah Khamenei:

Kushikamana na Uislamu ndiyo njia pekee ya uokovu

14:37 - July 17, 2011
Habari ID: 2155336
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa nchi mbili za Iran na Pakistan zina masuala mengi yanayozikutanisha pamoja katika nyanja za kidini, kihistoria na kiutamaduni na kulitaja taifa la Pakistan kuwa ni taifa kubwa na lenye historia ya muda mrefu ya mapambano.
Ayatullah Ali Khamenei ameyasema hayo leo katika mazungumzo yake na Rais Asif Ali Zardari wa Pakistan aliyewasili hapa nchini hii leo. Amesema wananchi wa Pakistan ni watu wanaoamini Uislamu na kwamba maendeleo na mafanikio yoyote ya Pakistan yanaifurahisha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa shakhsia wakubwa wa Pakistan kama Muhammad Ali Janah na Iqbal Lahori waling'ara katika mapambano ya muda mrefu ya wananchi wa nchi hiyo na sifa kuu ya mapambano hayo ilikuwa ni kushikamana wananchi na Uislamu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa njia pekee ya kuokoka wananchi wa Pakistan kutoka kwenye matatizo na mashaka yao ya sasa ni kuendelea kushikamana barabara na Uislamu na maarifa ya dini hiyo.
Ayatullah Khamenei ameashiria vitisho vya baadhi ya maadui dhidi ya umoja wa kitaifa na ardhi ya Pakistan na akasema adui halisi wa wananchi wa Pakistan na umoja wa kitaifa wa nchi hiyo ni Wamagharibi wakiongozwa na Marekani. Amesema anataraji kwamba Mwenyezi Mungu (SW) ataliepusha taifa la Pakistan na shari hiyo haraka iwezekanavyo.
Kwa upande wake Rais Asif Ali Zardari wa Pakistan amesema katika mazungumzo hayo ambayo pia yamehudhuriwa na mwenyeji wake Rais Ahmadinejad, kwamba kuwa na imani na Mwenyezi Mungu na kushikamana na Uislamu kunatayarisha uwanja mzuri wa maendeleo na ustawi wa mwanadamu na kumuondoa katika mashaka na matatizo mbalimbali. Vilevile amezungumzia mapambano ya taifa la Iran na kusimama kidete kwake mbele ya mashinikizo na akasema nchi na taifa la Iran limekuwa kigezo bora cha kusimama kidete na kupiga hatua katika njia ya ustawi na maendeleo. Amesisitiza pia juu ya dharura wa kudumishwa mazungumzo kati ya Islamabad na Tehran na kuendelezwa uhusiano na ushirikiano wa kieneo.
captcha