IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Umoja wa Kiislamu unapaswa kupewa kipaumbele zaidi katika ibada ya Hija

2:20 - October 04, 2011
Habari ID: 2198363
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu mapema leo amekutana na maafisa wanaoshughulikia Hija mwaka huu wa Iran akiitaja ibada hiyo kuwa ni fursa ya thamani kwa ajili ya kujenga mawasiliano na umma wa Kiislamu na kujifaidisha kimaanawi na kiroho.
Ayatullah Khamenei ameashiria njama zinazofanywa na maadui kwa ajili ya kuzusha hitilafu na kukabiliana na wimbi la mwamko wa Kiislamu katika msimu wa Hija na akasema, njia pekee ya kuweza kushinda njama hizo ni kukurubisha zaidi nyoyo na kuimarisha mshikamano.
Ayatullah Khamenei ameashiria pia ufisadi uliofanyika katika benki kadhaa hapa nchini na kusema kuwa sababu ya kutokea uhalifu huo ni kutotekelezwa maagizo aliyoyatoa miaka kadhaa iliyopita kuhusiana na jinsi ya kukabiliana na ufisadi wa kiuchumi. Amesisitiza kuwa viongozi wa vyombo vya mahakama wanapaswa kufuatilia kadhia hiyo kwa nguvu zote, kwa kina na kwa busara, kupasha habari kwa njia sahihi kwa wananchi na kukata mikono ya wahaini.
Ayatullah Khamenei ameitaja ibada ya Hija kuwa ni miongoni mwa nembo muhimu za Uislamu na ugeni mkubwa wa Mwenyezi Mungu katika kituo cha adhama, qudra, jamali na ukarimu. Ameongeza kuwa mahujaji wanapaswa kuimarisha mfungamano na umoja wa Kiislamu bila ya kujali utaifa, kaumu na madhehebu mbalimbali na watumie fursa hiyo kwa ajili ya kukurubisha pamoja nyoyo.
Amesema kuwa moja ya sifa makhsusi za Hija ya mwaka huu ni mwamko wa Kiislamu unaoshuhudiwa hivi sasa katika eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika hususan Misri, Tunisia, Yemen na Bahrain na akaongeza kuwa kwa kutilia maanani matukio hayo, njama za kutaka kuzusha hitilafu, mifarakano na kuchochea hisia kati ya umma wa Kiislamu zitashadidi zaidi mwaka huu na njia pekee ya kushinda njama hizo ni kukurubisha zaidi nyoyo na kuimarisha umoja na mashikamano.
Akisisitiza kuwa Waislamu ni kama mwili mmoja, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa mahujaji wa Iran wanapaswa kushiriki kwenye ibada ya Hija wakiwa na mtazamo kama huo wa kimataifa ya wayape mataifa yaliyofanya mapinduzi hivi karibuni tajiriba na uzoefu wao juu ya jinsi ya kupambana na ubeberu na maadui.
Ayatullah Khamenei amesema: “Kuwa na mwenendo mzuri unaoambatana na adabu na heshima ni miongoni mwa mambo ya dharura kwa mahujaji wa Kiirani.” Amesema kuwa ibada ya Hija ni fursa ya thamani kwa ajili ya kujisafisha na uchafu wa dunia na inakusanya majmui ya faradhi ambazo sambamba na kuthamini ibada hiyo kuna udharura wa kulinda hazina kubwa ya kimaanawi na kiroho inayopatikana kutokana na ibada hiyo.
Amewausia mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu kutayarisha nafsi zao kabla ya safari ya Hija na kuwa tayari kwa ajili ya kuwa wageni wa Mwenyezi Mungu. Amesema kuwa haji wa Kiirani anapaswa kuinua hadhi ya taifa, nchi na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mbele ya dunia kwa mwenendo wake mzuri wakati wa ibada ya Hija.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amewanasihi mahujaji kujiepusha na mienendo isiyofaa na akasema kuwa moja ya mienendo hiyo ni kiu ya kununua bidhaa masokoni wakati wa ibada ya Hija jambo ambalo mbali na kupoteza bure fedha za kigeni za taifa kwa kununua bidhaa zisizokuwa na ubora, humfanya haji apoteze fursa ya thamani ya kujipinda kwa ibada na kufaidika na masuala ya kiroho.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa ununuzi wa zawadi unapaswa kufanyika kwa kiasi cha haja na dharura. Ameongeza kuwa baadhi ya watu hufanya jambo la maana kwa kununua zawadi nzuri na zenye ubora wa juu katika masoko ya ndani ya Iran kabla ya safari ya Hija ili watumie vizuri wakati mwingi zaidi wa siku za ibada ya Hija kwa ajili ya masuala ya kimaanawi na kiroho.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amemalizia sehemu hii ya hotuba yake kwa kusisitiza kuwa: “Maarifa ya kidini, Qur’ani, Suna na Ahlul Bait ni rasilimali zetu za kiroho ambazo iwapo zitatumiwa vyema basi zitatayarisha uwanja mzuri wa maendeleo na ufanisi; na iwapo mwanadamu atajiweka mbali na rasilimali hizo, atapata madhara.”
