IQNA

Wimbi la tatu la watu kuelekea kwenye Uislamu limeanza

12:26 - October 13, 2011
Habari ID: 2204167
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei amesema kwamba wimbi la tatu la watu kuelekea kwenye dini ya Kiislamu linashuhudiwa sasa katika maeneo mbalimbali.
Ayatullah Khamenei aliyasema hayo usiku wa kuamkia leo katika kikao cha maulamaa na wanazuoni wa Kisuni na Kishia wa mkoa wa Kermanshah magharibi mwa Iran na kuongeza kuwa harakati za wananchi katika Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika na kukatishwa tamaa wananchi wa Magharibi na mfumo wa kibepari kumeanzisha wimbi la tatu la watu kuelekea kwenye dini tukufu ya Kiislamu. Ameongeza kuwa katika mazingira haya wanazuoni wa Kiislamu wanapaswa kujizatiti kwa silaha ya elimu na masuala ya kiroho ili waweze kueneza dini ya Kiislamu kwa kutumia kitabu cha Qur'ani na Suna kwa njia ya busara na inayofahamika kwa kizazi cha sasa.
Akigawa mawimbi ya watu kuelekea katika dini ya Kiislamu dunia kote katika sehemu tatu, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema wimbi la kwanza la watu kuelekea kwa wingi katika dini tukufu ya Kiislamu lilianza sambamba na kipindi cha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na wimbi la pili lilianza baada ya kushindwa mfumo wa utawala wa kimaxi.
Amesema kuwa hii leo ambapo utabiri wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu kusambaratika mfumo wa Kimaxi umetimia na utabiri wa kusambaratika mfumo wa kibepari unaelekea kutimia, maulamaa na wanazuoni wa Kiislamu wanapaswa kutangaza maarifa ya kimantiki na yenye misingi madhubuti ya Uislamu kwa watu wenye kiu kote duniani kwa kutumia misingi imara ya kiakili inayonasibiana na mahitaji ya zama hizi.
Ayatullah Khamenei amesema ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na ushindi wa mapinduzi makubwa zaidi katika kipindi cha sasa huko Misri ni miongoni mwa matukio ambayo yalionekana kidhahiri kuwa ni muhali. Ameongeza kuwa maulamaa wa Kiislamu wanapaswa kuwa na malengo makubwa katika kulingania dini na wakati wanatekeleza majukumu yao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema wapinzani wanatumia mbinu na njia mbalimbali za kisasa kuuhujumu Uislamu na kuzusha tashwishi katika fikra za vijana na kuna udharura wa kutumia mbinu na njia zinazonasibiana na mahitaji ya kizazi cha vijana katika kukabiliana na mbinu hizo.
Ayatullah Khameni amesisitiza kuwa mbinu nyingine inayotumiwa na maadui kwa ajili ya kudhoofisha Uislamu ni kuzusha hitilafu kati Waislamu wa Kishia na Kisuni. Ameongeza kuwa maulamaa wa Kishia na Kisuni wanapaswa kuwa macho mbele ya njama hizo na kutafuta njia za kupambana na njama hizo kwa kuitisha vikao vya pamoja na kushirikiana. 879046
captcha