IQNA

Kujiepusha na hitilafu ni wajibu wa kidini na kitaifa

18:20 - July 25, 2011
Habari ID: 2159802
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei jana usiku alihutubia hadhara ya maelfu ya wafanyakazi wa Jeshi la Majini la Iran, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah) na familia za wanajeshi hao huko Bandar Abbas kusini mwa Iran.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa kuwepo jeshi la Majini la Iran katika pwani ndefu ya Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman na kuwepo kistratijia jeshi hilo katika maji huru ya kimataifa ni ishara ya heshima ya taifa la Iran, nguvu ya Mfumo wa Kiislamu na heshima ya mataifa ya eneo hili. Amesisitiza juu ya udharura wa kuwa macho mbele ya njama za maadui za kutaka kudhoofisha uwezo wa kitaifa na akawataka wananchi wote hususan viongozi, makundi na mirengo mbalimbali ya kisiasa, kaumu na madhehebu tofauti kuwa na umoja na mshikamano na kujiepusha na hitilafu na migawanyiko.
Ayatullah Khamenei ameeleza kufurahishwa kwake na kukutana na wafanyakazi wa Jeshi la Majini na familia zao na akawashukuru kwa huduma na kazi zao nzuri. Amesema kuwepo kwa nguvu zote Jeshi la Majini na Sepah na familia za wanajeshi katika pwani ya kuanzia mashariki mwa Bahari ya Oman hadi magharibi kabisa mwa pwani ya Ghuba ya Uajemi ni dhihirisho la azma kubwa ya kulinda heshima na uwezo wa taifa la Iran.
Amezungumzia pia nafasi ya kistratijia ya Jeshi la Majini na Sepah na akasema, kuwepo jeshi la Iran kwa nguvu zote katika maji huru pia ni ujumbe wa heshima ya mataifa ya eneo hili, kwani kunaonyesha kwamba taifa la Iran limeweza kufikia kiwango cha juu cha nguvu na maendeleo katika kukabiliana na kambi kubwa ya maadui kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu Mtukufu na kujiamini, licha ya kuwa peke yake.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, kuwepo huko kwa jeshi la Iran katika maji huru ambako ni matokeo ya juhudi na jitihada kubwa za makamanda, askari wa Jeshi la Majini, Sepah na familia zao, ni huduma kwa jamii ya mwanadamu.
Ameongeza kuwa kutokana na kusimama imara juu ya misingi yake na kudumisha harakati yake bila ya kupotoka, taifa la Iran limethibitisha kwamba njia ya azma ya kitaifa na kujitawala kwa mataifa mbalimbali haiwezi kufungwa, na iwapo taifa lolote litaamua, basi hapana shaka kwamba linaweza kupata heshima, nguvu na utajiri kama lilivyo taifa la Iran.
Akiashiria mbinu mbalimbali zinazofanywa na maadui kwa ajili ya kuzusha hali ya kukata matumaini katika mataifa na kudhoofisha irada na azma yao ya kitaifa, Ayatullah Khamenei amesema miongoni mwa mbinu hizo ni pamoja na kusambaza dawa za kulevya kati ya watu wa mataifa hayo kwa malengo ya siri ya kisiasa na kuchochea hitilafu za ndani. Amesema kuwa miongoni mwa mbinu zinazotumiwa na maadui kudhoofisha irada na azma ya kitaifa ni kuzusha hitilafu miongoni mwa kaumu na madhehebu mbalimbali, kati ya mirengo na makundi ya kisiasa na kati ya jumuiya na asasi tofauti; hata hivyo taifa la Iran limeshinda njama na hila hizo zote za maadui na hapana shaka kwamba kufanyika kikao cha askari wa Jeshi la Majini, Sepah na familia zao ni mfano wa umoja na mshikamano mkubwa uliopo katika taifa la Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria aya 103 ya suratu Aal Imran inayosema: "Na shikamaneni na kambi ya Mwenyezi Mungu nyote wala msifarikiane.." na akasema maneno haya ya Mwenyezi Mungu yanawalenga wananchi wote wa taifa la Iran hususan viongozi, makundi na mirengo mbalimbali ya kisiasa, kaumu na madhehebu tofauti. Amesema, wananchi wote wanapaswa kulitambua suala la kujiepusha na hitilafu kuwa ni wajibu wao wa kidini na kitaifa kwa kushikamana na kamba ya Mwenyezi Mungu.