Ayatullah Ali Khamenei ameendelea na hotuba yake kwa kuashiria maagizo yake aliyoyasisitiza mbele ya viongozi wa taifa miaka kadhaa iliyopita hususan amri yake iliyotolewa miaka kumi iliyopita kwa ajili ya kupambana na ufisadi wa kiuchumi na akasema, japokuwa viongozi wa nchi walilikaribisha suala la kupambana na ufisadi wa aina hiyo lakini kama maagizo hayo hangefanyiwa kazi, basi ufisadi kama huu wa kibenki usingeweza kushuhudiwa hapa nchini.
Amesema kuwa matukio kama haya yanazishughulisha fikra na akili na wananchi na kuziumiza nyoyo za wengi miongoni mwao. Ameongeza kuwa si sawa kuwaumiza wananchi au hata kuwavunja moyo baadhi yao kutokana na uzembe wa baadhi ya maafisa.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa: “Tokea miaka kadhaa iliyopita ilisisitizwa juu ya kupambana na ufisadi kabla haujaota mizizi, kwani iwapo muda utapita itakuwa vigumu mno kung’oa mizizi yake na mwishowe kuwavunja moyo wawekezaji wema na wakweli; hata hivyo inasikitisha kwamba maagizo haya hayakutekelezwa.”
Ayatullah Khamenei amewahakikishia wananchi kuhusu azma thabiti ya vyombo vitatu vikuu vya dola ya kushughulikia ipasavyo tukio hilo na kuzuia matukio mengine kama hayo na akasema kuwa kuna baadhi ya watu wanaotaka kutumia kadhia hiyo kwa ajili ya kuwahusisha viongozi wa nchi ilhali viongozi wa Serikali, Bunge na Idara ya Mahakama wanajishughulisha na uchapakazi na kutekeleza majukumu yao.
Akiashiria mwenendo wa upashaji habari kuhusu kadhia hiyo, Ayatullah Khamenei amesema kuwa vyombo vya habari havipaswi kuendeleza makelele kuhusu suala hili na vinalazimika kuwapa viongozi husika fursa ya kuchunguza kadhia hiyo kwa kutumia busara, tadbiri na kwa umakini na nguvu zote.
Amesema kuwa kudumishwa makelele kama hayo hakuna maslahi yoyote hususan pale baadhi ya watu wanapotaka kutumia vibaya suala hili, hivyo pande zote zinapaswa kuwa macho.
Ayatullah Khamenei amesema: “Wananchi wanapaswa kuwa na matumaini kwamba kadhia hii itafuatiliwa na viongozi hadi mwisho na kukata mikono na waliofanya hiana.”
Ameviusia pia Vyombo vya Mahakama kuwapasha habari wananchi kuhusu ufuatiliaji wao wa faili hilo na ameitaka idara hiyo kutowaonea huruma watenda maovu, waharibifu na mafisadi.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, mwakilishi wa Faqihi Mtawala na kiongozi wa msafara wa Hija wa Iran Hujjatul Islam Walmuslimin Qadhi Askari alitoa ripoti kuhusu maandalizi na shughuli za Hija ya mwaka huu na pia kazi zilizofanyika kwa ajili ya kufanikisha ibada hiyo.
Vilevile Mwenyekiti wa Jumuiya ya Hija na Ziara ya Iran Bwana Layali alitoa ripoti kuhusu hatua zilizochukuliwa na kusema kuwa mwaka huu Wairani elfu 97 wataelekea katika miji mitukufu ya Makka na Madina wakiwa katika misafara 588 na kutumia makampuni mawili ya ndege ya Iran. 872543
captcha