IQNA

Bendera ya Uislamu itapepea katika eneo zima la Mashariki ya Kati

22:27 - October 15, 2011
Habari ID: 2205295
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kukana utambulisho wa Kiislamu wa taifa shujaa la Iran na kutaka kuitenga Jamhuri ya Kiislamu ndilo lengo muhimu zaidi la hujuma ya siku zote ya kambi ya ubeberu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei leo akiwa katika siku ya nne ya safari yake katika mkoa wa Kermanshah huko magharibi mwa Iran, amehutubia umati mkubwa wa wananchi wa eneo la Gilan Magharibi. Ayatullah Khamenei amelitaja taifa la Iran hususan vijana kuwa ni walinzi wa mipaka ya utambulisho, heshima na hadhi ya kitaifa na kidini. Ameashiria pia tuhuma zilizotolewa siku chache zilizopita na Marekani ikiihusisha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na ugaidi na akasema: "Adui anafanya kila liwezekanalo kwa ajili ya kulitenga taifa la Iran na kueneza hofu kuhusu Iran, lakini njama hizo hazitakuwa na natija ghairi ya chuki zisizokuwa na kikomo za mataifa mbalimbali dhidi ya Marekani na kuongezeka mapenzi na uungaji mkono wa wanadamu kwa nara na kaulimbiu za taifa la Iran."
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa kusimama kidete wananchi wenye ghera na azizi wa mji wa Gilan Magharibi katika kipindi cha hujuma ya utawala wa Kibaathi wa Saddam Hussein dhidi ya Iran ni fahari kubwa kwa vijana wa eneo hilo. Ameashiria safari zake za huko nyuma katika eneo la Gilan Magharibi na maeneo ya kandokando yake katika kipindi cha miaka minane ya vita vya kulazimishwa na akasema kuwa vijana wa eneo hili wanapaswa kuelewa kwamba wamelelewa katika familia zinazojifaharisha kwa ushujaa, ujasiri na ghera ya kulinda taifa, suala ambalo ni ishara ya kuwepo nyanja nyingi za kiroho na kibinadamu.
Ayatullah Ali Khamenei amesema, kipindi cha sasa ni kipindi cha vita vitakatifu vya kutetea utambulisho, heshima ya taifa na itikadi madhubuti za Kiislamu. Amesema, wavulana na wasichana wote vijana na wanawake na wanaume wenye imani ambao hawakuwepo wakati wa vita vya kujitetea kutakatifu, sasa wanapaswa kutoa mchango mkubwa katika medani ya kulinda heshima na hadhi kubwa ya taifa kwa moyo ule ule wa kitaifa.
Amesema kuwa kuhifadhi kumbukumbu nzuri za kipindi cha vita vya kujitetea kutakatifu ni miongoni mwa sababu za kulindwa utambulisho wa taifa. Amemsifu mwanamke Muislamu na shujaa wa Gilan Magharibi ambaye katika kipindi hicho cha vita vya kujitetea kutakatifu aliangamiza na kuteka idadi kadhaa ya askari wa Saddam Hussein na akasema kuwa, kulindwa kumbukumbu za kusimama kidete wananchi wa Gilan Magharibi, Qasre Shirin, Islamabad, Sarepole Zohab na maeneo mengine hapa nchini kuna umuhimu mkubwa unaopaswa kuzingatiwa na shakhsia wakubwa, wasomi, wanaharakati na wanafikra.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kukana utambulisho wa Kiislamu wa taifa shujaa la Iran na kutaka kuitenga Jamhuri ya Kiislamu ndilo lengo muhimu zaidi la hujuma ya siku zote ya kambi ya ubeberu. Ameongeza kuwa, Marekani, Ulaya na nchi tegemezi kwao zinafanya kila liwezekanalo na kujiumiza kwa ajili ya kuvunja mapambano ya taifa la Iran, na suala hili linaonyesha thamani ya kihistoria ya kusimama kidete taifa hili azizi.
Ayatullah Khamenei ameyataja makelele ya kipropaganda ya siku kadhaa za hivi karibuni ya vyombo vya habari vya kanali ya Uzayuni wa kimataifa ya kuihusisha Iran na ugaidi kuwa ni sehemu ya njama za mara kwa mara za viongozi wa kiimla duniani. Ameongeza kuwa, kwa kutoa tuhuma hizo zisizokuwa na maana wala mashiko dhidi ya Wairani kadhaa, wamefanya jitihada za kutafuta kisingizio na kuihujumu kipropaganda na kisiasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa inaunga mkono ugaidi, lakini njama hizo zimeambulia patupu na hazitakuwa na athari yoyote kama zilivyokuwa njama zao za huko nyuma; na kinyume na fikra zao, njama hizo zitawafanya watengwe zaidi.
