Nabih Berry ambaye alikuwa akihutubia mkutano wa tano wa kimataifa wa kuunga mkono Intifadha na mapambano ya ukombozi ya Palestina unaofanyika mjini Tehran amesema kuhusu sababu za mashinikizo ya nchi za Magharibi dhidi ya Iran katika suala la teknolojia ya nyuklia na kunyamaza kimya nchi hizohizo mbele ya silaha za nyulia za Israel kwamba, ni wazi kuwa sababu ya misimamo hiyo ya kindumakuwili ni uungaji mkono na himaya ya Iran kwa haki na malengo ya taifa la Palestina.
Spika wa Bunge la Lebanon amempongeza Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran Ayatullah Ali Khamenei na Mwenyeiti wa mkutano huo na akasema mkutano huu unadhihirisha tena ujumbe wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na mwasisi wake hayati Imam Khomeini ambaye baada tu ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu alifungua ubalozi wa Palestina mahala pa ubalozi wa Israel mjini Tehran na akatangaza Ijumaa ya mwisho ya kila mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds.
Nabih Berry ameashiria jinai za kila uchao za utawala wa Kizayuni wa Israel na akasema kuwa anataraji kuwa mkutano wa sasa wa kuunga mkono mapambano na Intifadha ya Palestina utakuwa fursa ya kufichua zaidi jinai na ukatili wa utawala huo na kubuni njia mpya za mapambano na kusitisha uhalifu wa Israel. 870912