IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Mpango wowote wa kuigawa Palestina hauwezi kukubalika

21:47 - October 01, 2011
Habari ID: 2196784
"Palestina yote ni mali ya Wapalestina." Hiyo ndiyo nukta muhimu zaidi iliyosisitizwa mapema leo na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei katika mkutano wa tano wa kimataifa wa kuunga mkono Intifadha na mapambano ya taifa la Palestina na kubainisha stratijia ya umma wa Kiislamu kuhusu maudhui ya Palestina.
Katika mkutano huo unaohudhuriwa na viongozi wa ngazi za juu wa makundi ya mapambano ya Palestina na Lebanon, maulamaa, wasomi na wanafikra huru na wanaopigania uadilifu ulimwenguni na vilevile maspika wa mabunge ya ulimwengu wa Kiislamu, Ayatullah Khamenei ameeleza mpango wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu kadhia ya Palestina na akaongeza kuwa lengo kuu la umma wa Kiislamu ambalo ni kukombolewa Palestina yote bila ya kufumbia jicho hata shubiri moja ya ardhi hiyo ya Kiislamu, litatimia kwa njia ya subira, tadbiri, kutawakali kwa Mwenyezi Mungu na jihadi ya makundi yote ya mapambano na mataifa na nchi za Waislamu.
Ayatullah Khamenei ameitaja Palestina kati ya maudhui zinazozishirikisha pamoja nchi za Kiislamu kuwa ndiyo suala muhimu zaidi. Akifafanua zaidi sababu za uhakika huo, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: "Kughusubiwa nchi ya Kiislamu na kupewa wageni waliokusanywa kutoka nchi mbalimbali, mauaji, jinai na udhalilishaji wa kudumu dhidi ya Waislamu katika tukio hilo lisilokuwa na mfano na la kihistoria na njama za kutaka kuharibu na kubomoa kabisa kibla cha kwanza cha Waislamu na vituo vingine vya kidini vya Palestina ni sehemu ya sababu zinazoonesha kwamba Palestina ndiyo kadhia muhimu ya kwanza ya ulimwengu wa Kiislamu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa ni sime ya nchi za Magharibi katika mbavu za umma wa Kiislamu. Ameongeza kuwa serikali na jamii bandia ya Kizayuni imekuwa kambi ya kijeshi, kiusalama na kisiasa ya madola ya kibeberu kwa ajili ya kukabiliana na Uislamu na Waislamu katika eneo nyeti mno la ulimwengu wa Kiislamu, na ukweli huo ni sababu nyingine ya kulipa kipaumbele zaidi suala la Palestina.
Suala la Uzayuni kutumia ardhi iliyoghusubiwa ya Palestina kwa ajili ya kupanua zaidi ushawishi wake ulimwenguni ni sababu ya tano iliyotajwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya kuthibitisha umuhimu wa kwanza wa kadhia ya Palestina.
Amesema kuwa gharama kubwa za kifedha na kibinadamu zilizotolewa na nchi za Kiislamu hadi sasa katika suala la Palestina, mashaka yasiyoisha ya mamilioni ya wakimbizi wa Palestina, kutoweka historia ya kituo muhimu cha ustaarabu katika dunia ya Kiislamu na sababu nyingine kadhaa vinaonesha kwamba Waislamu wanapaswa kulipa kipaumbele cha kwanza suala na kadhia ya Palestina.
Baada ya kueleza sababu hizo za kiitikadi, kibinadamu, kisiasa na kihistoria, Ayatullah Ali Khamenei ametaja sababu nyingine mpya, muhimu na ya kimsingi akisema kuwa, taathira kubwa ya kadhia ya Palestina katika kujitokeza harakati kubwa ya mwamko wa Kiislamu ambayo ni mwanzo wa ukurasa muhimu katika historia ya umma wa Kiislamu, ni sababu nyingine inayodhihirisha umuhimu wa maudhui ya Palestina.
Katika uwanja huo huo, Ayatullah Khamenei amesema kuwa mwamko wa Kiislamu ambao unawezsa kuanzisha majmui moja yenye nguvu, iliyopiga hatua na yenye uwiano ya Kiislamu na ambao kwa msaada wake Allah na azma ya wafuasi wa harakati hiyo utakomesha kipindi cha kubakia nyuma, udhaifu na kudhalilishwa mataifa mbalimbali, umepata sehemu kubwa ya nguvu na hamasa yake kutoka kwenye kadhia ya Palestina.
Akieleza taathira za maudhui ya Palestina katika kujitokeza mwamko wa sasa wa Kiislamu, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria dhulma na ukandamizaji wa kila siku wa utawala wa Kizayuni wa Israel, ushirikiano wa baadhi ya watawala madikteta, mafasidi na vibaraka wa Marekani na utawala huo, mapambano yenye kutoa ilhamu na ushindi unaoshabihiana na muujiza wa vijana wenye imani katika vita vya siku 33 huko Lebanon na mapigano ya siku 22 huko Ghaza na akasema kuwa uhakika huo ni miongoni mwa mambo muhimu ambayo yamekutanisha pamoja bahari inayoonekana kidhahiri kuwa tulivu ya mataifa ya Misri, Tunisia, Libya na nchi nyingine za kieneo na kuanzisha mwamko wenye baraka wa Kiislamu.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa masuala hayo yanapaswa kutiliwa maanani katika uchambuzi wa masuala ya Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika na akaongeza kuwa usahihi au kutokuwa sahihi kwa uamuzi wowote ule kutadhihirika kwa kutiliwa maanani masuala hayo.
Akikamilisha sehemu hii ya hotuba yake katika mkutano wa tano wa kimataifa wa kuunga mkono mapambano ya Intifadha, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, maamuzi sahihi yanaonesha kwamba leo hii kadhia ya Palestina imepata umuhimu mkubwa zaidi na katika hali hii wananchi wa Palestina wana haki ya kuwa na matarajio makubwa zaidi kutoka kwa nchi za Kiislamu. Inaendelea. 870771


captcha