Akiashiria matukio ya kieneo na dunia ya sasa, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja utawala wa Marekani kuwa umetengwa na ndio unaochukiwa zaidi na watu duniani. Ameongeza kuwa, miaka miwili iliyopita Rais wa sasa wa Marekani alitoa maneno ya kujikomba na kujipendeleza akiwa nchini Msri kwa shabaha ya kuzihadaa fikra za watu, lakini hii leo wananchi wa Misri na nchi nyingi za Mashariki ya Kati wanatoa nara na maneno yanayoilaani Marekani.
Ameashiria pia jinsi Rais wa Marekani anavyowaogopa wananchi wa Mashariki ya Kati na kusema: "Hata wakati wa safari yake katika nchi ya Afghanistan inayokaliwa kwa mabavu na jeshi la Marekani na NATO, kiongozi huyo hakutoka nje ya kituo cha jeshi la anga cha Bagram na hakuwa na ujasiri wa kwenda Kabul kwa sababu ametengwa na mataifa na anayaogopa."
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria wimbi kubwa la harakati ya Wall Street linaloenea kwa kasi katika miji mbalimbali ya Marekani na akawaambia viongozi wa nchi hiyo kwamba: "Mumetengwa hata katika taifa lenu wenyewe na mnawaogopa wananchi waliowengi, na wakati huo huo mnataka kueneza fikra ya kuwatisha watu na Iran kwa kutumia maneno ya kipuuzi?"
Ayatullah Khamenei amelipongeza taifa la Iran kwa kusimama kidete na akawahutubu viongozi wa kambi ya ubeberu akiwaambia kwamba: "Eleweni kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono na kutetea mataifa yanayodhulumiwa, inapambana na kuwapinga madhalimu na itaendelea kusimama kidete kwa nguvu zote kupambana na dhulma zenu na wala haitalegeza kamba hata kidogo katika thamani zake."
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria mapenzi na uungaji mkono mkubwa wa mataifa mbalimbali kwa nara na kaulimbiu za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na akasema kuwa, mkabala wa mapenzi na uungaji mkono huo unaoongezeka siku baada ya siku, viongozi wa Marekani hawana waungaji mkono isipokuwa idadi ndogo ambao ni sawa na asilimia moja tu, na ukweli huu unakabiliana na nafasi adhimu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Amewausia vijana hapa nchini kuthamini nafasi na uwezo huo mkubwa na akasema kuwa nchi hii ni mali ya vijana azizi wa Iran, na kizazi cha vijana kinalazimika kujitayarisha kwa ajili ya mustakbali unaong'aa wa Iran kwa kushiriki kwa wingi katika medani za sayansi na teknolojia na nyanja nyingizo na kupambana kwa uangalifu mkubwa na satua na ushawishi wa adui.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia pia kasi ya kuenea harakati ya Kiislamu katika eneo muhimu sana la Mashariki ya Kati na akasema kuwa, vijana werevu wa Iran wanapaswa kuulinda Uislamu ambao ndio sababu ya uokovu wa kimaada na kiroho, kwani hakuna shaka yoyote kwamba mustakbali ni wa Uislamu, na kwa matakwa yake Allah bendera ya Uislamu itapepea katika kanda hii yote na kuunda majmui yenye nguvu, umoja na heshima ya mataifa ya eneo hili.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Khamenei amesema kuwa kiwango cha watu wasiokuwa na ajira katika mkoa wa Kermanshah bado kiko juu na serikali inalazimika kutumia suhula na uwezo wake wote kwa ajili ya kutatua matatizo ya mkoa huo.
Mwanzoni mwa mkutano huo, Imam wa Swala ya Ijumaa ya mji wa Gilan Magharibi amemkaribisha Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mji huo na kutoa ripoti fupi kuhusu historia ya mapambano ya wakazi wa eneo hilo na kujitolea kwao katika kipindi cha vita vya kujitetea kutakatifu. 880033



captcha