IQNA

Ayatullah Khamenei:

Wamagharibi wanamdunisha mwanamke

10:16 - January 05, 2012
Habari ID: 2251640
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa mtazamo wa Magharibi kuhusu mwanamke ni upotufu, udhalilishaji mkubwa na dharba kwa utukufu wa mwanamke.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo usiku wa kuamkia leo katika kikao cha tatu cha Fikra za Kistratijia kilichowakutanisha pamoja wanafikra na wahadhiri wa vyuo vikuu ambacho kimejadili maudhui ya mwanamke na kuongeza kuwa, hata mafeministi wenye misimamo mikali zaidi wanatoa pigo kubwa kwa mwanamke, tofauti kabisa na wanavyodhania wao; kwani wanamfanya mwanamke kuwa chombo tu cha kushibisha matakwa ya ngono ya watu kupitia njia ya kumpoteza. Amesema, inasikitisha kuwa suala hilo limekuwa jambo la kawaida na linalokubalika katika fikra za waliowengi huko Magharibi.
Ayatullah Khamenei amesema suala la kufanywa mwanamke kuwa moja ya misingi ya hujuma ya kisiasa na kipropaganda ya maadui dhidi ya utawala wa Kiislamu wa Iran ni sababu muhimu ya kutiliwa maanani kikamilifu kadhia ya mwanamke. Ameongeza kuwa tunapaswa kuzuia malengo ya wapangaji wa siasa na sera wa Kimagharibi katika hujuma yao dhidi ya misingi ya Uislamu kuhusu mwanamke kupitia njia ya kuelimisha na kuzindua fikra za walimwengu.
Ayatullahil Udhmaa Ali Khamenei amesema mtazamo wa Uislamu kuhusu mwanamke ni wa hali ya juu kabisa. Amesisitiza kuwa katika mtazamo wa kimsingi wa Uislamu, mwanamke hatofautiani na mwanaume katika ubinadamu, na kwa mujibu wa aya za Qur'ani Tukufu, mwanamke na mwanaume wako sawa kabisa katika njia ya kuelekea kwenye ukamilifu na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu.
Ameashiria ujanja wa Wamagharibi wa kujiepusha mjadala wa masuala ya familia na akasema kuwa, Wamagharibi wanazungumzia mno masuala ya mwanamke lakini wanakwepa kabisa kadhia ya familia, kwa sababu mjadala kuhusu familia ni miongoni mwa nukta za udhaifu wao mkubwa.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema suala la jinsia ya mtu si jambo muhimu katika mtazamo wa Uislamu. Ameongeza kuwa suala la jinsia ya mtu huwa na maana katika mwenendo wa maisha lakini halina taathira yoyote katika nafasi ya mwanamke na mwanaume katika Uislamu.
Amesema kuwa mchango na nafasi ya wanawake katika utawala wa Kiislamu wa Iran ni nzuri sana na isiyokuwa na mbadala. Amesema wanawake wamekuwa na mchango na nafasi kubwa na isiyokuwa na mbadala katika kipindi cha mapambano, ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, baada ya ushindi wa mapinduzi hayo hususan katika kipindi kigumu mno cha vita vya kujitetea kutakatifu na katika nyanja mbalimbali. Amesisitiza kuwa nafasi hiyo haiwezi kupimwa kwa kipimo cha ina yoyote.
captcha