Ayatullah Khamenei amesema, vishawishi vya dunia, matamanio na hawaa ya nafsi, husuda, ubahili, vinyongo na uchu wa madaraka ni mithili ya kinamasi, na njia pekee ya kuokoka maangamizi hayo ni kushikamana kwa pamoja na kamba ya Mwenyezi Mungu.
Ameashiria pia mapinduzi makubwa ya taifa la Iran na pande nyingine ambazo hadi sasa hazijaeleweka vyema za harakati hiyo adhimu na akaongeza kuwa: "Katika kipindi chote cha miaka 33 iliyopita taifa la Iran limesonga mbele kwa imani, umoja na maarifa na kumuacha nyuma adui licha ya njama na mashinikizo yote ya ubeberu wa kimataifa na vibaraka wake."
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza juu ya udharura wa kudumishwa moyo wa kusimama kidete na kutoondoka nje ya njia asili ya Mapinduzi ya Kiislamu. Amesema kuwa njia pekee ya uokovu wa mataifa ya eneo hili ni kupiga hatua katika njia hii ambayo athari zake nzuri zinaendelea kuonekana wazi.
Amezungumzia pia propaganda za uongo za madola ya kigeni dhidi ya taifa la Iran na Uislamu na juhudi zao za kupotosha ukweli na akasema: "Mfano wa propaganda hizo chafu za Magharibi unaonekama katika jinai iliyofanyika hivi karibuni katika mojawapo ya nchi za Ulaya kaskazini ambapo baada tu ya jinai hiyo zimefanyika njama za kuwatuhumu Waislamu kuwa ndio waliohusika na uhalifu huo; hakika suala hili linadhihirisha uhabithi na orongo wa propaganda za Wamagharibi."
"Propaganda na tuhuma kama hizo hazitakuwa na taathira yoyote kwa irada na azma ya taifa la Iran na mataifa mengine ya Kiislamu" amesisitiza Kiongozi Muadhamu. Ameongeza kuwa: "Tunaamini kwamba saada na ufanisi wa duniani na akhera wa taifa la Iran utadhaminiwa chini ya kivuli cha Uislamu na harakati inayosonga mbele ya Mfumo wa Kiislamu wa Iran imepelekea kuhuishwa Uislamu na azma ya mataifa ya kanda hii."
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ametaja kazi na uchapakazi kuwa ni miongoni mwa sababu muhimu za kudumishwa harakati ya maendeleo na ustawi wa taifa la Iran. Ameongeza kuwa iwapo lengo litalindwa katika mpambano wa haki na batili, sambamba na uchapakazi, bidii, kuhudhuria kwenye medani mbalimbali na kuimarishwa zaidi hali ya kujiamini, hapana shaka kwamba kambi ya haki itaishinda batili.
Amezungumzia hali ngumu na mashaka makubwa yaliyolipata taifa la Iran katika kipindi cha vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran hususan siku za mwanzoni mwa vita hivyo na akasema kuwa katika siku za mwanzoni mwa vita hivyo ambapo baadhi ya watu walikuwa wakitoa maneno ya kukatisha moyo na matumaini, Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu) ambaye alikuwa ameshikamana na chanzo cha nuru ya Mwenyezi Mungu, alisimama kidete na kusema "tunaweza", na hatimaye "tumeweza".
Amesema, leo hii ambapo taifa la Iran limepata maendeleo makubwa na nguvu kazi adhimu ya kibinadamu tofauti na ilivyokuwa katika kipindi cha vita vya kulazimishwa, njia ya maendeleo inaweza kudumishwa kwa kuwa na moyo kama huo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewataja vijana kuwa ni dafina isiyokuwa na kifani ya taifa la Iran. Amesisitiza kuwa dafina hiyo inapaswa kuchimbwa na kutolewa ardhini ili pwani ya Mapinduzi ya Kiislamu ijae maji zaidi, na hapana shaka kwamba matarajio hayo yatatimia katika kipindi si kirefu.
Mwanzoni mwa mkutano huo Kamanda wa kikosi cha majini cha jeshi la Sepah Brigedia Jenerali Fadavi alimkaribisha Amir Jeshi Mkuu na akasema kuwepo jeshi la Sepah na majeshi ya wanamaji wa Iran wakiwa pamoja na familia zao katika pwani ya Ghuba ya Uajemi ni alama ya azma kubwa na ishara ya kuwa tayari majeshi hayo kwa ajili ya kukabiliana na tishio la aina yoyote.
830517
captcha