IQNA

Ayatullah Khamenei:

Dosari na matatizo ya umma wa Kiislamu yatafidiwa kwa kutekeleza mafundisho ya Qur'ani

14:19 - August 03, 2011
Habari ID: 2164333
Majlisi ya kiraa ya Qur'ani Tukufu imefanyika alasiri ya leo katika siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, ambao ni msimu wa machipuo wa Qur'ani, katika mahfali iliyohudhuriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamanei.
Majlisi hiyo ilitiwa nuru na hali ya kimaanawi kwa kiraa ya makarii, mahafidhi na walimu wa Qur'ani Tukufu na vilevile tungo za kumsifu na kumhimidi Mwenyezi Mungu SW.
Ayatullah Khamenei amehutubia majlisi hiyo na kusema kuwa kuhifadhi Qur'ani, kusoma tafsiri yake na kutafakari katika aya za kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu kutazidisha mafanikio ya Kiqur’ani ya Iran. Ameashiria uwanja mzuri na mapenzi makubwa yanayoshuhudiwa katika jamii kwa kitabu kitukufu cha Qur'ani na akasema: "Harakati ya Qur'ani hapa nchini inapaswa kudumishwa na kustawishwa kwa kiasi cha kulifanya taifa la Iran kuwa taifa imara na madhubuti kwa kuwa na watu wasiopungua milioni kumi waliohifadhi Qur'ani Tukufu.”
Amewataja vijana wanaosoma Qur'ani Tukufu kuwa ni mstari wa mbele wa harakati ya jamii kuelekea kwenye ustawi na maendeleo ya Kiqur’ani. Ameongeza kuwa iwapo kutakuwepo watu milioni 10 hadi 15 wanaotambua kwa kina maarifa ya Qur'ani hapa nchini na wakahuisha darsa, maonyo na bishara za Qur'ani katika roho, nyoyo na matendo yao, basi hali hiyo itafanikisha kazi ya kuijenga jamii kwa mujibu wa mafundisho ya Qur'ani Tukufu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja Qur'ani kuwa inadhamini mahitaji yote ya mwanadamu na ni mwongozo wa mataifa yote kuelekea kwenye saada na ufanisi wa dunia na akhera. Amesema, dosari, kubakia nyuma na matatizo ya umma wa Kiislamu vitafidiwa kupitia njia ya kuitambua na kuifanyia kazi Qur'ani.
Amesema kuwa tawala za viongozi waovu katika ulimwengu wa Kiislamu zimepelekea kupotea bure maslahi ya kiuchumi na kutoweka utambulisho wa kiutamaduni wa mataifa ya Kiislamu. Ameongeza kuwa Qur'ani ndiyo mhimili wa maendeleo ya kimaada na kimaanawi wa mataifa mbalimbali na kwamba taifa la Iran ni mfano wa wazi wa ukweli huo wa kihistoria.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema vipawa vikubwa vya taifa la Iran ni hazina kubwa ambayo serikali za watawala waovu katika zama za Kipahlavi na Kiqajar zilizuia ustawi na kuchanua kwake.
Amesema vijana wengi wenye nishati, wapenda maendeleo na wanaoipa Iran fahari na hesghima kila uchao na kupandisha juu hadhi ya nchi hii ni kielelezo cha vipawa muhimu ambavyo vimekombolewa kutoka kwenye udhibiti wa tawala za viongozi mataghuti na waovu kutokana na harakati ya taifa la Iran kuelekea kwenye Qur'ani Tukufu na sasa vinaliekeleza taifa kwenye maendeleo na ustawi.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni hatua moja mbele kuelekea kwenye Qur’ani Tukufu. Ameongeza kuwa kwa baraka za harakati hiyo leo hii taifa la Iran ni miongoni mwa mataifa hai na yenye nguvu zaidi duniani na kwa baraka za kushikamana na Qur’ani, Mwenyezi Mungu SW amelipa heshima, uwezo wa kumaizi baina ya mambo na nguvu kubwa.
Ameelezea kufurahishwa na hali ya kuenea nara na matakwa ya Kiislamu kati ya mataifa mbalimbali ya Kiislamu na kusema suala hilo ni ishara ya harakati ya umma wa Kiislamu. Ameongeza kuwa kwa baraka zake Allah na kwa mujibu wa sifa za maarifa ya Qur’ani, leo hii nara na kaulimbiu za Kiislamu na Kiqur’ani zimeenea kuwa na satua na taathira kubwa zaidi huku taathira za harakati za maadui, wanafiki na vibaraka dhidi ya taifa zikiendelea kupungua.
Mwishoni mwa hotuba yake Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema anataraji kwamba harakati ya sasa ya Qur’ani hapa nchini itashika kasi zaidi siku baada ya siku na chini ya kivuli chake maarifa ya Qur’ani yatastawi na kupanuka zaidi.
Mwishoni mwa mahfali hiyo ya Qur’ani iliyoendelea kwa kipindi cha masaa manne Ayatullah Khamenei aliongoza Sala za Magharibi na Ishaa na baadaye hadhirina walifuturu pamoja na Kiongozi Muadhamu. 836319
captcha